Jumapili, 7 Aprili 2019

RAIS WA Z'BAR ALHAJ DK.SHEIN AONGOZA HITMA YA KUMUOMBEA DUA MAREHEMU KARUME,DKT.BASHIRU,DK.MABODI NA RC AYOUB WANENA.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akiwa na Viongozi mbali mbali wa SMT na SMZ katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Zanzibar iliyofanyika leo Afisi kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.

 BAADHI ya Viongozi na Wananchi mbali mbali wakiwa katika maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika ofisi ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wa serikali,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Aboud Mohamed Aboud,Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma Saadalla na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud.

Pia viongozi mbali mbali wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania bara, wabunge,wawakilishi, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, wananchi kutoka maeneo mbali mbali na mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ya kumuombea dua marehemu mzee Abeid Amani Karume ambayo ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya mashujaa Zanzibar (Karume Day) ilitanguliwa na kisomo cha kur-ani iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.

sambamba na kisomo hicho chenye mnasaba na kumbukumbu ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume,  Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amesema kuna kila sababu ya kumuombea dua kiongozi huyo na mashujaa wenzake ili MwenyeziMungu awafanyie wepesi na awaruzuku pepo ya juu kutokana na mema waliyoyafanya.

Ameeleza kuwa Marehemu Mzee Karume aliasisi amani na utulivu wa Nchi na kuiweka Zanzibar katika misingi ya kimaendeleo kwa ajili ya Wananchi wote.

Ametoa Wito kwa wananchi waendelee kulinda amani ya nchi ili kutoa fursa pana kwa Serikali kutoa huduma bora na endelevu kwa jamii.

Sheikh Soraga alimtaja Rais wa Zanzibar Dk.Shein kuwa ni kiongozi mchapakazi anayeendeleza kwa vitendo urithi wa maendeleo ulioasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka ifikapo Aprili 7, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa ofisi ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini za kiislamu na kikristo nchini.

 Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aliyeweka shada la maua kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Mzee Abdallah Rashid Abdallah aliweka shada la maua akiwawakilisha wazee.

Wengine walioweka mashada ya maua ni Meja Jenerali Sharif Sheha Othman aliyeweka kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Balozi Ali Karume aliweka kwa niaba ya familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Jorge Augusto Menezes aliyewawakilisha Mabalozi wenzake waliopo hapa nchini.

Aidha, mama Mwanamwema Shein aliungana na akina mama wengine katika hitma hiyo iliyofanyika katika Ofisi hiyo Kuu ya CCM Kisiwandui, akiwemo mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Mara baada ya kumalizika kwa tukio hilo, Rais Dk. Shein alipata fursa ya kufanya mahojiano mafupi na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa marehemu mzee Karume aliweka misingi ya utawala bora katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ataendelea kukumbukwa kwa mengi aliyoyafanya.

Mapema Akizungumza katika Dua hiyo Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally, amewataka viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali kufuata nyayo za kiuongozi zilizoasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Karume.

Ameeleza kwamba Shujaa huyo wa Kimapinduzi aliongoza Zanzibar kwa wakati mfupi lakini mambo aliyoyaasisi hayatoweza kufutika katika maisha na mioyo ya Wanzania na Wazanzibar kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma Mabodi amesema njia pekee ya kuenzi kwa vitendo mema yaliyotekelezwa na Mzee Karume ni wananchi kuwa na mshikamano na umoja wa kweli katika kuthamini masuala mbali mbali ya kimaendeleo yanayotekelezwa na Serikali.

Akizungumzia masuala mbali mbali yaliyoasisiwa na Mzee Karume,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira katika Serikali ya Awamu ya Tano Mhe.January Yusuph Makamba amesema muungano wa Nchi mbili za Tanzania Bara na Zanzibar ambao ni miongoni mwa muungano wa kihistoria Duniani ni sehemu ya Matunda ya Mzee Karume.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema huwezi kutaja mafanikio ya Zanzibar pamoja na harakati za ukombozi wa nchi za Afrika usimtaje Mzee Karume aliyejitolea kuikomboa nchi ili kusimamisha haki kwa wananchi.

Aprili 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 47 tokea utokee msiba huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni