Ijumaa, 20 Aprili 2018

CCM YAWATAKA WANANCHI KUFUATA MAELEKEZO YA SMZ

KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni Bakari Hamad Khamis(kulia) akizungumza na uongozi wa CCM Mkoa wa Mjini chini ya Mwenyekiti wa Mkoa huo ndugu Talib Ali Talib (wa pili kushoto), kabla ya kuanza ziara ya kuwafariji wananchi waliopata maafa yaliyotokana na mvua.

 VIONGOZI wa CCM wakiongozwa na Katibu wa NEC, Idara ya organazesheni ndugu Bakari wakiangalia nyumba za wananchi wa shehia ya Sebleni zilizovamiwa na maji ya mvua yaliyojaa katika bwawa lililopo katika maeneo hayo.

 NYUMBA  ya mkaazi wa sebleni Masoud Issa iliyopo katikati ya maji katika eneo hilo.
 SHEHA wa shehia ya Kwa wazee Khalfan Salum akitoa maelezo juu ya nyumba za wananchi zilizopata maafa ya mvua katika eneo la shehia yake.

 NYUMBA za wananchi wa maeneo ya Kwa wazee zilizoingiliwa na maji ya mvua za masika.

 MTAA wa mtumwa jeni Jimbo la magomeni lililoathiwa na maji ya mvua kutokana na baadhi ya wananchi kujenga katika njia za kusafirisha maji ya mvua.

 KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni Bakari Hamad Khamis(kulia)akizungumza na Mwenyekiti wa CCM jimbo la Magomeni Mahmoud Juma Ali katika ziara ya kuwafariji wananchi waliopata maafa jimboni humo.

 DARI ya nyumba ya mzee Ali Haji Makame iliyoharibika kutokana na mnazi kuangukia nyumba yake huko Pwani mchangani.

 NYUMBA ya Bi. Jina Makame Hamdu iliyoanguka kutokana na mvua zinazonyesha nchini huko Chaani kubwa Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

 MMOJA wa wanafamilia ya Bi. Jina akitoa maelezo juu ya athari walizopata katika maafa hayo.


 NYUMBA ya Juma Khamis Mohamed iliyoporomoka kwa mvua huko Chaani kubwa Wilaya ya Kaskazini Unguja.



 KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni Bakari Hamad Khamis kimfariji mkaazi wa shehia ya Mkwajuni ndugu Kero Chumu Juma ambaye ukuta wa nyumba yake umeanguka kutokana na mvua.



 KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni Bakari Hamad Khamis akizungumza na bi.Maua Vuai Ame mkaazi wa shehia ya Kiwengwa ambaye nyumba yake imeezuka kutokana na maafa hayo.


 KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni Bakari Hamad Khamis na msafara wake wakiwa katika eneo la shughuli za uvuvi huko Mwanga pwani Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja, kwa ajili ya kuwafariji wananchi ambao boti sita zimeharibiwa na maafa hayo

 BOTI aina ya ngwanda iliyoharibika kutokana na mvua zinazonyesha huko mwanga pwani.

 JOPO la viongozi wa CCM wakisikiliza maelezo kutoka kwa wakaazi wa maeneo hayo ya mwanga pwani.

 BOTI iliyoharibika kutokana na maafa hayo katika eneo la mwanga pwani.



CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka wananchi kufuata maelekezo na ushauri wa Serikali juu ya kujikinga na maafa yanayotokana na mvua za masika.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakar Hamad Khamis, alipotembelea maeneo mbali mbali yaliyoathiriwa na mvua katika Mikoa ya Mjini na Kaskazini Unguja.

Alisema kila mwananchi anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo ya Serikali hasa  kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi kwa lengo la kujikinga na madhara hayo yanayosababishwa na mvua za masika zinazonyesha kila mwaka nchini.

Bakari alisema lengo la ziara hiyo ni kuwafariji wananchi wote waliopata majanga sambamba na kuitaka serikali kupitia mfuko wa maafa iharakishe misaada kwa wananchi ambao nyumba zao zimebomolewa na mvua hizo.

Akizungumza Katibu wa Wilaya ya Mjini Fatma Shomari, alisema katika Wilaya hiyo jumla ya nyumba 68 zimeathiriwa na mvua hizo pamoja na kusababisha kifo cha mtoto Ramadhan Juma Khamis (4) katika shehiya ya Sebleni.

“Bado tunaendelea kukusanya taarifa za wananchi mbali mbali waliopata maafa katika Wilaya yetu ili tuziwasilishe kwa serikali kwa ajili ya hatua stahiki za misaada”, alisema Katibu huyo.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Kwa wazee Khalfan Salum alieleza kuwa jumla ya nyumba 130 zenye wakaazi wanaokisiwa kufikia 1300 zimeathiriwa na mvua hizo na wananchi wa maeneo hayo wamehama na kutafuta hifadhi kwa majirani waliopo katika maeneo salama.

Akizungumza mkaazi wa eneo hilo Haji Makame ‘London’ aliiomba serikali kupitia Manispaa ya mjini kuharakisha mradi wa ujenzi wa mtaro mkubwa utakaokuwa ukisafirisha maji yanayotwaama katika maeneo hayo ambayo kwa sasa ni makaazi ya kudumu kwa wananchi.

Aidha Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mulla Othaman Zubeir alisema zaidi ya nyumba 18 na boti sita za uvuvi aina ya mtando na ngwanda zimeharibiwa na mvua zilizonyesha katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo na kuathiri mali za wananchi.

Mbali na maafa hayo Mulla alifafanua kuwa maafa hayo yamesababisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja aliyetumbukia katika shimo la takataka katika shehia ya Chaani kubwa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Akiwafariji wananchi wa Mkoa huo Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakari Hamad aliuagiza uongozi wa CCM Mkoa huo kusaidia shughuli za ujenzi wa nyumba ya Mkaazi wa shehia ya Mwange Mbaki Makame Ali (54), ambaye nyumba yake imeanguka kutokana na mvua zinazonyesha nchini.

Katibu huo wa Organazesheni Bakari aliwasihi wananchi waliopata maafa kuwa wavumilivu kwa kipindi hichi, huku Chama Cha Mapinduzi kikiendelea kuisimamia serikali iharakishe misaada kwa wananchi waliopata maafa hayo.

Naye mkaazi wa shehia ya Mkwajuni  Kero  Chumu Juma alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuendeleza utamaduni wa waasisi wa ASP waliokuwa wakiwatembelea wananchi mara kwa mara kwa lengo la kuratibu changamoto zao na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali.

“Nimefurahi sana kuona uongozi wa CCM umekuja kunifariji kwani utamaduni huu ulikuwa umepotea kwa muda mrefu na kwa sasa naona umerudi kwa kasi kubwa, hii inaonyesha wazi kuwa Chama kinarudi kwa wananchi wake”, alisema Mkaazi huyo ambaye ukuta wa nyumba yake ulianguka kutokana na mvua hizo.

Maeneo yaliyotembelewa katika ziara hiyo ni shehia ya Sebleni, Kwa wazee, eneo la Mtumwa jeni, Pwani mchangani, Chaani kubwa, shehia ya Kibeni, Shehia ya Mwange, shehia ya Mkwajuni na Mwanga pwani.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni