Jumatatu, 7 Januari 2019

UVCCM WATUA WILAYA YA CHAKE CHAKE, WENYEJI WASEMA HAIJAWAHI TOKEA.

VIJANA mbali mbali wa UVCCM wakishiriki shughuli ya kutia kifusi katika Skuli ya Msingi ya Chanjaani iliyopo katika Wilaya ya Chake Chake Pemba.

 VIJANA wa UVCCM wakiwa katika harakati za kushiriki shughuli za kijamii katika Wilaya ya Chake Chake Pemba.


NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Chake Chake Pemba Ndugu Khamis Mbarouk Salum amesema maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar yameleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo na kuubadilisha Mji wa Wilaya hiyo kuwa wa kisasa na wenye huduma muhimu zinazokidhi na mahitaji ya jamii.

Udhibitisho huo ameutoa leo wakati akipokea matembezi ya Umoja wa Vijana wa Ccm wakitokea katika Wilaya ya Mkoani na kuwasili Wilayani humo kwa lengo la kuendelea na matembezi hayo kwa siku ya tatu ndani ya kisiwa cha Pemba.

Amesema dhamira ya Mapinduzi imeendelea kuishi katika mioyo na maono ya viongozi wa awamu mbali mbali za uongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake wanaobuni masuala mbali mbali ya maendeleo kwa nia ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Anaeleza kuwa Mji wa Chake Chake ambao ndio kitovu cha biashara na Sekta za umma na binafsi kisiwani humo umeimarishwa na kujengwa miundombinu ya kisasa ya nyumba za biashara, nyumba za makaazi ya watu pamoja na miundombinu ya barabara zenye kiwango cha lami hatua ambayo ni kubwa katika maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Pia ameongeza kuwa hatua hizo za kimaendeleo zimerahisishia wananchi ambao wengi wao ni wakulima kupata fursa pana ya kusafirisha kwa urahisi mazao yao kutoka vijijini kwenda mjini kuuza bila usumbufu.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Khamis amewakaribisha vijana wote watembeaji ambao ni zaidi ya 400 katika Wilaya hiyo na kuwambia kuwa wajisikie huru kwani eneo hilo lipo shwari kisiasa na kijamii kwa ujumla.

Akizungumza Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mhe.Suleiman Sarahani amesema Mapinduzi yanagusa maisha ya wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania bara kwani kufanyika kwake kulifungua fursa ya maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili za jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Akiyataja maendeleo yaliyofikiwa ndani ya Jimbo hilo amesema kwa sasa wananchi wanapata huduma bora za kijamii zikiwemo Elimnu bora, Afya, maji safi na salama pamoja na kujengewa masoko ya kisasa ya kufanya biashara hasa wajasiriamali wadogo wadogo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Ndugu Mussa Haji Mussa,amesema umoja huo walichodhamiria ni kuenzi kwa vitendo mapinduzi kwa kufanya shughuli mbali mbali za kijamii.

Amesema katika matembezi hayo watashiriki katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo za Serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt,John Pombe Magufuli ambao wamekuwa ni viongozi bora katika kuitekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Ametoa wito kwa vijana wa Wilaya mbali mbali Kisiwani Pemba kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki matembezi hayo, yanayowaweka pamoja vijana na kuwajengea uzalendo vijana wa Tanzania.

Wakizungumza kwa wakati tofauti wakaazi wa Chanjaani, wameeleza kuwa kitendo kilichofanywa na vijana wa UVCCM katika kushiriki shughuli mbali mbali za kijamii katika eneo hilo hakijawahi kufanyika na ni mara ya kwanza na kinastahiki kupongezwa.

Khadija Issa Hamad Mkaazi wa kijiji hicho, amesema kuwa alipowaona vijana hao kwanza alishutuka kwani walikuwa ni wengi wakifanya kazi ya kuingiza kifusi katika madarasa mbali mbali ya Shule ya msingi.

Matembezi hayo yaliyoendelea kutoka Wilaya ya Mkoani Wadi ya Kangani hadi Wadi ya Wawi Wilaya ya Chake Chake Pemba.

















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni