KATIBU Mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally Kakurwa akizungumza katika Kipindi Maalum kinachozungumzia Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Zanzibar huko katika Kituo cha Radio ya Bahari FM Migombani Zanzibar. |
RAIS mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya Sita Dkt.Amani Abeid Karume(kushoto), Katibu Mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally Kakurwa(katikati) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM zanzibar Dk.Abdulla Juma mabodi(kulia). |
KATIBU Mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally Kakurwa akizungumza na Watendaji,Maafisa na Wakuu wa Idara za CCM Zanzibar. |
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Dk.Bashiru Ally Kakurwa amewataka vijana nchini kuwa mstari wa mbele kulinda kwa vitendo urithi wa fikra za kimaendeleo zilizoasisiwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema kundi hilo la vijana linatakiwa kujengewa mazingira rafiki ya kuelezwa na kurithishwa maadili,historia na itikadi yakinifu zinazotokana na harakati za miongozo ya ASP na TANU ili kupata viongozi bora na makini wa sasa kama akina hayati Karume,Nyerere na Aboud Jumbe.
Wito huo ameutoa katika Mahojiano Maalum na Kituo cha Radio ya Bahari FM kilichopo Migombani Zanzibar, wakati akizungumzia siku ya Mashujaa ya kumbukizi ya miaka 47 toka kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume.
Amesema bila Waasisi wa Mapinduzi ya Januari 12,mwaka 1964 wakiongozwa na Hayati Karume pasingekuwepo na Muungano pamoja na uhuru wa Waafrika wa Zanzibar.
Ameeleza kuwa ukweli ni kwamba Mapinduzi hayo ndio chimbuko la uhuru wa kimwili na kifikra,utu,haki za binadamu,ustawi wa kijamii na kimaendeleo pamoja na ukuaji wa Demokrasia.
Amesema miaka 47 ni umri ni mingi lakini ni muhimu kukumbushana kuwa bila jasho na damu za wanamapinduzi bado Zanzibar mpaka leo ingendelea kuwa chini ya Utawala wa Kisultani.
" Lazima tukumbushane japo kwa muda mdogo kwani miaka 47 ni mingi kwa umri lakini kwa nchi ambayo ni tegemezi na ipo katika nchi zinazoendelea ni michache sana kwani Watu waliopinduliwa bado wapo na wanatamani kurudi tena, jambo ambalo haliwezekani.",alisema Dkt.Bashiru.
Pamoja na hayo alisisitiza mambo matatu ya msingi yanayotakiwa kuzingatiwa na Vijana pamoja na makada wa CCM kuwa kwanza kutambua historia halisi ya Taifa lao, pili kusimamia misingi ya waasisi wa Taifa lao na tatu kuwa wabunifu ili waendeleze mapambano katika Mazingira Mapya ya zama za sasa za Sayansi na Teknolojia.
Dkt.Bashiru ameweka wazi kuwa ukombozi haupatikani bila ya mapambano baina ya pande mbili, hivyo CCM katika suala la Mapinduzi na Muungano ni lazima iwe imara katika kulinda upande wa kulinda historia isipotoshwe na waliopinduliwa.
Amesema CCM ambayo imeshinda kwa awamu ya kwanza ya ukombozi wa kisiasa ni lazima Jeshi lake ambalo ni Wanachama, Viongozi na Watendaji wasibweteke bali waendelee kuongeza nguvu za kumiliki umma na kuhakikisha upinzani unakosa sifa za kubaki katika ushindani wa kisiasa.
"Tusipojimarisha vizuri hata haya Mapinduzi tunayoyazungumzia leo yatatuponyoka kwani mifano ipo mingi Nchi kama Somalia, na Sudan yaliwahi kuwa Mataifa huru yakawa shwari lakini leo hii katika mataifa hayo kunawaka moto.",amefafanua Katibu Mkuu huyo.
Ameongeza kuwa uwepo wa Muungano ni kwa sababu unalindwa hivyo ni muhimu kuambizana ukweli kuwa waliopinduliwa bado wapo na hawautaki muungano na wanaendelea kujenga hoja dhaifu ili muungano huo uvunjike.
Akizungumzia dhana ya Umoja uliossisitizwa na Waasisi wa Mapinduzi Dkt.Bashiru ameeleza kuwa dhana hiyo ya umoja inatakiwa kurutubishwa hasa katika kusimamia misingi ya ukweli,haki,usawa na utu.
Katika maelezo yake Dkt.Bashiru alifafanua kuwa pindi wananchi wanapoanza kudharau yale yaliyopatikana kwa jasho na damu basi panavunjwa msingi mkuu wa maendeleo.
Amesema watu wanatakiwa kupewa haki mbali mbali kama haki ya kufikri, haki ya elimu, haki ya Afya pamoja na haki ya elimu pamoja na haki ya kujitawala kama Taifa mambo ambayo toka enzi ya Katiba za ASP na TANU mpaka hivi sasa zimeanishwa vizuri katika Katiba ya CCM ya mwaka 1977 iliyoeleza namna ya haki kuzilinda na kuzisimamia haki hizo.
Amesema CCM na Serikali zake inapambana vikali na vitendo vya rushwa ambayo ndio chimbuko la kuwakosesha haki mbali mbali wananchi.
Dkt.Bashiru akizungumzia mfumo wa Vyama vingi kuwa upo Kikatiba na Kisheria na kueleza kuwa miongoni mwa faida za mfumo huo ni vyama hivyo kuchangia uwepo wa amani na utulivu.
Amesema Chama Cha Mapinduzi hakikukurupuka kukubali mfumo huo bali kiliamini kuwa vyama hivyo vitakuwa na imani ya kisiasa,kushindanisha imani hizo na mikakati ili kupata Taifa bora na imara kwa nyanja zote hatua ambayo bado haijafikiwa.
Pamoja na hayo alipongeza kasi ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwa kueleza kuwa ameridhishwa na kazi hiyo ambayo ndio sehemu muhimu ya Chama Cha Mapinduzi kujijenga kisiasa kwa kuvuna wanachama wengi.
Aidha alitoa wito kwa Wanachama wa CCM kwa Zanzibar na Tanzania bara kuwa wahakikishe CCM inashinda kwa kura nyingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 pamoja na uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020,ili kuendelea kulinda Tunu za Taifa za Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika mahojiano yake hayo ameahidi kuwa CCM itaimarisha Vyombo vyake vyoye vya Habari vilivyopo Zanzibar na Tanzania bara ili Watendaji wake wafanye kazi katika mazingira rafiki na kupata maslahi yanayoendana na hadhi ya Taasisi wanayoifanyia kazi.
Pamoja na hayo alizipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na CCM kwa ujumla kwa kuandaa utaratibu mzuri wa kuwaenzi na kuwaombea Dua ya Kitaifaa Waasisi mbali mbali walioshiriki katika harakati za Ukombozi wa Zanzibar wakiongozwa na Hayati Karume.
Mapema Katibu Mkuu huyo amewatembelea Viongozi wastaafu mbali mbali wa CCM na Serikali zake akiwemo Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Waziri wa Zamani wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Ameir Mohamed, Rais mstaafu wa awamu ya Sita Dkt. Amani Abeid Karume na Mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni