Jumatano, 2 Mei 2018

" VIJANA HAKIKISHENI MNAULINDA MUUNGANO WETU " ZAHORO



NA EMMANUEL MOHAMED,ZANZIBAR

MJUMBE wa Baraza kuu la Jumuiya ya Wazazi,Zahor Salehe Mohamed amewataka vijana visiwani humu kuhakikisha wanaendelea kuwa wazalendo katika kuulinda muungano.

Amesema muungano huo kwa vijana hao una faida nyingi ikiwemo kuwepo kwa ulinzi na usalama wa uhakika ambapo isingekuwepo muungano kusingekuwepo na hali ya amani.

Hayo aliyasema jana wakati akizungumza na vijana wa Umoja wa Vijana(UVCCM) kutoka wilaya ya Mjini na Kati,ambapo alieleza kuwa faida nyingine ni kufaidika na ardhi ilioko upande wa Tanzania bara katika kujikita kwenye kilimo.

Alisema Zanzibar ina ardhi ndogo ikilinganishwa na upande wa Tanzania bara ambapo itawasaidia vijana hao kupata fursa ya kujikita kwenye sekta ya kilimo.

"Tushukuru viongozi wetu ambao ni wahasisi wetu Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume kwa kuungana kwa maslahi ya taifa letu hivyo kuna haja ya kuhakikisha tuna endelea kuu  linda muungano wetu,"alisema Zahor

Mjumbe huyo aliongeza kuwa viongozi hao walikuwa wana umoja kupitia chama hadi serikali hivyo vijana wanapaswa kuwa wazalendo kuulinda muungano,chama na serikali zote mbili.

"Umoja wenu utasaidia kuleta maendeleo ya taifa na kuifanya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuendelea kukaa madarakani kwa serikali zote mbili na kuhakikisha muungano unaendelea hakuna ubishi kuwa vijana ndio wanakiweka chama madarakani,"alisema Mjumbe huyo.

Katika maelezo yake Zahor alisema vijana kwa sasa wana kazi moja ya kukusanya takwimu za idadi ya wanachama kwa vijana ili kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2020 na kwamba takwimu ndio uchaguzi wenyewe.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM, wilaya ya Mjini, Hudhaima Mbaraka Tahir, alisema umoja huo unaendelea kufanya kazi nyingi katika jamii ili kuhakikisha CCM inapata kura nyingi kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema vijana hao wako tayari kufanya kazi kubwa ya kukusanya takwimu nyumba hadi nyumba na baadae kuwasilisha CCM kwa ajili ya kuifanyia kazi.

"Katika wilaya yetu hakuna makundi kwa vijana na kwamba jambo linalojivunia ni kuwa na umoja ambao ni nguvu ya umoja wetu wa UVCCM katika kukitumikia chama katika mapambano ya uchaguzi wa mwaka 2020,"alisema Mwenyekiti huyo

Mwenyekiti Hudhaima aliongeza kuwa katika UVCCM ya wilaya yake haitavumilia kuona mtu anajaribu kutaka kuvunja umoja huo uliopo kwenye jumuia hiyo na kwamba umoja ni nguvu kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni