MBUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mahonda, Bahati Ali Abeid amewataka watendaji na viongozi wa ngazi mbali mbali za Chama na jumuiya katika jimbo hilo kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha taasisi hiyo kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo makatibu na wenyeviti wa CCM na Jumuiya zake ngazi za matawi hadi jimbo huko katika ofisi ya Jimbo la mahonda iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.
Amesema viongozi hao wanatakiwa kufanya kazi za CCM na kutekeleza maagizo mbali mbali ya viongozi wa ngazi za juu kwa lengo la kuongeza kasi ya kuwatumikia wananchi waliokipa ridhaa Chama kuongoza dola.
Mh. Bahati amewakumbusha viongozi hao kwamba wanakiwa kulinda na kutetea maslahi ya CCM kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili Chama kishinde katika uchaguzi mkuu ujao.
Amesema viongozi hao wanatakiwa kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ambayo ni miongoni mwa nyenzo za kurahisisha majukumu yao ya kiutendaji ndani Chama Cha Mapinduzi.
Ameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo Chama kinatarajia kuona mabadiliko ya haraka ya kiutendaji kutoka kwa viongozi na watendaji hao.
"Baada ya mafunzo haya mnatakiwa kusimama imara na kujiamini ili wanachama waliokuchagueni muwe viongozi waone umuhimu wenu katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Pia mnatakiwa kufanya maamuzi na kujadili matatizo na kero za wanachama kupitia vikao halali vya kikatiba ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima katika ngazi zenu za kiutendaji na kiuongozi", alisema Mbunge huyo ambaye ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya Jimbo hilo.
Akitoa mada ya kuliwa kwa CCM, Katibu wa Kamati maalum ya NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakari Hamad Khamis, alisema CCM ina historia ndefu ambayo msingi wake unatokana na juhudi za waasisi wa ASP na TANU ambao ni marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kuleta umoja na mshikamano kwa wananchi.
Amesema mwaka 1964 Chama cha ASP kiliamua kufanya Mapinduzi kwa lengo la kuwakomboa wananchi wa visiwa vya Zanzibar, waliotawaliwa kwa mabavu na utawala wa kisultani.
Alieleza kwamba baada ya Mapinduzi hayo waasisi hao walifanya maamuzi ya kuziunganisha nchi mbili ya Zanzibar na Tanganyika ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Pamoja na hayo Katibu huyo amefafanua kuwa mwaka 1977 vyama vya ASP na TANU baada ya kushauriana kwa muda mrefu vikaamua kuungana na kuunda Chama kimoja chenye nguvu ambacho ni Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa lengo la kusimamia siasa na demokrasia za kweli kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania bara.
Katibu huyo Bakari amewasisitiza vijana nchini kusoma historia halisi ya Zanzibar ili wajifunze na kutambua mambo ya maendeleo yaliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake kwa awamu mbali mbali za uongozi wa dola.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni