WAKILISHI wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk,(kushoto) akikabidhi Vyakula mbali mbali vikiwemo Mchele, Unga wa Ngano na Mafuta ya kula kwa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Chukwani Mohamed Abdallah Mohamed(kulia), kwa ajili ya Wanafunzi waliopo katika kambi ya maandalizi ya Mitihani ya Kidato cha Nne kwa Skuli hiyo.
|
WANAFUNZI wanaojiandaa kufanya Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne Mwaka huu, Visiwani Zanzibar wametakiwa kusoma kwa bidii ili wafaulu mitihani hiyo.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk, katika mwendelezo wa ziara zake katika Mkoa wa Magharib,wakati akikabidhi Vyakula kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Chukwani kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mitihani kwa mwaka huu.
Mwakilishi huyo amewasihi Wanafunzi hao kusoma kwa bidii ikiwa ni sehemu ya maandalizi rasmi ya kuwawezesha kufaulu.
Amesema wanafunzi hao wakifaulu vizuri watapata nafasi ya kuendelea na masomo ya ngazi za juu hadi kufikia Chuo Kikuu, hatua inayohitaji juhudi binafsi za kila mwanafunzi.
Pamoja na hayo amewasisitiza wanafunzi hao kuachana na vitendo visivyofaa hasa kushiriki katika masuala ya dawa za kulevya, mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo sambamba na matumizi mabaya ya simu.
Akipokea Vyakula hivyo Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Chukwani Mohamed Abdallah Mohamed, ameshukru kwa msaada huo na kueleza kuwa utawasaidia wanafunzi hao kupata Chakula kwa wakati na kupata muda wa kusoma vizuri katika kambi hiyo.
Mwl.Mohamed, amesema kuwa Uongozi wa Skuli hiyo umejipanga vizuri kwa kuwaanda vizuri wanafunzi hao 122 wanaotarajiwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne kwa Mwaka huu.
Vyakula vilivyotolewa na Mwakilishi huyo ni pamoja na Mchele,Sukari, Unga wa Ngano pamoja na Mafuta ya kula.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni