Jumamosi, 5 Januari 2019

UVCCM YAANZA RASMI MATEMBEZI YA KUENZI MIAKA 55 YA MAPINDUZI LEO TAREHE 05/01/2019.


 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla akiwahutubia vijana wa CCM mara baada ya ufunguzi wa matembezi hayo.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Tabia Maulid Mwita akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa matembezi ya UVCCM Pemba.

 KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl.Raymond Mwangwala akizungumza katika ufunguzi wa matembezi ya UVCCM ya kuazimisha miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar ndugu Mussa Haji Mussa akisoma taarifa ya matembezi ya UVCCM Zanzibar.

 BAADHI ya Vijana wa UVCCM wakisikiliza nasaha mbali mbali za viongozi wa Chama na Jumuiya hiyo katika hafla ya ufunguzi wa matembezi ya miaka 55 ya Mapinduzi.

 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla akipokea picha ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

 VIONGOZI wa CCM na UVCCM wakiwa katika matembezi hayo mara baada ya kufunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi huko Wilaya ya Mkoani Pemba.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatua ya Vijana wa Chama hicho kutembea kwa miguu kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kinadhihirisha uzalendo,ukakamavu,ujasiri na  mshikamano wa vijana hao katika kuthamini mambo mema ya kimaendeleo yaliyoasisiwa na viongozi waliofanya Mapinduzi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi wakati akifungua matembezi ya UVCCM ya kuwaenzi waasisi wa Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya shamrashara ya maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar , hafla iliyofanyika katika Wilaya ya Mkoani Pemba.

Dk.Mabodi alifafanua kuwa Vijana wanapotembea masafa marefu kwa miguu inakuwa ni sehemu ya kuwaenzi kwa vitendo waasisi mbali mbali wa mapinduzi hayo waliotembea umbali mrefu kwa lengo la kupigania uhuru wa kudumu katika visiwa vya Zanzibar.

Alieleza kuwa ndani ya miaka 55 ya Mapinduzi hayo Serikali ya Mapinduzi imetekeleza mambo mbali mbali ya kimaendeleo katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi,kijamii na kisiasa.

Alizitaja baadhi ya Sekta zilizoimarika kwaasilimia kubwa ni pamoja na sekta za Afya,Elimu, Miundombinu ya usafiri wa anga na nchi kavu,upatikanaji wa maji safi na salama, kilimo, uvuvi pamoja na ulinzi na usalama wa nchi.

Alieleza kuwa CCM ina dhamira ya kudumu kuzisimamia Serikali zake zitowe huduma bora kwa wananchi wa maeneo mbali mbali ya mijini na vijijini kwa upande wa Pemba na Unguja.

Akizungumzia Muungano wa Zanzibar na Tanganyika Dk.Mabodi alisema muungano huo umekuwa chachu ya maendeleo ya kudumu na umezidisha mahusiano wa kiundugu  baina ya wananchi wa  nchi hizo mbili.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa ndugu Tabia Maulid Mwita,ameahidi kuyafanyia kazi maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chama Cha Mapinduzi kwa lengo la kujenga umoja wa vijana imara kimkakati na kisiasa.

Amesema kuwa matembelezi ya vijana hao wa UVCCM yamekuwa sehemu muhimu ya kuwajenga kifikra na kuwaongezea ujasiri katika utendaji wao wa shughuli za Taasisi hiyo.

“Vijana tupo imara, na hakuna mtu yeyote wa kuzuia ama kuharibu mshikamano tuliokuwa nao ndani ya UVCCM na lengo la kujiimarisha ni kuhakikisha tunayafuata kwa vitendo mambo yote yaliyoasisiwa na waasisi wa ASP na TANU hadi ikazaliwa CCM.”, amesema Makamu Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa.

Akizungumza Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Mwl.Raymond Mwangwala alisema Tanzania inajengwa na vijana imara waliohokwa katika tanuru la UVCCM ambao ndio viongozi wa leo na kesho katika taasisi za Chama na Serikali za Chama Cha Mapinduzi.

Kupitia hafla hiyo ya ufunguzi wa matembezi hayo, Katibu Mkuu huyo Raymond ametangaza kuwa UVCCM itahakikisha inafuta Chama Cha CUF Kisiwani Pemba ambacho hakina tija wala manufaa kwa wananchi wa kisiwa hicho.

Amesema ni wakati mwafaka wa Pemba kufanya maamuzi sahihi ya kupima faida na hasara za kuendelea kubaki katika chama cha upinzani hali ya kuwa Chama Cha Mapinduzi ndio kinachowaletea maendeleo bila ya ubaguzi wa kisiasa,kidini na kikabila.

Amesema sababu za kuweka azimio la kuufuta upinzani kabla ya mwaka 2020 ndani ya kisiwa cha Pemba zinatekelezwa kwa mikakati imara ya Kisera kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayotekelezwa kwa vitendo na kwa kasi kubwa ndani ya Pemba.

Amesema Pemba ya miaka 20 iliyopita sio Pemba ya sasa kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeimarisha Sekta mbali mbali zikiwemo Afya, Elimu, miundombinu ya umeme na barabara pamoja na mshikamano wa kijamii na kisiasa.

Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo aliwataka Vijana wa Umoja huo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mipango mbali mbali ya kufanikisha ushindi wa kishindo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka huu wa 2019.

Amesema uchaguzi huo ni miongoni mwa mchakato muhimu utakaosaidia kufanikisha ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Uchaguzi Mkuu  unaotarajiwa kufanyika  mwaka 2020.

Mwl.Raymond amewaagiza viongozi wa ngazi mbali mbali za UVCCM Tanzania nzima kutoa matamko ya kupongeza juhudi za usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, zilizoinua hali ya kipato cha mwananchi mmoja mmoja , ustawi wa kijamii pamoja na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Pamoja na hayo Raymond alieleza kwamba UVCCM kwa sasa imejikita katika kuandaa viongozi madhubuti walioiva katika fani mbali mbali na makada wasiokuwa na shaka yoyote katika kulinda na kutetea kwa vitendo tunu za Taifa ambazo ni Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Serikali mbili za Zanzibar na Tanzania bara.

Alisema UVCCM sio Taasisi ya kuandaa viongozi wasaka tonge na wenye uchu wa madaraka na mali bali ni chachu ya kuandaa viongozi wazalendo na waadilifu wenye uwezo wa kuendeleza mema yote yaliyoasisiwa na viongozi wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU na baadae ikazaliwa CCM.

“Vijana wa UVCCM watapikwa kupitia Vyuo vya Uongozi vya CCM vilivyopo maeneo mbali mbali ya Tanzania vikiwemo Chuo cha Kibaha, Chuo cha Katunguru, Chuo cha Ihemi pamoja na Chuo cha Tunguu kilichopo Zanzibar ili kupata viongozi walioiva kisiasa na kiutendaji.

Pia tunajipanga kuwa miongoni mwa taasisi imara ya uzalishaji mali hasa kupitia sekta ya kilimo kwa kuyatumia mashamba yetu kwa shughuli za kilimo cha kisasa ili tuzalishe mazao ya biashara yatakayotumika kuendeleza Sera ya mageuzi ya viwanda nchini.”, alieleza Mwl.Raymond.

Akisoma taarifa ya matembezi hayo, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar ndugu Mussa Haji Mussa ameeleza kuwa lengo la matembezi hayo ni kuenzi kwa vitendo juhudi za waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar waliothubutu kufanya mapinduzi  ambayo yameleta mabadiliko chanya kwa wananchi  wa visiwa vya Zanzibar.

Alisema waasisi hao wakiongozwa na aliyekuwa Jemedari wa Mapinduzi hayo Marehemu Mzee Abeid Karume, walijitolea kufanya mapinduzi hayo kutokana na vitendo vya udhalilishaji na dhuruma vilivyokuwa vikifanywa na utawala wa kisultani kwa wakati huo.

Alieleza kwamba UVCCM itaendelea kuwa taasisi imara inayotoa vijana wenye uwezo wa kukitumikia chama cha mapinduzi kwa uzalendo na uadilifu mkubwa katika masuala mbali mbali ya kisiasa.

Naibu Katibu Mkuu Mussa, alieleza kuwa Umoja huo utapambana na mtu yeyote atakayethubutu kupinga maendeleo yanayotekelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Ali Mohamed Shein, katika uimarishaji wa uchumi wa nchi.

Katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa matembezi hayo alikabidhiwa picha maalum za viongozi mbali mbali wa Kitaifa wakiwemo waasisi wa Mapinduzi hayo ya Zanzibar  ambao ni Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati Mwl.Nyerere, Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.

Pamoja na makabidhiano ya picha hizo pia walikabidhi Bendera mbali mbali zikiwemo bendera ya Tanzania, Bendera ya Zanzibar, Bendera ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na bendera ya Afro Shiraz Party (ASP) ikiwa ni ishara ya kutoa heshima ya kuenzi juhudi za viongozi hao.

Matembezi hayo yaliyofunguliwa Januari 4 mwaka huu yanatarajiwa kufikia kilele chake januari 10 mwaka 2019 yaliyowashirikisha zaidi ya vijana 400.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni