NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein akipokea risala ya mabalozi wa CCM Wilaya ya Kati Unguj. |
BAADHI ya wajumbe wa NEC waliofuatana na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar katika ziara yake ya kuzungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya Kaskazini Unguja. |
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein amewaonya baadhi ya watu wanaofanya kampeni za kusaka Urais wa Zanzibar
kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika na kusisitiza kuwa yeye bado ni Rais wa Zanzibar.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wa Chama na
Serikali tayari wameanza kupanga timu za Urais badala ya kushughulika na mambo
ya msingi ya kufanya shughuli za Chama zitakazofanikisha kuiweka serikali
madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.
Onyo hilo amelitoa
katika mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa
kuzungumza na mabalozi wa mashina katika Wilaya ya kati Unguja,iliyofanyika
ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) ulipo Tunguu Mkoa wa Kusini
Unguja.
Amesema nafasi ya
Urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyokuwa halali bali
inapatikana kwa utaratibu maalum kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa
mujibu wa Katiba na miongozo na kanuni
mbali mbali za CCM.
Alibainisha kuwa kwa wakati tofauti
amewatahadharisha baadhi ya viongozi na wanachama hao kuacha tabia hizo kwani
zinaweza kuleta migogoro na mgawanyiko isiyokuwa ya lazima ndani ya CCM kabla
ya uchaguzi mkuu ujao.
Amebainisha kuwa watu hao wanaosaka Urais kwa
sasa wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia mpaka 2020, atawachukulia hatua kali za
kinidhamu zikiwemo kufikishwa katika vikao vya usalama na maadili vya
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa dhidi ya
mwenendo wao juu ya mwenendo wao
usiokuwa na manufaa kwa CCM.
Alisema viongozi, watendaji na wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza mipango mbali
mbali ya kukisaidia Chama kushinda na sio kuangaika na urithi wa kiti cha
Urais.
“Naheshimu Katiba ya nchi muda wangu ukifika
naondoka madarakani kwani huo ndio utaratibu wa Chama chetu na kwa mujibu wa
sheria za nchi, lakini sifurahishwi hata kidogo kuona baadhi yenu mnaanza
kuangaika na Urais badala ya kufanya kazi za kuitafutia ushindi CCM mwaka
2020", alisisitiza Dk.Shein na kuwataka Mabalozi na viongozi wengine wa
ngazi za mashina kukataa kuingizwa katika mitandao hiyo ya kampeni.
Akizungumzia umuhimu wa viongozi hao, Dk.Shein
alisema CCM inathamini mchango mkubwa wa kuimarisha Chama unaofanywa na
viongozi wa mashina ambao ndio jeshi la kisiasa la Chama Cha Mapinduzi.
Alisema Chama kitaendelea kuisimamia vizuri
serikali ili itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kama
ilivyowaahidi wananchi katika kampeni za uchaguzi zilizopita.
Kupitia mkutano huo Dk.Shein aliwataka viongozi
hao kujenga utamaduni wa kusoma Katiba ya CCM
ya mwaka 1977 toleo la 2017, ili wajue majukumu waliokuwa nayo kwa
mujibu wa Katiba na kuyatekeleza ipasavyo.
Alisema katika hatua za kuzitafutia ufumbuzi
changamoto zinazowakabili wananchi, serikali inaendelea na mikakati ya matengenezo
ya barabara ya maeneo ya Mwanakwerekwe na kutengeneza daraja la kisasa katika
eneo la Kibonde mzungu ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wa Mkoa wa Kusini
Unguja.
Aidha alisema kwa upande wa changamoto ya maji
yanayotwaama katika eneo la Kibonde mzungu tayari serikali inaendelea na
mikakati ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa litakaloweza kumaliza tatizo hilo la
maji katika maeneo hayo.
Pia aliwambia mabalozi hao kuwa hakuna wa kuzuia
ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao kwani Chama hicho kimejiandaa kushinda
kwa nguvu za demokrasia, kwani kina wananchi wengi wanaokiamini na kukiunga
mkono kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.
Alisema Serikali inaendelea kutekeleza kwa
vitendo dhamira ya ASP ya kuwapatia wananchi huduma bure za kijamii hasa elimu
na Afya.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.
Abdulla Juma Mabodi, amesema mabalozi wa Chama Chama Mapinduzi wamekuwa mstari
wa mbele kurejesha Chama kwa wananchi.
Alisema
Chama Cha Mapinduzi kwa sasa kinaendelea na mfumo wa uongozi shirikishi
unaowashirikisha viongozi wa ngazi tofauti jambo ambalo Dk.Shein anaendeleza
mfumo huo kwa kuzungumza na mabalozi hao kila mwaka.
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Ramadhan Abdalla Ali 'Kichupa', alipongeza
Dk.Shein kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa huo katika
nyanja za kijamii,kiuchumi na kisiasa.
Mapema akisoma risala ya mabalozi, ndugu Mkombe
Vuai Khamis alisema serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk.Shein wananchi
wameshuhudia kuimarika kwa sekta mbali mbali nchini hasa suala zima la
kuanzisha penchini ya kuwalipa wazee ya
shilingi 20,000 kwa kila mwezi.
Kupitia risala hiyo walimpongeza Dk.Shein kwa
kuasisi na kuendeleza kwa vitendo hatua yake ya kutoa pencheni kwa wazee hatua
ambayo ni ya kishujaa kwani imesaidia mamia ya wazee wengi kupata fedha za
kujikimu kila mwezi.
Walisema wataendelea kulinda na kutetea maslahi
na miongozo ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo ili kishinde kwa ngazi zote
katika uchaguzi mkuu ujao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni