MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Ofisi ya Jimbo la Donge.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu
Hassan amesema wakati umefika wa Serikali kuzuia uchimbaji wa mchanga katika maeneo ya Donge Chechele ili kuepuka madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo.
Ushauri huo ameutoa leo katika mwendelezo wa ziara
zake kichama katika Mkoa wa Kaskazini
Unguja, Amesema serikali isipochukua maamuzi magumu ya
kudhibiti uchimbaji mchanga katika maeneo hayo, visiwa vya Zanzibar vitatoweka.
Amesema miongoni mwa njia za kupunguza uharibifu wa mazingira
katika maeneo hayo ni kuweka mkazo katika matumia ya njia mbadala za ujenzi
unaotumia mchanga kidogo kuliko unaotumiwa hivi sasa.
“Haiwezekani tukaendelea kufumbia macho hali hii
inayosababisha hatari kubwa katika mazingira yetu, kwani maeneo yanayochimbwa
sioni juhudi za kuyarejesha katika hali yake japo kupanda miti ili ardhi ainze
kurudi katika sehemu zake.
Pia wananchi msiangalie fedha za siku moja mnazopata
katika shughuli za uchimbaji mchanga bali muangalie na vizazi vyenu mtaviacha
katika mazingira ya aina gani na mjiulize watalima na kujenga wapi kama maeneo
yote yakishaharibiwa.”, amesema Mhe. Samia.
Amesisitiza kuwa kila mwananchi anatakiwa kulinda
mazingira yasiharibiwe ikizingatiwa Zanzibar ni nchi ya visiwa.
Baadhi ya takwimu mbali mbali za kimazingira
zilizowahi kufanyika nchni, zinaeleza kuwa miaka 50 ijayo visiwa vya Zanzibar
vipo hatarini kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa
mazingira unaoendelea kufanyika.
Pia mhe. Samia ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ametembelea miradi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja
katika eneo la uwekezaji katika kijiji cha Nungwi.
Akizungumza katika eneo hilo Mhe. Samia ameuagiza
uongozi wa CCM kutumia vizuri vitega uchumi vya miradi ya Chama ili Mkoa huo na
Wilaya zake zijitegemee kiuchumi.
Amekemea vitendo vya ubadhirifu na uhujumu wa mali za
Chama na kuweka wazi kuwa mtu yeyote mtu yeyote atakayebainika anahujumu miradi
ya chama hatobaki salama.
Katika ziara hiyo pia amefungua Ofisi ya CCM Jimbo la
Donge na kuwataka Wana CCM wa jimbo hilo kutumia Ofisi hiyo ipasavyo kwa
kufanya vikao na mikutano ya kikatiba ya kuimarisha Chama.
Wakati huo huo amefungua Ofisi ya CCM Mkoa wa
Kaskazini Unguja, na kuwataka viongozi wa Mkoa huo kuendeleza juhudi za
kurejesha katika mstari hali ya kisiasa katika Mkoa huo.
Amesema huu sio wakati wa Wana CCM hasa viongozi
kurumbana na kutengeneza migogoro isiyokuwa na tija, bali washikamane na
kukijenga Chama ili kipate ushindi wa kihistoria katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Idd Ali Ame
amefafanua kuwa viongozi mbali mbali kuanzia wazi hadi Mkoa wamejipanga
uchaguzi Mkuu ujao wanashinda kwa ngazi zote hadi kiwango cha asilimia 70.
Katika Mkutano wa ndani uliofanyika katika Ofisi mpya
ya Mkoa huo, zaidi ya wanachama wapya 5501 wamekabidhiwa kadi za CCM na Jumuiya
zake.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni