Alhamisi, 3 Mei 2018

DK.SHEIN ATANGAZA VITA DAWA ZA KULEVYA Z'BAR.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akiwa na viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zake katika ziara ya kuimarisha Chama ya kuzungumza na mabalozi wa mashina wa CCM Wilaya ya Micheweni Pemba.

MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amesema hatokubali Zanzibar kugeuzwa uchochoro wa kupitisha, kuuza na kusambaza dawa za kulevya.

Msimamo huo ameutoa leo wakati akihutubia mabalozi na viongozi wa ngazi za mashina wa Wilaya ya micheweni Pemba, amesema haiwezekani dawa za kulevya kuthibitiwa Tanzania bara na kituo cha kuuza dawa hizo kikahamia visiwani Zanzibar.

Ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vya Idara maalum za SMZ kuongeza ulinzi na kuhakikisha watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya kisheria.

“Haiwezekani Zanzibar kuwa kituo cha kufanya biashara za dawa za kulevya na kuangamiza nguvu kazi ya nchi, vyombo vya ulinzi hakikisheni kila muhusika anakamatwa kisheria hata akiwa ni Mwana CCM ama mtu yeyote ndani ya Chama na serikali.

Zanzibar haikuwa na vitendo hivyo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wachache kwa tama za kupata fedha za haraka huku wakiangamiza vizazi vya sasa na nguvu kazi ya baadae.

Kupitia mkutano huo Dk.Shein amewataka mabalozi kutoa taarifa sahihi juu ya matukio mbali mbali ya kuhatarisha amani ya nchi yanayotoikea katika jamii kwani wao wapo karibu zaidi za wananchi wa ngazi za chini.

Makamo Mwenyekiti huyo amesema anatambua na kuthamini mchango wa viongozi wa CCM ngazi za mashina wakiwemo mabalozi kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Dk.Shein amewasihi viongozi hao kwamba ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi ni lazima wasome na kuchambua kwa kina majukumu yao yaliyotajwa katika Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.

Pamoja na hayo Dk.Shein ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewakumbusha mabalozi hao kwamba licha ya kukabiliwa na majukumu mbali mbali bado wanatakiwa kuendeleza na mikakati ya kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi(CCM),katika uchaguzi Mkuu ujao.

Pia Dk.Shein ameahidi kuzitafutia ufumbuzi  changamoto zinazoikabili wilaya hiyo zikiwemo kumaliza tatizo la ukosefu wa nishati ya umeme katika kijiji cha Kijongwani, ujenzi wa barabara ya kutoka kijiji cha Kiuyu kwenda Micheweni pamoja na ujenzi wa daharia katika skuli ya sekondari ya Chwaka chumbe katika Wilaya ya Micheweni.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi amesema Chama Cha Mapinduzi kimesimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2018 katika Wilaya ya micheweni na kuwatoa wananchi katika kiwango cha umasikini uliokithiri na kufikia kiwango cha uchumi wa kati.

Alisema kupitia sera imara za CCM zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, wataendelea kuimarisha huduma muhimu za kijamii ili kila mwananchi anufaike na maendeleo hayo.

Aidha Dk. Mabodi ameeleza kwamba Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuimarika kisiasa, kijamii na kiuchumi kutokana na kuwa karibu na wananchi wa makundi yote sambamba na kutekeleza kwa wakati ahadi zinazokidhi mahitaji yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mbwerwa Hamad Mberwa ameipongeza serikali kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM katika Nyanja mbali mbali na kueleza kuwa hatua hiyo imekijengea heshima kubwa Chama mbele ya wananchi.

Katika risala yao mabalozi wa Wilaya hiyo wamesema CCM ni Chama chenye nia ya dhati ya kumaliza changamoto za wananchi wa makundi yote bila ya ubaguzi.

Wamesema katika jitihada za kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi viongozi na watendaji wa ngazi hizo wameendelea kuwafariji wananchama ili waendelee kushikamana licha ya kukabiliwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa wapinzani.

Wameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi januari hadi april mwaka 2018 Chama ngazi ya wilaya na jumuiya zake kimefanya ziara ya kutembelea ngazi za mashina kwa lengo la kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa ngazi hiyo.

Wameomba kupatiwa mafunzo kwa lengo la kuongeza uelewa na ufahamu mzuri wa masuala mbali mbali ya kisiasa, kwa lengo la kuiletea ushindi CCM kwa kila uchaguzi.

Hata hivyo wameeleza kwamba wataendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, ili serikali iweze kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni