Jumatano, 23 Oktoba 2019

UWT MKOA WA MAGHARIB WAANZA ZIARA MAJIMBO 13.


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Magharibi Kichama Ndugu Zainab Ali Maulid, akizungumza na Wanawake wa Umoja huo katika Jimbo la Dimani huko Kombeni Unguja katika ziara ya Kamati ya utekelezaji ya Mkoa huo ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika Majimbo 13 ya Mkoa.

Akina Mama wa UWT jimbo la Dimani wakiwemo Wajasiriamali wa  kutengeneza bidhaa mbali mbali wakisikiliza mada zinazotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Magharibi katika ziara hiyo maalumu ya kuimarisha uhai wa CCM.

MJUMBE wa Kamati utekelezaji ya Mkoa wa Magharibi kichama Asha Makungu Othman,akizungumza katika ziara ya UWT Jimbo la Dimani Unguja.

 MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Magharibi Maulid Mohamed Othman, akizungumza katika ziara hiyo na akina mama wa UWT jimbo la Dimani.


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania(UWT) Mkoa wa Magharibi kichama Ndugu Zainabu Ali Maulidi, amewaagiza uongozi wa ngazi za matawi hadi wilaya mkoani humo kuandaa mipango mikakati ya kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Agizo hilo amelitoa katika ziara maalumu ya Kamati ya Utekelezaji ya UWT ya Mkoa huo ya kutembelea Majimbo 13 ya Umoja huo huko katika Jimbo la Dimani Unguja,amesema huu ni wakati wa kazi hivyo kila mwanachama anatakiwa kutumia kutumia uwezo na maarifa yake kuhakikisha Chama kinashinda.

Zainabu,amesema mipango mikakati hiyo baada ya kuandaliwa ni lazima itekelezwe kwa vitendo ili kuongeza tija katika mipango ya kujiimarisha kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainabu,amesema ziara hiyo itafanyika kwa majimbo yote ya Mkoa huo na kusikiliza changamoto na ushauri wa viongozi, Watendaji na wanachama wa ngazi mbali mbali kisha kutoa maelekezi yatakayosaidia Utatuzi wa changamoto hizo.

Akitoa mada ya udhalilishaji Mjumbe wa Kamati utekelezaji ya Mkoa huo ndugu Asha Makungu Othman, amesema licha ya serikali kutunga sheria za kudhibiti uhalifu huo bado umeendelea kufanyika kwa kasi na kuwaathiri Watoto na Wanawake.

Ameshauri jamii kufanya mikutano ya mara kwa mara ya zoni na shehia kuvitumia vikundi vya polisi jamii kuthibiti udhalilishaji huo kama walivyodhibiti vitendo vya uhalifu wa aina mbali mbali mitaani.

Amesema tatizo linalochangia kuongezeka kwa udhalilishaji ni jamii kuacha malezi,utamaduni na desturi za zamani badala yake kufuata utamaduni wa kigeni unachongia kuporomoka kwa maadili.

kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Fatma Ali Ameir, akizungumza katika ziara hiyo amewasihi akina mama hao kuepuka kufanya kampeni za kuwanadi watu wenye nia ya kugombea uongozi kabla ya wakati uliopangwa kisheria.

Amewaomba viongozi na wanachama ndani ya UWT wafuate miongozo,kanuni na maelekezo ya Katiba za Umoja huo na Chama cha Mapinduzi ili kujiepusha na migogoro.
  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni