Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Abdi Ali Mzee ‘Mrope’ (anayezungumza wa pili kulia) akifungua mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa maskani ya Kisonge. |
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi
wakifuatilia matukio mbali mbali yanayoendelea kabla ya uchaguzi kufanyika. |
Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa maskani ya CCM
Kisonge Juma Raja Juma akipiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa maskani hiyo
kabla ya kushinda nafasi hiyo. |
MASKANI ya Kisonge ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar imempata Mwenyekiti wao mpya,Juma Rajab Juma baada ya
kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana,ukumbi wa Nasari ya matumbaku
Miembeni.
Uchaguzi huo ulikuwa ni wa
ushindani mkubwa ambapo Mwenyekiti huyo aliibuka kidedea baada ya kupata kura
93 kati ya 198 huku kuura 6 ziliharibika.
Wagombea wengine wa waliogombea
nafasi hiyo ni Mohamed Haji Dau aliyepata kura 3,Mwanangasama Mohamed aliyepata
kura 66.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano
huo Mwenyekiti huyo mpya,Juma, aliwashukru
wanachama hao kwa kumuamini na kumchagua ambapo ameahidi kushirikiana
nao kwa lengo la kuiletea maendeleo Kisonge.
Mapema akifungua Mkutano wa
uchaguzi wa maskani hiyo , Mwenyekiti wa CCM Wilaya Amani Abdi Ali Mzee ‘Mrope’ amewataka wajumbe wa
mkutano huo kutochaguana kwa urafiki na kwamba wachaguane kwa uwezo wa
kiutendaji na watakaounganisha wana CCM.
Aidha, Mwenyekiti huyo
amewasisitiza viongozi watakaochaguliwa kupitia uchaguzi huo kutokubali
kuharibiwa heshima ya maskani hiyo ambayo imekuwa na historia ya ukomavu wa
kisiasa.
“ Baadhi ya watu wasioipenda CCM
wakisikia maskani ya Kisonge ina mpasuko basi wao wanafurahi na kuendeleza
mbinu chafu za kuihujumu, kwani hata uchaguzi huu najua kuna watu nje huko
hawakupenda ufanyike lakini ndo sasa ushakuwa endeleeni na mapambano ya
kukilinda na kukitetea Chama Cha Mapinduzi.
"Kisonge haiwezi kusimama
bila ya umoja na mshikamano kwani wazee wetu walioasisi CCM na kuikomboa
Zanzibar walikuwa na umoja wakipendana na kutumia vikao halali kusuluhisha
migogoro iliokuwa ikijitokeza katika kuwagawa hivyo na sisi tunatakiwa kuweka
fikra zetu katika utamaduni huo na
kuachana na misuguano isiyokuwa ya lazima na yenye kubomoa chama,"alisema
Mwenyekiti huyo wa Wilaya
Alisema ni wakati wa kila mwana-
CCM kuelekeza nguvu zake katika kujiandaa na ushindi wa uchaguzi wa mwaka 2020
na kupoteza muda katika kurumbana wenyewe kwa wenyewe katika mambo yasiyokuwa
na tija.
Mwenyekiti huyo wa Wilaya ya
mjini Mrope, alitoa wito kwa wagombea
ambao kura zao hazitotosha wasinune na badala yake washirikiane katika kushauri
viongozi watakaochaguliwa ili kuendelea kuwa wakomavu wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa katiba na kanuni
viongozi mbali mbali waliochaguliwa katika maskani hiyo wataongoza kwa kipindi
cha miaka mitano.
Pia, kwa upande wa wagombea wa
nafasi ya wajumbe wa kamati ya uongozi ya maskani hiyo ambao ni wajumbe wanne
lakini walijitokeza ni 12, ambapo jumla ya kura zilizopigwa ni 168 huku
zilizoharibika ni 13.
Walioshinda nafasi ya wajumbe wa
kamati hiyo ni ni Dauwat Saleh kwa kura 70, Omar Mohamed Suleiman kura 84,
Suwaila Masoud Mohamed kura 96 na Mbaraka Haji Vuai kwa kura 85.
Kupitia uchaguzi huo uongozi mpya
wa Kisonge ulimteuwa mjumbe mmoja ambaye ni Suwaila Masoud Mohamed kuwa Katibu
wa maskani hiyo kati ya wanne waliochaguliwa katika uchaguzi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni