Ijumaa, 26 Aprili 2019

RC AYOUB- ATAKA MUUNGANO ULINDWE NA KUTHAMINIWA.



 MKUU wa Mkoa wa Mjini na Magharib Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud akiwahutubia Vijana wa UVCCM Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu katika Bonanza la kuadhimisha miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika Maisara Zanzibar.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Ndugu Mussa Haji Mussa akitoa maelezo juu ya Bonanza hilo.

 MATEMBEZI ya UVCCM kupitia Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Mhe.Ayoub Mohamed.

 WASHIRIKI wa matembezi hayo ambao ni Vijana wa UVCCM kupitia Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu wakifanya mazoezi ya kunyoosha viungo mara baada ya Matembezi katika Viwanja vya Maisara.

 WASHIRIKI wa matembezi hayo ambao ni Vijana wa UVCCM kupitia Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu wakicheza Mpira wa Nage.







VIJANA nchini wametakiwa kujitathimini na kujipima kifikra juu ya mwenendo wao wa uzalendo kama unaenda sambamba na dhamira ya Waasisi wa Muungano wa Serikali mbili ya Zanzibar na Tanganyika.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharib Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud wakati akiwahutubia Vijana zaidi ya 700 katika Bonanza la UVCCM kupitia Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu katika maadhimisho ya Kilele cha miaka 55 ya Muungano wa Tanzania, huko katika Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.

Amesema ni muda wa Vijana wa sasa kujipanga vizuri kwa kuendeleza mema yaliyoasisi na Waasisiwa wa Muungano huo ambao ndio chimbuko la maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Ameongeza kuwa lengo la Muungano huo ni kuhakikisha Ulinzi na Usalama wa Nchi zote mbili unaimarika sambamba na kukua kwa Uchumi.

Ameeleza kwamba dhamira ya Wazee walioasisi Muungano huo waliamini kwamba maendeleo ya Nchi yoyote Duniani yanapatikana baada ya kuwepo kwa Amani na Utulivu ya kudumu.

Katika maelezo yake Mhe.Ayoub,amesema ni wajibu wa kila kijana kulinda Muungano huo, uliobeba mafanikio na matumaini ya Mamilioni ya Watanzania.

Amesema wapo baadhi ya Watu wanaopotosha juu ya Muungano kwa kudai hauna maslahi hali ya kuwa wao wananufaika na fursa mbali mbali zinazopatika katika Muungano huo.  

"Vijana nakuombeni tuendelee kuwa Wamoja katika kulinda Muungano huu ili Nchi zetu ziendelee kustawi Kiuchumi,Kisiasa na Kijamii", amesema RC Ayoub.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Ndugu Mussa Haji Mussa amesema lengo la Matembezi hayo ni kuunga mkono juhudi za Waasisi waliobuni jambo la kimaendeleo la kuanzisha Muungano, kama Chombo rasmi cha kulinda maslahi ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'B' Mhe.Rajab Ali Rajab, amewataka Vijana Wasomi kuwa Mabalozi wazuri wa kuelimisha Jamii juu ya faida zilizopatikana katika kipindi cha miaka 55 ya Muungano huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu ya UVCCM Zanzibar Ndugu Masoud Shibli Makame amesema katika Sekta ya Elimu Vijana wa Zanzibar wananufaika na fursa ya Mikopo miwili ya Elimu ya Juu hatua inayochochea upatikanaji wa Wasomi wengi Nchini. 

Bonanza hilo limetanguliwa na Matembezi ya Vijana zaidi ya 700 kutoka Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na UVCCM wa Mikoa mbali mbali ya Zanzibar sambamba kuchezwa Michezo mbali mbali ikiwemo Mpira wa Nage,Mpira wa Miguu na kuvuta kamba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni