Ijumaa, 6 Aprili 2018

BALOZI SEIF APOKEA MATEMBEZI YA KUMUENZI KARUME, VIJANA 450 WASHIRIKI

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Idd akihutubia  vijana walioshiriki matembezi hayo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na vijana katika kilele cha matembezi hayo yaliyofanyika kisiwandui leo.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza katika kilele cha matembezi hayo yaliyofanyika kisiwandui leo.

KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Abdulghafari Idrissa Juma akizungumza katika kilele cha matembezi hayo yaliyofanyika kisiwandui leo

 MKE wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume akitoa nasaha kwa vijana na Wana CCM walioshiriki matembezi ya kumuenzi marehemu Abeid Aman Karume

 VIONGOZI wa CCM, UVCCM na SMZ pamoja na Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar  Mama Fatma Karume, wakiongozwa na Balozi Seif Ali Idd kupokea matembezi hayo.
 VIJANA wa UVCCM wakiwa na picha mbili ya muasisi mzee karume na picha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein


 VIONGOZI wa CCM, UVCCM na SMZ pamoja na Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar  Mama Fatma Karume, wakiwa katika matembezi hayo

VIJANA wa UVCCM wakiwa katika matembezi ya kumuenzi marehemu mzee Abeid Karume yaliyofanyika kutoka kijiji alichozaliwa cha mwera kiongoni hadi katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui eneo alilozikwa.


 VIJANA walioshiriki matembezi wakiwasili Kisiwandui.




MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kuwatoza fedha wananchi huduma ambazo serikali imetangaza kuwa zitolewe bure.

Amezitaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni huduma za afya na matibabu, elimu ngazi ya msingi hadi sekondari pamoja na ardhi heka tatu zilizogawiwa baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Akizungumza katika mapokezi ya matembezi ya kumuenzi Marehemu Mzee Abeid Karume yaliyofanyika katika uwanja wa Afisi Kuu CCM Zanzibar yaliyoandaliwa na UVCCM na kushirikisha   vijana 450 waliotembea kutoka Mkoa wa Kusini Unguja Mwera Kiongoni hadi Mkoa wa Mjini Magharibi Kisiwandui.

Kupitia hotuba aliyoitoa balozi katika mapokezi hayo amesema mtumishi yeyote wa umma anayewatoza wananchi fedha katika huduma zilizotangazwa na serikali kuwa ni bure kufanya hivyo ni kinyume na sheria.

Amefafanua kuwa hivi sasa kuna baadhi ya watu wasiowaaminifu wanauza heka tatu za ardhi zilizotolewa na serikali kwa wananchi na serikali ikiingilia kati kutatua migogoro baadhi ya wananchi wanatoa kauli zisizofaa.

Pia ameeleza kuwa tabia hizo zinafanyika katika hospitali za umma kuna baadhi ya watumishi wanawatoza wananchi fedha katika huduma za afya hali ya kuwa serikali imetangaza huduma za matibabu na vipimo ni bure.

“ Hatutowavumilia watumishi wanaokwenda kinyume na maelekezo na busara za marehemu mzee abeid karume zinazoendelea kuenziwa na Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Shein”, alisema balozi seif.

Amewambia vijana hao kuwa wana kila sababu ya kumuenzi mwasisi huyo wa mapinduzi kutokana na juhudi zake za kuikomboa Zanzibar na kuwa taifa huru linalojitawala kiuchumi na kiuongozi.

Balozi Seifa amesema kupitia sera ya elimu bure iliyoasisiwa na marehemu Karume Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu mpaka sasa imepata vijana wengi wasomi kupitia Vyuo vikuu vitatu vinavyomilikiwa na SMZ.

Ametoa tahadhari kwa vijana kutambua kuwa jamii ya watu waliomuua mzee Abeid Karume bado wapo mpaka leo na wanatamani kuja kuitawala tena Zanzibar , jambo ambalo haliwezekani.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa njia pekee ya kulinda mema, busara na maelekezo ya mwasisi huyo wa Mapinduzi ni kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuongozwa na Serikali iliyowekwa madarakani na CCM hivyo wanatakiwa kuipigania nguvu zote ili ishinde katika uchaguzi Mkuu ujao.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zannzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi amesema CCM inaendelea kuenzi mema yote yaliyoasisiwa na ASP kupitia aliyekuwa kiongozi mkuu wa Chama hicho Mzee Abeid Karume.

Amesema  vijana wa ASP walitoa sadaka maisha yao kupigania haki isimame katika ardhi ya waafrika wa visiwa vya Zanzibar ili kila mwananchi aweze kuishi kwa amani na utulivu.

“ Zanzibar toka enzi na enzi ilikuwa ni milki ya waafrika hivyo ASP kuwaondosha wavamizi waliotutawala kimabavu haikuwa dhambi bali ni sehemu ya kuleta ukombozi kwa wananchi wote”, alisema Dk.Mabodi amefafanua.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita amesema  vijana wapo tayari kuyaendeleza mema yote yaliyoasisiwa na mzee Abeid Karume.

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Abdulghafari Idrissa Juma alisema ukweli ni kwamba mzee karume aliuawa na wapinga maendeleo kwa lengo la kuhujumu maendeleo ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa wakati wa kuwafumbia macho watu wanaopeza na kudharau fikra, mema na maelekezo ya  CCM nao ni sehemu ya wapinga maendeleo  ya Zanzibar.

Akitoa nasaha kupitia mapokezi hayo Mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume amelipongeza jeshi la Wananchi Tanzania pamoja na Serikali zote mbili kwa kumuenzi muasisi huyo sambamba na kulitunza kaburi la mzee karume likawa katika mazingira bora.

Matembezi hayo hufanyika kila  April 6, ya kila mwaka kwa lengo la kumuenzi muasisi wa ASP na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni