NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akiwaonyesha moja ya ripoti ya ukaguzi wa miradi watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja(hawapo pichani)
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WATENDAJI wa Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kujenga
utamaduni wa kufanya ziara za kiutendaji kwa wananchi wa ngazi zote ili
kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zinazowakabili wananchi.
Rai hiyo ameitoa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.
Abdulla Juma Saadalla Mabodi katika mwendelezo wa ziara zake za kukagua
utekelezaji wa Ilani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.
Amesema lazima watendaji na viongozi waliopewa dhamana ya
kusimamia mfumo wa ugatuzi washuke kwa wananchi kwa lengo la kufuatilia masuala
mbali mbali yatakayosaidia kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi katika
ngazi za serikali za mitaa.
"Lengo la Serikali Kuu kushusha madaraka katika
Serikali za Mitaa kupitia dhana ya ugatuzi ni kuongeza ufasini wa uimarishaji
wa huduma za kijamii kwa wananchi, hivyo watendaji nyote mlioaminiwa na kupewa
dhamana ya kuwahudumia wananchi lazima muwe katibu na jamii", amesisitiza
Dk.Mabodi.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amewataka
wamewasihi watendaji hao kuwa wabunifu katika kuibua miradi mbali mbali ya
kijamii inayoweza kuongeza ufanisi wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Pia Dk. Mabodi kupitia ziara yake hiyo ameelezea kuridhishwa
kwake na utendaji mzuri wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'A' katika
kutekeleza vizuri miradi inayotekelezwa kupitia ugatuzi.
Dk. Mabodi aliwasihi wananchi kuendelea kuthamini na kuamini
juhudi kubwa za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Saba ya
Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein, kwa utekelezaji mzuri wa Ilani
ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'A' Mussa Ali Makame, amesema katika
ukusanyaji wa mapato katika mwaka 2018/2019 wamekisia kukusanya shilingi
milioni 869,300,000 hadi Novemba wamekusanya kiasi cha shilingi milioni
157,697,081 sawa na asilimia 18.
Amesema Halmashauri hiyo imetoa mafunzo kwa wakulima 144 ili
kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula cha biashara.
Aidha ameeleza kuwa wametoa mafunzo kwa wafugaji 1,027 wa
ng'ombe na mbuzi kwa lengo la kuwajengea uelewa wa matumizi ya huduma ya
chanjo.
Mussa amesema jumla ya Shule 32 za Wilaya ya Kaskazini 'A'
Unguja ambapo wanafunzi 6,158 wa maandalizi wamepatiwa huduma ya lishe kwa
mwaka wa fedha kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 pamoja na 2018/2019.
Akizungumza Mjumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya
CCM Taifa Zanzibar Amini Salmin Amour, amewataka wataalamu wa fani mbali mbali
waliopelekwa katika mfumo wa ugatuzi kutumia ujuzi wao kuwaelimisha wananchi
juu ya masuala ya kilimo bora, ufugaji, uvuvi sambamba na kuhakikisha miradi
yote inayotekelezwa inawanufaisha watu husika.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idd Ali Ame, amempongeza
Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi kwa ziara yake hiyo ambayo ameitaja kuwa
imeongeza ari na kasi ya watendaji kutatua kero za wananchi kwa wakati.
Kwa upande wake Mkaazi wa Kijiji cha Mbuyu Tende Ramadhan
Ali Mcha ameeleza kuwa mfumo wa ugatuzi umewasaidia wananchi kupata huduma
muhimu za kijamii.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni