Jumanne, 8 Januari 2019

DK.MABODI: AONGOZA MAELFU YA WANANCHI KATIKA MAZISHI YA MNEC MAREHEMU BAKARI.

 WANACHAMA wa CCM pamoja na wananchi kwa ujumla wakimzika Marehemu Bakari Hamad Khamisi.


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi leo ameongoza maelfu ya Wana CCM na Wananchi kwa ujumla katika mazishi ya aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Oganazesheni CCM Zanzibar Marehemu Bakari Hamad Khamis aliyezikwa katika eneo la Mwanakwerekwe Unguja. 


Marehemu Bakari Hamad pia alikuwa ni Mjumbe wa NEC, amefariki jana katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mara baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Kisukari.

Dk.Mabodi kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein  amewaongoza wananchi,Viongozi wa Chama na Serikali katika mazishi hayo.

Awali asubuhi Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein alitoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu na kushiri katika katika maandalizi ya mazishi.


Viongozi mbali mbali walioudhuria katika mazishi hayo ni  pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Samia Suluhu Hassan,Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Wenyeviti wa CCM wa ngazi Matawi hadi Mikoa, Makatibu wa CCM wa ngazi za Matawi hadi Mikoa, Wazee wa Chama, wanachama wa CCM pamoja na wananchi mbali mbali.

Pia Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Jumuiya zote tatu za Chama cha Mapinduzi wamejitokeza kwa wingi katika mazishi hayo ya kiongozi huyo wa CCM. 

Marehemu Bakari enzi za uhai wake aliwahi kuhudumu nafasi mbali za Kiuongozi na Kiutendaji ndani ya Chama na Jumuiya zake na kuacha historia nzuri ya Ubunifu, Uadilifu na kiutendaji uliotukuka katika Taasisi alizozifanyia kazi. 

Marehemu Bakari ameacha Vizuka watatu na watoto 17.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pema peponi Amin.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni