Jumatatu, 7 Mei 2018

DK.SHEIN AZUNGUMZA NA MABALOZI WILAYA YA AMANI, APOKEA WANACHAMA WAPYA.

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akiwahutubia mabalozi wa CCM Wilaya ya Amani, katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Zanzibar.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi kadi ya CCM mwanachama mpya aliyejiunga na Chama katika mwendelezo wa ziara zake katika Wilaya CCM Amani.
 ALIYEKUWA Kada wa CUF aliyejiunga na CCM Salim Mussa Omar(kushoto), akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.


WANACHAMA wapya wa CCM wakila kiapo  cha  Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ziara ya Dk.Shein Wilaya ya Aman.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akionyesha kadi za CUF zilizorejeshwa na aliyekuwa kada wa Chama hicho aliyejiunga na CCM Salim Mussa Omar, katika ziara ya Dk.Shein.


MABALOZI na viongozi mbali mbali wa CCM Wilaya ya Amani walioshiriki mkutano wa kuimarisha Chama katika ziara ya Dk.Shein.

 MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib akizungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya Amani katika ziara ya Dk.Shein.

 MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Amani Abdi Mzee 'Mrope' akizungumza na mabalozi wa CCM Wilaya hiyo.


JUMLA ya wanachama wapya 1457 akiwemo kigogo mmoja wa Chama Cha CUF wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Amani.

Wanachama hao wamepokelewa na Makamu Mwenyekiti wa (CCM) Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika mwendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na mabalozi wa CCM Wilaya ya Amani Unguja.

Mapokezi hayo ya wanachama wapya yamejumuisha na aliyewahi kuwa mjumbe wa Baraza la vijana CUF Taifa,  Salim Mussa Omar ambaye amejiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi.

Katika ziara hiyo Dk.Shein aliwambia mabalozi hao kwamba wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa ili kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema ushindi wa CCM unatokana na juhudi za mabalozi ambao wanatakiwa kueleza vizuri sera za CCM kwa wananchi waliopo katika ngazi ya mashina.

Aliitaja dhamira ya serikali ni kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, ili Zanzibar iwe na miji bora nay a kisasa.

Alisema katika kutekeleza mipango hiyo tayari serikali imefungua milango ya uwekezaji kwa wageni na wazawa ili wawekeze katika sekta ya ujenzi wa miji ya kisasa ikiwemo maeneo ya Fumba, Nyamanzi na Matemwe na inaendelea na maandalizi ya kuanza ujenzi wa nyumba za kisasa katika maeneo ya Chumbuni na Kwahani.

“Mipango hii ya kuifanya Zanzibar kuwa nchi yenye makaazi ya kisasa inawezekana, lakini lazima tufanye kazi ya ziada ya kuhakikisha serikali ya CCM inaendelea kubaki madarakani.”, aliwambia Mabalozi hao Dk.Shein.

Kupitia hotuba hiyo Dk.Shein alisema hatowavumilia baadhi ya watu wanaotaka kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Alieleza na kuongeza kuwa maendeleo yaliyopatikana visiwani Zanzibar yametokana na  uwepo wa amani na utulivu.

Dk.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema kuna watu waliowahi kuanzisha vikundi vya kuchafua hali ya amani lakini wamedhibitiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“ Nchi mbali mbali walichezea amani na utulivu wa nchi na sasa wameshindwa kurejesha hali hiyo na badala yake mamia ya wananchi wasiokuwa na hatia wanakufa kila siku”, alieleza Dk.Shein.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk.Abdalla Juma Mabodi alisema ziara hiyo ya Dk. Shein inatokana na matakwa ya sera za CCM zinazomtaka kila kiongozi kushuka ngazi za chini kuangalia utekelezaji wa ilani na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.

Alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeendelea kuaminiwa na wananchi kutoka na utarabu wake wa uongozi shirikishi kwa wanachama wote.

Akizungumza Mwenyekiti wa Mkoa huo, Talib Ali Talib alimpongeza Dk.Shein kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wa mijini na vijijini.

Mapema akisoma risala ya mabalozi hao, Fatma Kassim alisema viongozi hao wanaridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyotekelezwa ndani ya Wilaya hiyo.

 Mabalozi hao wamesema serikali imejenga mitaro mikubwa ya kusafirisha maji machafu katika majimbo ya Magomeni, Mpendae ,Shaurimoyo na Chumbuni pamoja na ujenzi wa skuli ya ghorofa iliyopo Mabanda ya ng’ombe Chumbuni.

Nyingine ni Ukarabati wa barabara ya Saaten hadi Shirika la Umeme Gulioni pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika Wilaya hiyo.

Aidha wamezitaja Changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa ajira kwa vijana, tatizo la udhalilishaji wa kijinsia na baadhi ya watendaji wa serikali kuwadharau viongozi na watendaji wa Chama.

Pamoja na hayo mabalozi hao wameahidi kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinashinda na kuendelea kuongoza Dola.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni