Jumamosi, 13 Aprili 2019

NDG.TUNU: ATAKA JAMII KUWA KARIBU NA WATOTO WA KIKE, ATANGAZA DONGE NONO KWA MAKATIBU WA WILAYA.

 Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akiwahutubia Wanawake wa UWT Wilaya ya Dimani  pamoja na viongozi mbali mbali wa CCM na jumuiya zake .

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kufuatilia mienendo ya watoto wa kike ili wapate malezi bora yatakayowaepusha na changamoto za udhalilishwaji wa kijinsia.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) anayefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa Kamati tekelezaji ya UWT Wilaya ya Dimani kichama.

Amesema wazazi,walezi na jamii kwa ujumla inatakiwa kuwa karibu na watoto wa kile ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira hatarishi ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji vinavyopelekea kuwakosesha haki zao za msingi zikiwemo elimu,uongozi na haki ya kuishi huru.

Amesema wazazi wahakikishe watoto kila wanapotoka kwenda skuli na sehemu zingine za kijamii wakaguliwe mikoba yao kwani wengine wanaondoka na nguo za ziada na kwenda sehemu za starehe hali inayopelekea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Ameeleza kuwa jukumu la malezi ya watoto ni jukumu la kila mtu hivyo pindi watoto wakionekana katika mazingira hatari wananchi wa mtaa husika wanatakiwa kuchukua hatua za kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi ama kwa wazazi husika.

Amebainisha  kwamba kuna baadhi ya wanaume wasiokuwa na maadili mazuri wamekuwa ni chanzo cha kuwadanganya na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji watoto wa kike hasa wanaosoma shule za maandalizi na msingi,jambo ambalo ni kinyume na mila,desturi na utamaduni wa kizanzibar.

Naibu Katibu Mkuu huyo Tunu, amesema CCM kupitia UWT Zanzibar itaendelea kulaani vitendo vyote visivyofaa vinavyokatisha malengo ya maendeleo ya wanawake nchini na kuishauri serikali ichukue hatua stahiki kwa wahalifu wote wa matukio ya udhalilishaji.

Akizungumzia uimarishaji wa CCM Tunu, amewataka Wanawake hao kulipa ada za uanachama kwa wakati ili kurahisisha mipango ya kiutendaji ya Chama na Jumuiya kwa ujumla.

"Juzi Katibu Mkuu wetu bi.Queen Mlozi alininongoneza kuwa kuna mpango wa kuwapatia zawadi ya shilingi milioni moja (Sh.1,000,000),Katibu yeyote wa jumuiya ambaye Wilaya yake itaongoza kwa kulipa ada na kuongeza wanachama wapya kwa hiyo kazi kwenu", amewambia akina mama hao.

Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao,aliwasihi kuendelea kuongeza wanachama wapya na waliotimiza umri wa kupiga kura kisheria kwa lengo la kuongeza Jeshi la ushindi la CCM, litakalopambana vita ya kisiasaa na kukiletea ushindi Chama mwaka 2020.

Pamoja na hayo aliwataka akina mama hao kuitumia vizuri fursa ya ujasiriamali kwa kuanzisha na kuendeleza vikundi mbali mbali vya kuzalisha bidhaa za ujasiriamali ili kwenda sambamba na malengo ya serikali ya kupiga vita wimbi la umaskini na utegemezi.

"Wanawake tutaweza kufikia malengo yetu ya 50 kwa 50 endapo tutakuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mali na miradi mbali mbali ya kimaendeleo, wito wangu tuitumie vizuri fursa ya ujasiria mali itatukomboa kiuchumi",amesisita.

Katika maelezo yake Tunu, amewasihi akina mama hao kuwakaribisha wanawake waliopo katika vyama vya upinzani ambao mpaka sasa wamekosa muelekeo wajiunge na CCM ili wanufaike na siasa na demokrasia iliyotukuka.

Amewapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kasi yao ya usimamizi imara wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020. 

Pia amewashukru akina mama hao kwa mapokezi mazuri yaliyoambatana na zawadi mbali mbali ambazo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na umoja ndani na nje ya Chama na jumuiya.

Kupitia ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo amepokea mamia ya wanachama wapya kutoka vyama mbali mbali vya upinzani waliojiunga na CCM.

Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi, Zainab Ali Maulid amesema kuwa akina mama ndani ya Mkoa  huo wanaendelea kufanya kazi za kuimarisha CCM ili itimize malengo yake ya kuendelea kuongoza dola.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani ndugu Hussein Ali Mjema 'Kimti' ameeleza Chama kitaendelea kuwa karibu na jumuiya zote kwa lengo la kuongeza nguvu ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo.

Katika risala yao iliyosomwa na Kaimu Katibu wa UWT Wilaya ya Dimani Fatma Ramadhan Mandoba, amesema wanawake katika wilaya hiyo wameendelea kujikusanya pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.

kupitia risala hiyo waliwashukuru baadhi ya Wabunge na Wawakilishi wa viti Maalum  Wilaya hiyo waliotoa vitendea kazi mbali mbali vya kusaidia shughuli za kiutendaji za UWT. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni