Ijumaa, 4 Oktoba 2019

MHE.AIFARIJI FAMILIA YA KADA WA CCM ALIYEPOTEZA NYUMBA KWA AJALI YA MOTO


 MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe.Amina Idd Mabrouk(kushoto) akimfariji na kumkabidhi Magodoro Kada wa CCM aliyepata ajali ya kuungua kwa Nyumba yake hivi karibu Ndugu Amina Wajihi Kitwana (kulia), makabidhiano hayo yamefanyika Nyumbani kwao Kwa Mchina Zanzibar.


MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe.Amina Idd Mabrouk,amewashauri Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla kuendeleza Utamaduni wa kuwafariji wananchi wenzao wakati wanapokabiliwa na majanga mbali mbali yanayosababisha kupoteza mali na maisha ya watu.

Rai hiyo ameito wakati alipofanya ziara ya kumtembelea Kada wa CCM Bi.Amina Wajihi Kitwana aliyepata ajali ya kuungua kwa nyumba yake na kifo cha Mtoto mmoja hivi karibuni huko Mombasa SOS Zanzibar.

Akizungumza Mhe.Amina Idd huko nyumbani kwao kada huyo huko kwa Mchina,ametoa pole kwa familia ya kada huyo na kumsihi aendelee kuwa na moyo wa subira kwa kipindi hiki na kutambua kuwa Wanachama wa CCM wako pamoja naye wakati wote.

Amesema suala la Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kusaidiana wakati wa majanga kama hayo ni jambo muhimu kwani wananchi wanaopata majanga wanakuwa katika wakati mgumu wa kimaisha hivyo wanatakiwa kufarijiwa ili waondokana na mawazo mabaya yanayoweza kuwaletea madhara ya Kisaikolojia.

Mwakilishi huyo Amina aliyefuatana na Viongozi wa UWT Wilaya ya Dimani,ametoa msaada wa Magodoro kwa familia ya Kada huyo ikiwa ni sehemu ya kumfariji kwa kumpatia vifaa hivyo vitakavyotumika kwa malazi ya familia yake.

Katika maelezo yake Mhe.Amina, alikishukuru Chama Cha Mapinduzi na Serikali pamoja na Wananchi mbali mbali waliojitokeza kumsaidia kwa masuala mbali mbali kada huyo mara baada ya kupata majanga hayo.

Naye Kada huyo aliyepata ajali ya kuungua kwa nyumba yake bi.Amina Wajihi Kitwana, amemshukuru Mwakilishi huyo wa Viti Maalum kwa mchango wake alioutoa kwani utasaidia kupunguza changamoto katika familia hiyo.

Amesema ajali hiyo imetokea na kusababisha hasara kubwa ya kupoteza mali na kifo cha Mtoto jambo ambalo kwa upande wake amelichukulia kama ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwa sasa anajipanga kutafuta makaazi mengine ya kuishi kwani kwa sasa anaishi kwa Mama yake mzazi.

Ajali hiyo ya kuungua kwa nyumba ya kada huyo iliyotajwa kuwa imetokana na hitilafu za Umeme ilitokea siku za hivi karibuni na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na kuteketea kwa nyumba yote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni