VIONGOZI wa ngazi mbali mbali za Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya Diman, wakisoma Dua katika kaburi la Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Aman Karume.
WANACHAMA
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kuendeleza harakati za kulinda,
kutetea na kusimamia misingi ya taasisi hiyo ili kuenzi kwa vitendo juhudi za
waasisi wa ASP na TANU.
Hayo ameyasema Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Dimani Hassan Suleiman Jaku katika ziara ya watendaji na viongozi mbali mbali wa Wilaya hiyo walipotembelea maeneo ya historia ya kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman Karume, Kisiwandu Unguja.
Amesema nguvu za Chama Cha Mapinduzi zinatokana na wanachama wazalendo wanaolinda na kuthamini urithi wa Chama hicho toka enzi za vyama vya ASP na TANU.
Katibu huyo Mwenezi amesema lengo la ziara hiyo ni kuwajengea uwezo watendaji wa Chama hasa wenye dhamana ya masuala ya itikadi na uenezi wajue uhalisia wa historia ya nchni ili nao wawafundishe wanachama wengine.
Amesema viongozi hao wamepewa darasa la itikadi na kujifunza mambo mbali mbali darasani na kwa sasa wamefikia hatua ya kujifunza kwa vitendo na kwenda katika maeneo mbali mbali ya kihistoria na kujionea wenyewe maeneo hayo.
Ameeleza kuwa mambo mema yaliyoasisiwa na marehemu Karume na Wana Mapinduzi wenzake ni urithi wa kudumu unaotakiwa kuthaminiwa na kila mwananchi.
Pia ameeleza kuwa moja ya mbinu ya kushinda mbinu chafu za wapinga maendeleo ni kuhakikisha CCM inashinda na kuendelea kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao.
“ Tusomeni historia ili tuwe na ujasiri wa kulinda neema hizi tulizorithiwa na wazee wetu na baadae vizazi vyetu viweze kujifunza mambo mema kukoka kwetu na kupigania nchi yao ibaki katika mikono ya Serikali ya CCM.”, amesema Hassan.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Dimani, Abdallah Maulid amesema viongozi, wanachama na watendaji kwa ujumla wanatakiwa kujifunza historia halisi ya Zanzibar kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upotoshwaji zinazosambazwa na wapinzani.
Amesema vijana wa CCM wanatakiwa kujiunga na madarasa ya Itikadi kwa lengo la kujifunza masuala mbali mbali ya historia, Demokrasia na mwenendo wa siasa za visiwa vya Zanzibar.
Katika ziara hiyo wametembelea eneo alilouwawa marehemu Abeid Aman Karume pamoja na kumuombea dua katika eneo la kaburi alipozikwa Mwasisi huyo wa Mapinduzi
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni