Jumapili, 6 Januari 2019

UVCCM YASHIRIKI UJENZI WA TAWI LA CCM, YAENDELEA NA MATEMBEZI YA MGUU KWA MGUU PEMBA.


 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Tabia Maulid Mwita.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Tabia Maulid Mwita amesema Umoja huo unafanya matembezi ya kuenzi miaka 55 ya Mapinduzi kwa nia ya kuendeleza utamaduni wa kizalendo ulioasisiwa na Vijana wa ASP walioshiriki kwa ari hamasa kubwa katika shughuli za kijamii zikiwemo kujenga nyumba za maendeleo, Afisi za Chama na Jumuiya pamoja na kuwasaidia kazi mbali mbali Wazee waliopo katika jamii.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kushiriki shughuli mbali mbali za ujenzi wa Tawi la Chama Cha Mapinduzi(CCM)huko Kangani ambapo maelfu ya vijana wameshiriki katika ujenzi huo kwa kushirikiana na Viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zake.

Tabia amesema matembezi ya mwaka huu yameangazia zaidi katika ushiriki wa shughuli za kijamii katika maeneo mbali mbali yaliyopangiwa kupita matembezi hayo kwa lengo la kuacha alama bora ya viongozi wengine wa UVCCM kuendeleza utaratibu huo.

Kupitia mahojiano Maalum na cHAMA BORA TV alisema waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya ZAnzibar ya mwaka 1964 walikuwa ni wamoja,wazalendo,waadilifu na wachapakazi licha ya zama za wakati wao zilikuwa na changamoto mbali mbali za kisiasa na uhaba wa miundombinu.

Katika maelezo yake Makamu Mwenyekiti huyo aliwataka vijana kuwa wazalendo na kuwa tayari kutumika kwa jambo lolote linalogusa maslahi ya wengi ili kuandaa mazingira rafiki ya kutekeleza kwa vitendo ibara ya Tano ya CCM ya kushinda kwa kishindo 2020.

Pia alieleza kwamba matukio mbali mbali yanayofanywa na UVCCM kupitia matembezi hayo yanakubalika kwa wananchi wote kwani wanashiriki katika kufanya kazi za kuisaidia jamii husika.

Alizitaja baadhi ya kazi zitakazotekelezwa katika matembezi hayo ni pamoja na kujenga vyoo mbali mbali vya kuwasaidia vitakavyosaidia kuwasitili wanawake, kusaidia vifaa vya michezo, ujenzi wa Ofisi za Chama na Jumuiya pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya Mikoa miwili ya Pemba.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Magharibi Unguja Fahmy Ali Mwinyi ameeleza kuwa matembezi hayo yamekuwa ni sehemu ya darasa la kujifunza mambo mengi ambayo awali hakuyajua ikiwemo historia halisi ya Pemba.

Ametoa wito kwa vijana wenzake kuendeleza utamaduni wa kujitolea katika masuala ya kijamii kwani yanawajengea ujasiri na ukomavu wa kisiasa sambamba na ujasiri wa kupambana na changamano mbali mbali za kimaisha.

Akitoa historia fupi ya Tawi hilo la CCM lililojengwa, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mkoani Mohamed Abdalla Ali amesema Tawi hilo ni miongoni mwa Matawi ya Zamani ya ASP awali lilijengwa kwa miti na chokaa ambapo kwa sasa kupitia michango mbali mbali ya Wanachama wa CCM litajengwa Tawi la kisasa linaloendana na hadhi ya CCM.

Ameelezea furaha yake kuwa ujenzi wa Tawi hilo lingechukua muda wa mwezi mmoja lakini kupitia matembezi hayo litajengwa kwa kiwango kiwango kikubwa na siku chache litakuwa limekamilika.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mtambile Mhe.Mohamed Mgaza, ambaye ni miongoni mwa viongozi walioshiriki kuchangia vifaa vya ujenzi wa Tawi hilo amesema kila mwanachama wa CCM ana wajibu wa kushiriki katika harakati mbali mbali za ujenzi wa taifa ili Chama kiwe na majengo ya kisasa.

Pamoja na hayo, Mohamed amewapongeza vijana wa UVCCM waliobuni mfumo wa kufanya matembezi sambamba na shughuli za kijamii na kuongeza kuwa yatasaidia kukirejesha chama katika utamaduni wa imara uliokuwa ukifanywa na vijana mbali mbali wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni