WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar wakikagua
boti na vifaa vya kisasa vilivyopo katika Hoteli ya Kimataifa ya Verde huko Mtoni
Marine Zanzibar. |
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
WAJUMBE wa Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Zanzibar wamesema CCM itaendelea
kuisimamia Serikali ikusanye kwa wingi mapato bila kuruhusu uvujaji wa
rasilimali fedha.
Wamebainisha kuwa hatua hiyo itasaidia nchi kujitegemea
na kuondokana na mfumo wa kutegemea baadhi ya fedha za wadau wa maendeleo zenye
masharti yanayokwenda kinyume na Ustawi wa kijamii na Utamaduni wa wananchi wa
Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe hao, Mjumbe wa NEC
Ndugu Amini Salmin Amour huko katika Kituo cha ufugaji wa Kasa Mnarani Nungwi,
ameeleza kwamba endapo Serikali itazidisha kasi ya usimamizi na ubunifu wa
vyanzo vipya vya mapato Zanzibar itakuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa.
Ndugu Amini ameeleza kwamba Sekta ya Utalii ni moja ya
Taasisi muhimu zinazochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia
fedha za kigeni.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi mbali
mbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Sekta ya Utalii na maeneo ya Uwekezaji
kwa lengo la kushauri na kutoa maelekezo kwa baadhi ya sehemu zenye changamoto
za kiutendaji.
Aliipongeza Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa utendaji wao
mzuri uliochangia kuimarika kwa taasisi hiyo na kufanikiwa kutekeleza kwa
kiwango kikubwa Ilani ya CCM.
Pamoja na hayo aliwasihi wananchi kuendeleza Utamaduni
wa kufanya Utalii wa ndani ili wajionee vivutio mbali mbali vya utalii
vilivyopo nchini pamoja na kufahamu historia na hatua za kimaendeleo
zilizofikiwa kupitia Sekta ya Utalii nchini.
Pamoja na hayo aliwapongeza Marais wote wawili ambao
ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kudhibiti vitendo vya ubadhilifu wa mali za umma huku wakibuni na kutekeleza
mikakati ya ukuaji wa Uchumi wa nchi.
Naye Kamishna wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Mhe. Khamis Mbeto amesema kamisheni hiyo kwa
sasa tayari imevuka malengo ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyoelekeza kuwa
ifikapo mwaka 2020 Zanzibar itakuwa na Watalii 500,000 ambapi kwa sasa tayari
idadi ya Watalii inakaribia kufikia 600,000 kabla ya mwaka 2020.
Ameeleza kuwa lengo la Kamisheni hiyo ni kutengeneza
mazingira rafiki ya kukarabati baadhi ya miundombinu iliyopo katika Vivutio vya
Utalii nchini ili wageni na wenyeji mbali mbali wanaotembelea maeneo hayo wawe
mabalozi wazuri wa kuendelea kutangaza vivutio hivyo kwa wananchi wengine.
Akieleza mikakati mbali mbali ya kiutendaji inayotekelezwa
na Kamisheni hiyo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt.Abdallah Mohamed Juma amesema kamisheni hiyo inashirikiana vizuri na taasisi za kimataifa
zinazoshughulikia masuala ya Utalii ili kupata mbinu za kisasa zitakazoleta
ufanisi wa kimaendeleo ndani ya sekta hiyo.
Aliitaja miongoni mwa mikakati hiyo ni uwepo wa Vituo
maalum vya Matangazo na Uratibu wa takwimu na taarifa za masuala mbali mbali ya
Utalii katika Viwanja vya Ndege pamoja na Bandari Kuu ya Zanzibar Malindi
pamoja na Vituo vidogo vidogo katika maeneo mbali mbali nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni
hiyo, Dkt. Miraji Ussi, alieleza kuwa kamisheni hiyo inafanya ukarabati mkubwa
katika Vivutio mbali mbali vilivyopo nchini hasa katika eneo la Kihistoria
linalolojulikana kama Bihole lililopo katika Kijiji cha Bungi katika Mkoa wa
Kusini Unguja ili wananchi wa maeneo hayo na maeneo mengine wapate sehemu nzuri
ya kutembelea na kufanya shughuli za kibiashara.
Dkt. Miraji alifafanua kwamba mpaka sasa tayari
wamekamilisha ramani ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa kama Soko la
ujasiriamali,hoteli na bustani ya kisasa na eneo maalum michezo ya watoto na
makumbusho ambayo itakarabatiwa kwa kufuata vigezo vya awali vya eneo.
Wajumbe hao walitembelea maeneo mbali mbali yakiwemo
eneo la Uwekezaji wa Hoteli ya Kisasa ya Verde, Uwanja wa Ndege wa Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume,Bandari Kuu ya Zanzibar, Eneo la Kihistoria la Bihole
pamoja na Kituo cha kufuga Kasa kilichopo Nungwi katika Mkoa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni