Jumamosi, 22 Desemba 2018

NAIBU KATIBU MKUU WAZAZI ATUA Z'BAR, MAPOKEZI YAKE HAIJAWAHI KUTOKEA.

 NAIBU Katibu Mkuu wa Wazazi Ndg.Othman Ally Maulid akivishwa koja mara baada ya kuwasili Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa kushika wadhifa wake. 

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya ya Wazazi Zanzibar,Najma Murtaza Giga, amemtaka Naibu Katibu Mkuu mpya wa jumuiya hiyo, Othman Ally, kuendeleza mabadiliko yaliofanyika ndani ya jumuiya ikiwemo kutunza na kuthibiti mali za jumuiya hiyo. 

Giga amesema jumuiya hiyo kwa sasa inaendana na mabadiliko hayo ambayo jumuiya imeshirikiana na chama katika kuzitunza mali hizo.

Amesema  jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi(CCM),kimefanikiwa kuwabaini na kuwatia nguvuni waliohusika na upotevu wa mali za jumuiya hiyo hivyo ni vyema kwendana na mabadiliko hayo.

Mbali na hilo, Giga amesema  jumuiya hiyo iko salama na kwamba hakuna tuhuma zozote zilizoikumba wanachama wa jumuiya katika suala la usaliti na mambo mengine.

Kauli hiyo ameitoa katika hafla ya mapokezi ya mrithi wake kiungozi mjini Unguja ambapo amesema anamkabidhi jumuiya hiyo ikiwa katika hali ya usalama ikiwemo kutokuwepo kwa majungu na makundi.

"Hali hii inatokana na kuwepo kwa upendo baina ya viongozi wa jumuiya hiyo ikumbukwe katika jumuiya hii hakuna viongozi waliopatikana na suala la usaliti wa tuhuma zozote zile," amesema

Naye Naibu Katibu Mkuu huyo mpya, Othman Ally alisema atahakikisha anaendeleza hatua zilizofanyika na uongozi uliopita kwa kuzingatia katiba na misingi ya jumuiya hiyo.

Amesema  jukumu lilokabidhiwa ni kubwa ikiwemo kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 CCM ina shinda na kwamba lazima wanachama wa jumuiya hiyo watoe ushirikiano ili kutekeleza azma ya ushindi wa chama katika uchaguzi huo.

"Tufanye kazi kwa ushirikiano tuache makundi,majungu na hata hivyo ninamshukuru Rais na Mwenyekiti wa Taifa John Magufuli kwa kuendelea kukijengea heshima chama,"amesema 

Ameongeza kuwa kazi ambayo ataendelea kufanya ni pamoja na kuhakikisha jumuiya hiyo inaongeza idadi ya wanachama katika CCM na kwamba hatokubaliana na kuwepo kwa makundi ndani ya jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar wa CCM,Dk.Abdallah Sadala Juma 'Mabodi' amewataka  wanajumuiya na viongozi wa jumuiya hiyo kumpa ushirikiano Naibu Katibu Mkuu huyo mpya katika kutekeleza maendeleo ya CCM.

Amesema jumuiya hiyo ni chachu,tegemeo kubwa kwa chama katika kusimamia maadili na mambo ya kisiasa hivyo wanachama wa jumuiya wanapaswa kuelewa kuwa jumuiya hiyo ina historia ndefu.
"Jumuiya hii ndio msimamizi wa kazi za chama hivyo tunatakiwa tumpe ushirikiano wa kutosha Naibu huyu mpya mimi nimefurahi kuwa tumempata mtu makini na tunakukaribisha katika utendaji kichama,"ameeleza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni