Jumatatu, 9 Aprili 2018

SMZ NA CHINA WAZINDUA TEKNOLOJIA YA KILIMO CHA MPUNGA.

 WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud(kushoto wa pili) akimkabidhi zawadi ya mlango mdogo Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke, ikiwa ni ishara ya kuendeleza mahusiano baina ya Zanzibar na China.
  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud(kushoto wa pili) akimkabidhi zawadi ya mlango mdogo wataalamu wa kilimo.


 MGENI Rasmi Waziri Aboud Mohamed Aboud akiwasha pikipuki maalum ya kubebea mpunga kutoka bondeni ambayo ni miongoni mwa vifaa vya kisasa vilivyotolewa na Serikali ya China kwa wakulima wa bonde la Cheju waliofundishwa teknolojia mpya ya kilimo cha mpunga.
 


  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud, akiwahutubia wananchi katika uzinduzi wa mashamba ya maonyesho ya kilimo bora cha mpunga na makabidhiano ya vifaa kwa ajili ya kilimo hicho kutoka serikali ya China  iliyofanyika bonde la Cheju Mkoa wa Kusini Unguja.

WAZIRI wa Kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi Rashid Ali Juma akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga bonde la Cheju.
 BONDE la mpunga la Cheju Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 

WAZIRI wa Kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi Rashid Ali Juma akitoa maelezo katika shamba darasa la kilimo cha mpunga katika bonde la Cheju.
 MKULIMA wa zao la mpunga kutoka Mkoa wa Pwani Zulfiker Mituro, akitoa ushuhuda baada ya kunufaika na kilimo hicho .

 WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar  Aboud Mohamed Aboud(kushoto) akibadilishana mawazo na Balozi wa Tanzania Nchini China Wang Ke, katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.
 Balozi wa Tanzania Nchini China Wang Ke, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.
 BAADHI ya wananchi na wataalamu wa masuala ya kilimo kutoka China wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Aboud Mohamed Aboud amewataka wakulima  wa zao la mpunga kuchangamkia fursa ya teknolojia ya kisasa ya kilimo hicho kutoka nchini China.

Wito huo ameutoa leo katika hafla ya uzinduzi wa mashamba ya maonyesho ya kilimo bora cha mpunga na makabidhiano ya vifaa kwa ajili ya kilimo hicho kutoka kwa serikali ya China.

Hafla hiyo iliyofanyika katika bonde la mpunga la Cheju lililopo Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo Waziri huyo  amesema kilimo hicho kimefanyiwa tafti mbali mbali Tanzania bara na kubaini kina uwezo wa kuzalisha tani 4.5 hadi tani tisa kwa heka moja.

Aboud aliyemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd katika hafla hiyo, amewasihi wakulima wa mpunga visiwani Zanzibar kuipokea teknolojia hiyo na kuifanyia kazi ili wapate mavuno ya uhakika na kupunguza umaskini.

“ Itumieni vizuri teknolojia hii ya kilimo cha kisasa cha mpunga hakika mtapata mafanikio na Cheju itakuwa eneo maarufu kwa uzalishaji wa mpunga mwingi utakaosaidia serikali kupunguza uagizishaji wa chakula cha mchele kutoka nje ya nchi.” Amesema 

Teknolojia hii imekuja wakati mwafaka ikizingatiwa mchele ndio chakula kikuu hapa visiwani Zanzibar, na wakulima mkiweza kwenda sambamba na ujuzi na mbinu za kilimo hiki, naamini tutafikia kiwango cha kuwa na chakula cha kutosha hapa nchini”, anafafanua, Aboud.

Waziri Aboud ameeleza kuwa urafiki baina ya China na Zanzibar ulianza kuimarika baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na baada ya hapo China imekuwa ikitoa misaada katika sekta mbali mbali za SMZ na binafsi.

Ameahidi kuwa Serikali  itaendelea kushirikiana na China ili kuhakikisha wananchi wa nchi zote mbili wananufaika na mahusiano hayo ya kudumu na yenye tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza Waziri wa kilimo, maliasili, uvuvi na mifugo, Rashid Ali Juma amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya kilimo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanaondokana na kilimo duni na kufanya kilimo chenye manufaa ya kupata mazao mengi katika eneo dogo.

Amewasisitiza wakulima waliopewa taaluma hiyo mpya kuwa walimu wa kuwafundisha wakulima wengine ili teknolojia hiyo isambae katika mabonde mbali mbali hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi wa China Nchini Tanzania, Wang Ke amesema kilimo hicho kimekuwa ni sehemu ya mafanikio ya uzalishaji wa chakula cha kutosha katika taifa la China.

Amefafanua kuwa kilimo hicho kinafanyika kwa mfumo wa kanuni za kitaalamu kupitia utaratibu wa teknolojia hiyo, hivyo wakulima wanatakiwa kuwa makini ili wapate mazao mengi kwa kila msimu wa kilimo.

Amesema mbali na teknolojia hiyo pia taifa la China limetoa vifaa mbali mbali vya kumsaidia mkulima aweze kurahisisha kazi wakati wa kilimo.

Pia amesema baada ya kusambaza teknolojia hiyo ya zao la mpunga katika maeneo mbali mbali nchini, wataendelea kutoa teknolojia zingine zikiwemo ukulima bora wa mboga mboga na maboga.

Mapema Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao ameeleza kuridhishwa kwake na hatua za uimarisha wa serikali ya kilimo zinazotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema CCM inaisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kikamilifu ili wakulima wanufaike na sekta ya kilimo na kujinasua wimbi la umaskini na utegemezi wa chakula.

" Nampongeza Dk. Shein kwa kasi yake ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, na tukio la leo ni sehemu ya juhudi zake kwa kufungua milango ya ushirikiano na taifa la China.", amesema Catherine.

Amewambia wakulima wa bonde hilo kuwa wanatakiwa kuwa wabunifu pindi wanapofundishwa matumizi ya teknolojia hiyo ili wataalamu hao waweze kuwapa ujuzi wa teknolojia tofauti za kilimo.













                              



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni