Ijumaa, 4 Mei 2018

DK.SHEIN ASEMA USHINDI WA CCM 2020 UKO PALE PALE

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Dk.Ali Mohamed Shein  akizungumza nao katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Mohamed Juma Pindua Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi.

MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kazi kubwa ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia Shina hadi Taifa ni kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi Mkuu na ule wa Serikali za Mitaa na hatimae kukamata Dola kwa Zanzibar na Tanzania Bara.

Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Kusini Pemba huko katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Mohammed Juma Pindua Mkanyageni katika mkutano wake wa kukutana na Mabalozi wa Wilaya zote za Zanzibar ulioanza katika Wilaya hiyo.

Kuchaguliwa kwao ni kwa lengo la kukitumikia chama cha CCM ili kushinda uchaguzi na kuongoza dola kwani CCM ni chama kinachopendwa na wananchi wenyewe na chenye wafuasi wengi sana na hayo ni maelekezo ya Katiba ya CCM kuwa chama hicho ni lazima kishinde chaguzi zake zote.

Alisema kuwa CCM ni chama halisi cha Watanzania halisi na Wazanzibari halisi wanayoipenda nchi yao na hakina mbadala kwa Tanzania huku akisisitiza kuwa suala la ushindi katika uchaguzi ni lazima kwani ni maelekezo ya Katiba na Kanuni ya Chama hicho na kuzingatia historia ya TANU na ASP, CCM ni lazima ishike Dola kwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliongeza kuwa kazi kubwa ya siasa ni kutafuta na kuikamata Dola na hatimae kuikabidhi Serikali ambapo pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza Mabalozi wote waliochaguliwa na waliokuwa kura zao hazikutosha.

Alieleza kuwa kazi kubwa ya viongozi wa CCM ni kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho na Mabalozi pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbali mbali ni kuhakikisha inatekelezwa kwa vitendo.

Alieleza kuwa CCM ni chama chenye mtandao mkubwa sana wa utumishi na uongozi na kusisitiza haja ya kila kiongozi kutekeleza wajibu wake na kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yake na ndio maana mambo yake yamekuwa yakienda kwa kasi kutokana na mtandao huo.

Alisisitiza haja ya kuwa makini na kutekeleza vyema majukumu yao na kukiimaraisha chama cha Mapinduzi na kutumia fursa hiyo kueleza wajibu wa Mabalozi kwani ni watu wakubwa sana ndani ya chama hicho.

Alieleza kuwa wao ni walinzi namba moja wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwani wao ndio wa mwanzo wa kuyalinda, kuyadumisha na kuyatetea na viongozi wote wa ngazi za juu wataendeleaa kuwaunga mkono.Aidha, alisisitiza haja ya kujengwa kwa majengo ya chama, na kueleza umuhimu wa Mashina na kusisitiza kuwa Mabalozi ndio muhimili mkuu wa chama kwani wao ndio wawakilishi wa CCM katika nyumba zao wanazoziongoza.

Alieleza kuwa hakuna mkataba kuliko hati za Muungano ambayo ndio makubaliano makubwa waliyosainiwa kati ya Marehemu Mzee Ameid Karume na Mwalimu Julius Nyerere na kuwataka Mabalozi wasisikilize mambo yatakayowapotezea mwelekeo.

Alisema kuwa wanaCCM wapo macho na wapo hadhiri katika kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.Aliongeza kuwa maadili ni ungozi wa chama hicho kwani yapo mambo ambayo viongozi wa CCM hawatakiwi kufanya katika uongozi wao huku akisisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki na ni aibu kwa mwanaCCM kutoa na kupokea rushwa.

Aliwataka viongozi hao kutoogopa kusema wala kuwataja watoaji na wapokeaji wa rushwa na wala wasinungunike pembeni kwani hata vitabu vyote vya dini vinakataza rushwa na lazima Mabalozi washirikiane na viongozi wa CCM wa Jimbo, Wilaya na hatimae viongozi wa ngazi za juu katika kuwataja watoaji na wapokeaji rushwa.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa tayari ameshatangaza kuwa elimu ya Msingi bure na ikifika Julai katika Bajeti ya mwaka huu 2018/2019, elimu ya Sekondari itakuwa bure kwani pesa sio tatizo na kusisitiza kuwa atakaetoza fedha kuanzia muda huo Serikali itapambana nae.Kwa upande wa afya, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inauwezo mkubwa wa kutekeleza huduma za afya bure kwa wananchi kwa kutekeleza azma ya Marehemu Mzee Karume katika sekta hiyo.

Alieleza kuwa hakuna mwananchi hata mmoja anaebaguliwa kwa jinsia yake, rangi yake, dini yake, kabila yake huku akieleza kuwa hakuna haja ya kuleta lugha ya istizai katika maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Shein aliwataka viongozi wote wa CCM kuyatangaza mafanikio ya Serikali pamoja na kwenda kuwaeleza watu mafanikio yaliofikiwa “Na nyie mnajua kuwa wengine uongo imekuwa kama jadi yao”,alisema Dk. Shein.

Alisikitishwa na uongo wa baadhi ya wanasiasa wanaosema kuwa kuna walimu wamepelekwa skuli ya Chokocho wakati hakuna mwalimu hata mmoja aliepelekwa katika skuli hiyo. Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka Mabalozi kushirikiana katika mapambano ya unyanyasaji wa kijinsia.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi alieleza umuhimu wa Mabalozi na mchango wao mkubwa katika kuimarisha chama na kueleza haja ya kutekeleza majukumu yao ipasavyo huku akitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa rais Dk. Shein kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kutekeleza Ilani pamoja na uongozi wake madhibuti katika Serikali anayoiongoza.Katika risala yao, Nao Mabalozi walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuwajali na kumpongeza kwa kuwajali wazee wanaopata pencheni huku wakieleza jinsi wanavyofaidika na miradi ya TASAF ambayo imekuwa mkombozi katika maisha yao.

Mwajuma Hassan Kaduara akisoma risala ya Mabalozi, alieleza kuwa kuwepo kwa baadhi ya watumishi serikalini ambao hawatoi huduma vyema kwa wananchi hali ambayo inapelekea kuipaka matope Serikali inayoongozwa na CCM.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Hemed Suleiman alitumia fursa hiyo kueleza ukweli juu ya suala zima la ajira lilivyofanyika katika mkoa huo na kueleza kuwa Skuli ya Chokocho hakuna mwalimu hata mmoja aliyopelekwa na maneno yanayovumisha na baadhi ya wanasiasa si ya kweli kama skuli hiyo wamepelekwa walimu wanane na kueleza kuwa ajira zilikuwa zinazingatia Wizaya zote, na kuwataka wale wote wanaovumisha hivyo kuutafuta ukweli. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni