Jumanne, 16 Aprili 2019

U.W.T ZANZIBAR YAWATAKA WATOTO WA KIKE KUCHANGAMKIA FURSA YA ELIMU.


 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo akiwahutubia Wanawake wa UWT Wilaya ya Kaskazini ‘A’ katika Ofisi za Jumuiya hiyo Gamba.

 MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja akisoma taarifa ya Wilaya  hiyo kwa mgeni rasmi.

 BAADHI ya Wanawake wa UWT wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’  wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi Naibu Katibu mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo katika ziara yake ya kujitambulisha Wilayani humo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar akitoa kadi ya UWT kwa mwanachama mpya wa Umoja huo.

 BAADHI ya Viongozi mbali mbali wa UWT wakiwa katika Mkutano huo.

 WANACHAMA wapya wakila kiapo cha uanachama wa UWT na CCM mara baada ya kukabidhiwa kadi za CCM.

 MWENYEKITI wa CCM Wilaya hiyo akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika mkutano huo.



NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar  ndugu Tunu Juma Kondo amewataka watoto wa kike kuchangamkia fursa ya elimu ili kupata wasomi wanawake wenye sifa za kuwa viongozi wa kitaifa,kikanda na kimataifa.

Wito huo ameutoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa Kamati Tekelezaji ya UWT Wilaya ya Kaskazini ‘A’ huko Gamba Mkoa wa Kaskanizi Unguja, alisema elimu ndio nyenzo pekee ya kuwakomboa kiuchumi na maendeleo wanawake nchini.

Ameeleza kwamba kwa sasa watoto wa kike wanatakiwa kujengewa mazingira rafiki ya kupewa elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Amesema wanawake wanaopewa fursa mbali mbali za uongozi,utendaji na utaalamu wa fani mbali mbali katika jamii wamekuwa mfano wa kuigwa katika utendaji na uchapakazi wao hivyo hicho ni kipimo sahihi cha uadilifu uliotukuka kwa kundi hilo.

Amesema  kwamba mararajio ya UWT Zanzibar ni kuona wanawake wanajitokeza kwa wingi kushindana na wanaume katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika chaguzi mbali mbali za kisiasi zijazo kwani wanawake wengi wana sifa za kiutendaji.

Amebainisha kuwa kila mwanamke anatakiwa kuchukua hatua ya kuwalinda na kuwasimamia watoto wa kike dhidi ya vitendo vya udhalilishwaji ili waweze kutimiza malengo yao bila kukatishwa na baadhi ya watu wanaokwamisha juhudi za kundi hilo kijamii.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo ndugu Tunu, alisema anawashukru akina mama wote walioshiriki kumuombea dua na kumuunga mkono kwa kumuona anafaa kuongoza nafasi hiyo na hatimaye akateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo.

Alieleza kwamba atakuwa kiongozi na mtendaji mchapakazi anayetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na kushauriana na watu anaowaongoza ili kufikia malengo mahsusi ya jumuiya hiyo.

Amesema kuwa ni lazima viongozi na watendaji wa Umoja huo wafanye kazi kwa bidii ili kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo Jipya la mwaka 2017 inayoeleza namna CCM inavyotakiwa kushinda kwa kishindo kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Dola.

Pamoja na hayo amewataka akina mama hao kulipa ada kwa wakati ndani ya umoja huo na CCM kwa ujumla hili kulinda haki zao za kuwa wanachama hai na wenye sifa za kuchagua na kuchaguliwa.

Aidha amewasisitiza Chama ,Jumuiya na Serikali kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea maendeleo endelevu wananchi ambao ndio wenye maamuzi ya kukiweka madarakani Chama Cha Mapinduzi.
Amewashukru akina mama hao kwa ushiriki wao mzuri katika Kongamano la Kitaifa la kupongeza Dk.Shein kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM lililofanyika hivi karibuni.

Tunu amewashukru na kuwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa utendaji wao uliotukuka na wenye kuacha alama za uongozi bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika risala yao UWT Wilaya hiyo walisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaongeza wanachama wapya wa Chama na Umoja huo ili kuongeza jeshi la kufanikisha ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kupitia ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo Tunu, amewapokea wanachama wapya wa UWT 70.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni