Jumanne, 11 Desemba 2018

KAMATI MAALUM YA NEC CCM Z'BAR, YAUNGA MKONO KUSAINIWA KWA MKATABA WA UZALISHAJI WA MAFUTA NA GESI (PSA).

 WAJUMBE wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar wakiwa katika Kikao cha kawaida kinachofanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu, huko Kisiwandui Afisi Kuu Zanzibar.

KAMATI Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar imekutana chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, imeunga mkono juhudi za Serikali kusaini Makubaliano ya Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia (PSA) na Kampuni ya RAKGAS ya Ras al Khaimah ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Akitoa ufafanuzi jana Disemba 11, mwaka 2018 juu ya masuala mbali mbali yaliyoazimiwa kupitia Kikao hicho Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi', huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, ameeleza kwamba Kikao hicho kimeipongeza Serikali kwa kusaini mkataba huo na kueleza kuwa ulifuata taratibu zote za kisheria.

Dk. Mabodi amesema maamuzi ya kusaini mkataba huo yametokana na kukamilika kwa taratibu mbali mbali za kisheria kwa pande zote za Muungano ambapo kupitia maamuzi ya kisheria Zanzibar imepewa mamlaka ya kuchimba na kusimamia yenyewe masuala ya Mafuta na Gesi.

Amesema kufanikiwa kwa mchakato huo wa kusainiwa mkataba huo ni hatua kubwa ya maendeleo iliyofanywa na Dk.Ali Mohamed Shein, kwa kushirikiana na Viongozi mbali mbali wakiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jonh Pombe Magufuli.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi ameeleza kwamba Kikao hicho kimelaanmi vikali kitendo cha kuvuja mitihani ya Kidatu cha Pili na kutaka watu wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi kutokana na usaliti wao ulioisababishia hasara kubwa Serikali.

Aidha Dk.Mabodi alifafanua kwamba jambo jingine lililoazimiwa kupitia kikao hicho ni  kukemea  vitendo vya udhalilisha wa kijinsia vinavyoendelea katika maeneo mbali mbali nchini, na kuiagiza Serikali idhibiti vitendo hivyo kwani vinasababisha madhara kwa watu wanaotendewa uhalifu huo.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo alisema Kikao hicho kilikuwa cha kawaida, na kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni