Jumapili, 27 Oktoba 2019

NDG.CASSIAN -AZINDUA KITUO CHA UJASIRIAMALI JANG'OMBE.


 KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo(wa pili kutoka kulia),akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo cha mafunzo ya ujasiriamali cha Jimbo la Jang'ombe,Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Ramadhan Hamza Chande (wa kwanza kushoto) na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Jimbo hilo (wa kwanza kutoka kulia).
KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo akihutubia wananchi katika uzinduzi wa Kituo cha ujasiriamali Jang'ombe.
MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande,akizungumza katika hafla hiyo.




BAADHI ya Waalikwa na wanafunzi wa kituo hicho wakisikiliza nasahas mbali mbali kutoka kwa viongozi wa JImbo la Jang'ombe.

MWENYEKITI wa UVCCM Mkoa wa Mjini ndugu Kamaria Suleiman Nassor,akitoa shukrani katika hafla hiyo.

KATIBU wa Siasa na Uenezi CCM Jimbo la Jang'ombe akizungumza katika hafla hiyo.


KATIBU wa Kamati Maalumu ya NEC,idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ndugu Cassian Galos Nyimbo,amewataka Wanawake na Vijana wa jimbo la jang'ombe kutumia vizuri fursa ya ujasiriamali kwa kujiajiri wenyewe.

Wito huo ameutoa wakati akizindua Kituo cha Mafunzo ya Ujasiriamali cha Jimbo la Jang'ombe kilichoanzishwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo uko Kilimani Mnara wa mbao Unguja.

Amesema ujasiriamali ni kazi kama zilivyo kazi zingine katika jamii hivyo ujuzi unaotokana na sekta hiyo unatakiwa kuthaminiwa na kupewa kipaumbele.

Galos ameeleza kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali watakayopewa wananchi wa jimbo hilo kupitia Kituo hicho yawe na tija ya kujikwamua kichumi na kujiongezea kipato.

Katika maelezo ya Katibu huyo, amempongeza Mwakilishi huyo kwa ubunifu wake wa kuanzisha Kituo kitakachozalisha wataalumu wengi wa masuala ya ujasiriamali wenye uwezo wa kutengeneza bidhaa mbali mbali zenye viwango.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande,alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuwapatia ujuzi wa masuala ya ujasiriamali wananchi wa jimbo hilo hasa vijana na wanawake.

Amesema wakati alipokuwa akiomba wananchi wampatie ridhaa ya uongozi aliahidi kuanzisha kituo hicho cha kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kwa sasa tayari ametekeleza ahadi hiyo.

Amesema katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 imeelekeza uanzishwaji wa vituo vya mafunzo  ya ujasiriamali nchini, hivyo jimbo hilo wametekeleza maelekezo ya Ilani.

Amesema kituo kimesajiliwa na kupitia taratibu zote za kisheria pia wana wakufunzi waliobobe katika kufundisha utengenezaji wa bidhaa bora zinakubalika katika soko la ndani na kimataifa.

Aidha ameeleza kuwa kituo hicho kwa awamu ya kwanza kinatarajia kutoa Wanafunzi zaidi ya 300 na kitakuwa ni endelevu.

Akitoa shukrani katika hafla hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mjini ndugu Kamaria Suleiman Nassor, amewapongeza viongozi wa jimbo la Jang'ombe kwa ushirikiano wao uliozaa matunda ya kuanzisha kituo hicho kitakachowanufaisha Vijana wengi.

Amewasihi vijana wa jimbo hilo kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga kituo hicho ili wapate ujuzi utakaowawezesha kutengeneza bidhaa zitakazowapatia kipato.

Jumamosi, 26 Oktoba 2019

MHE.RAMADHAN HAMZA CHANDE -AZING'ARISHA MASKANI ZA CCM JANG'OMBE.



MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande (kushoto) ,akimkabidhi mabati saba ya kuezekea maskani ya Bora Imani iliyopo Urusi Jang'ombe ndugu Omar Said Salum 'Saa nane' (wa nne kutoka kulia)

MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande (kushoto) , akimkabidhi fedha taslimu shilingi 70,000 Mjumbe wa maskani ya Karume ndugu Ibarahimu Abass Faki kwa ajili ya matengenezo ya maskani hiyo.
 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande (kushoto), akimkabidhi fedha na mabati Katibu wa Masskani ya Buda iliyopo Ziwani Ndugu Ramadhan Salmin Songoro.

 KATIBU wa Siasa na Uenezi CCM Jimbo la Jang'ombe ndugu Ali Ahmad Ibrahim akizungumza na Wana Maskani ya Ramadhan Hamza Chande katika ziara ya Mwakilishi huyo ya kutembelea maskani za CCM. 



 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande akiwa na viongozi na wanachama wa maskani Buda.

 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande akikabidhi Mabati kwa Uongozi wa Maskani ya Mtundani iliyopo Matarumbeta Jang'ombe Zanzibar.

 MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande akizungumza na Wana maskani ya  CCM Kidongochekundu Zanzibar.


MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande (kushoto),akimkabidhi seti moja ya jezi Meneja wa timu ya mpira wa miguu ya Kidongo chekundu City ndugu Omar Shamna (kulia).
 KATIBU wa Siasa na Uenezi CCM Jimbo la Jang'ombe ndugu Ali Ahmad Ibrahim akizungumza n Wana Maskani ya CCM ya Ramadhan Chande katika ziara ya Mwakilishi huyo katika Jimbo hilo.
MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande  akikabidhi Uongozi wa Maskani ya Ramadhan Hamza Chande Mabati ya kuezekea Maskani hiyo.

MWAKILISHI wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande, ametoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 1.5 kwa maskani nane za Chama Cha Mapinduzi zilizomo katika jimbo hilo.

Akizungumza katika mwendelezo wa ziara zake katika maskani mbali mbali za CCM jimboni humo, Mhe.Ramadhani amesema vifaa hivyo ambavyo ni Mabati ya kuezekea nyumba, Jezi za mpira wa miguu na fedha taslimu ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizowaahidi wananchi katika kampeni za uchaguzi zilizopita.

Alisema kwamba wakati akiomba ridhaa ya wananchi katika jimbo hilo aliahidi kuzipatia vifaa hivyo maskani za Chama Cha Mapinduzi zilizokuwa na changamoto mbali mbali  zilizotakiwa kutatuliwa na viongozi wa Chama.

Alieleza kuwa katika uongozi wake ndani ya jimbo hilo ataendelea kuwa karibu na Wananchi wa makundi yote, bila kubagua rika zao kwani kila mmoja ana umuhimu wake katika maisha ya kisiasa.

Katika maelezo yake Mwakilishi huyo Mhe.Ramadhan, aliwambia viongozi na makada wa maskani hizo kuwa Chama Cha Mapinduzi kinawathamini kutokana na mchango wao wa kuimarisha taasisi hiyo Kisiasa na Kiuchumi.

Alitoa nasaha zake kwa  wanachama mbali mbali wa maskani hizo kubuni miradi  ya ujasiriamali ili Vijana,Wanawake na Wazee wapate sehemu mbadala ya kujiingizia kipato.

Katika ziara hiyo aliwakumbusha Wananchi hasa Wana CCM kuhakiki vitambulisho vyao vya mzanzibar mkaazi sambamba na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate uhalali kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alieleza kwamba kutokana na kazi aliyopewa na Wananchi wa Jimbo hilo ametekeleza Ilani ya Chama kwa zaidi ya asilimia 70 na anaendelea kukamilisha ahadi zake ili ifika mwishoni mwa mwezi Desemba awe amemaliza utekelezaji wa ahadi zake.

"Nawashukru sana Viongozi wenzangu wa jimbo letu wakiwemo mbunge ,madiwani na viongozi wote wa Chama na Jumuiya zake kwa ushirikiano wenu, ulioteta tija kubwa kwa wananchi wetu wote.

Naye Diwani wa wadi ya Kwaalinatu Mhe.Fatma Suleiman Juma, amewataka wananchi kuendelea kujali na kuitunza  miradi ya maendeleo inayotekelezwa na viongozi wa CCM ili idumu kwa muda mrefu kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Diwani wa wadi ya Urusi Mhe.Ibrahimu Abass Faki, amesema kwamba jimbo hilo limeendelea kuimarika kimaendeleo kutokana na ushirikiano wa viongozi wake katika kutekeleza Ilani ya CCM.

Akizungumza Katibu wa Siasa na Uenezi wa Jimbo hilo Ali Ahmad Ibrahim, amesema ziara hiyo imeongeza hamasa kubwa wa wana maskani hao kwani changamoto zao za muda mrefu zimetafutiwa ufumbuzi na kudumu na mwakilishi huyo.

Ameongeza kuwa kila mwanachama na viongozi wa CCM ndani ya jimbo hilo anatakiwa kuandaa vizuri zana zake za mapambano ya vita ya kisiasa kuelekea 2020,kwani muda kusema kwa maneno umepita na kilichobaki ni kutekeleza kwa vitendo.

Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Mjini kichama ndugu Habiba Nasib Suleiman, amemshukru Mwakilishi huyo kwa kutekeleza Ilani ya CCM na kuwataka Viongozi wengine wa Wilaya hiyo kufuata nyayo za kiongozi huyo kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kutatua changamoto zinazowakabili.


























Alhamisi, 24 Oktoba 2019

CCM ZANZIBAR YAPOKEA UJUMBE KUTOKA CHAMA CHA CPC CHINA.


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, akizungumza na ujumbe wa watu watano kutoka Chama cha Kikoministi cha China (CPC), walipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha (CPC) Mhe.Guo Yezhou,akivishwa sikafu na Vijana Maalumu wa UVCCM baada ya kuwasili Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.



NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, leo ameupokea Ujumbe wa Watu  watano kutoka Chama Cha Kikoministi Cha China (CPC).

Ujumbe huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha (CPC) Mhe.Guo Yezhou wamewasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Viongozi wengine walioshiriki mapokezi hayo ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa,Wajumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar,Wenyeviti wa CCM wa Mikoa,Makamu Wenyeviti wa Jumuiya  na Watendaji wa ngazi mbali mbali za Chama.  

Mara baada ya mapokezi hayo ujumbe huyo uliwasili Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Kisiwandui Zanzibar na kuweka shada la maua katika kaburi  la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.  

Lengo la ziara ya ujumbe huo kutoka Jamhuri ya Watu wa China ni kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliodumu kwa miaka mingi baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikoministi cha China (CPC).

Aidha,Viongozi hao wa Vyama hivyo vyenye undugu wa muda mrefu watazungumzia masuala mbali mbali sambamba na kubadilishana uzoefu wa Kisiasa, Kiuchumi,Kijamii. 

 Ziara hiyo ya CPC itakuwa ya siku mbili visiwani Zanzibar.

Jumatano, 23 Oktoba 2019

WANAWAKE UWT JIMBO LA DIMANI WAPIGWA MSASA.


 KATIBU wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Zuwena Suleiman Mohamed,akizungumza katika ziara hiyo na Viongozi na Wanachama wa UWT Jimbo la Dimani.

 MKUFUNZI wa masuala ya uwezeshaji  kutoka Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar Zanzibar  Safia Mwinyi, akitoa mada ya uwezeshaji kwa akina Mama wa UWT Jimbo la Dimani.

 WAJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji wa UWT Mkoa wa Magharibi kichama wakiwa katika Ofisi ya UWT Jimbo la Dimani Unguja kwa ajili ya ziara maalumu.

 WANAWAKE wa UWT Jimbo la Dimani wakisikiliza nasaha za Uongozi wa UWT Mkoa wa Magharibi waliofanya ziara katika Ofisi ya jimbo hilo.

 MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Maghabi kichama Ndugu Mwaka Abrahman, akiwasalimia akina mama wa UWT  jimbo la Dimani.

 Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Zainab Abdalla Salum akitoa akizungumza katika ziara hiyo.


KATIBU wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Zuwena Suleiman Mohamed,amewataka kulipa ada zao kwa wakati uliopangwa na umoja huo.

kauli hiyo ameitoa katika ziara ya UWT ya Mkoa huo huko katika Jimbo la Dimani iliyofanyika katika Tawi la CCM Kombeni Unguja, alisema sifa ya uanachama hai inatimia kutokana na ulipaji wa ada wa mwanachama.

Katika maelezo yake Katibu Zuwena, amewasisitiza viongozi hao kufanya vikao kwa mujibu wa Katiba ya UWT ya mwaka 1978 toleo la mwaka 2017.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji wa Mkoa huo Maulid Mohamed Othman, amewambia wanawake hao waendelee kuhamasisha vijana na wanachama wengine wajitokeze kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pindi muda wa zoezi hilo utakapofika.

Amesema ushindi wa CCM utatokana na uwepo wa takwimu nzuri za wanachama wenye sifa ya kupiga hivyo kila mwanachama ana wajibu wa kuwa balozi wa kuhamasisha watu wengine wenye sifa za kuiunga mkono CCM.

Akizungumza Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Magharib kichama Mhe.Mwanaid Kassim Mussa, ametoa wito kwa wanachama hao kuwa wanatakiwa kuwa wamoja ili kuzikabili changamoto za kisiasa na kuhakikisha Chama na Jumuiya zake zinaimarika.


Akitoa mada ya mikopo, mkufunzi kutoka Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar  Safia Mwinyi, amewataka Wanawake wa UWT kuchangamkia fursa mbali mbali zinazopatikana katika idara ya Uwezeshaji zikiwemo mkopo wenye masharti nafuu na usikuwa na riba.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,wameimarisha  idara ya uwezeshaji ambayo kwa sasa inatoa mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali na kutoa mikopo ya kuwainua wanawake kiuchumi.

Katika ziara hiyo Wawakilishi wa Viti Maalumu wa Mkoa huo ambao ni Mhe. Hamida Abdalla Issa, Mhe.Zainab Abdalla Salum na Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa wametoa vitendea kazi kwa Wadi mbili za UWT zilizopo katika jimbo hilo, ambavyo ni Katiba za UWT pamoja na Viti vya Ofisi.
                                                             

UWT MKOA WA MAGHARIB WAANZA ZIARA MAJIMBO 13.


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Magharibi Kichama Ndugu Zainab Ali Maulid, akizungumza na Wanawake wa Umoja huo katika Jimbo la Dimani huko Kombeni Unguja katika ziara ya Kamati ya utekelezaji ya Mkoa huo ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika Majimbo 13 ya Mkoa.

Akina Mama wa UWT jimbo la Dimani wakiwemo Wajasiriamali wa  kutengeneza bidhaa mbali mbali wakisikiliza mada zinazotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Magharibi katika ziara hiyo maalumu ya kuimarisha uhai wa CCM.

MJUMBE wa Kamati utekelezaji ya Mkoa wa Magharibi kichama Asha Makungu Othman,akizungumza katika ziara ya UWT Jimbo la Dimani Unguja.

 MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Magharibi Maulid Mohamed Othman, akizungumza katika ziara hiyo na akina mama wa UWT jimbo la Dimani.


MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania(UWT) Mkoa wa Magharibi kichama Ndugu Zainabu Ali Maulidi, amewaagiza uongozi wa ngazi za matawi hadi wilaya mkoani humo kuandaa mipango mikakati ya kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Agizo hilo amelitoa katika ziara maalumu ya Kamati ya Utekelezaji ya UWT ya Mkoa huo ya kutembelea Majimbo 13 ya Umoja huo huko katika Jimbo la Dimani Unguja,amesema huu ni wakati wa kazi hivyo kila mwanachama anatakiwa kutumia kutumia uwezo na maarifa yake kuhakikisha Chama kinashinda.

Zainabu,amesema mipango mikakati hiyo baada ya kuandaliwa ni lazima itekelezwe kwa vitendo ili kuongeza tija katika mipango ya kujiimarisha kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainabu,amesema ziara hiyo itafanyika kwa majimbo yote ya Mkoa huo na kusikiliza changamoto na ushauri wa viongozi, Watendaji na wanachama wa ngazi mbali mbali kisha kutoa maelekezi yatakayosaidia Utatuzi wa changamoto hizo.

Akitoa mada ya udhalilishaji Mjumbe wa Kamati utekelezaji ya Mkoa huo ndugu Asha Makungu Othman, amesema licha ya serikali kutunga sheria za kudhibiti uhalifu huo bado umeendelea kufanyika kwa kasi na kuwaathiri Watoto na Wanawake.

Ameshauri jamii kufanya mikutano ya mara kwa mara ya zoni na shehia kuvitumia vikundi vya polisi jamii kuthibiti udhalilishaji huo kama walivyodhibiti vitendo vya uhalifu wa aina mbali mbali mitaani.

Amesema tatizo linalochangia kuongezeka kwa udhalilishaji ni jamii kuacha malezi,utamaduni na desturi za zamani badala yake kufuata utamaduni wa kigeni unachongia kuporomoka kwa maadili.

kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Fatma Ali Ameir, akizungumza katika ziara hiyo amewasihi akina mama hao kuepuka kufanya kampeni za kuwanadi watu wenye nia ya kugombea uongozi kabla ya wakati uliopangwa kisheria.

Amewaomba viongozi na wanachama ndani ya UWT wafuate miongozo,kanuni na maelekezo ya Katiba za Umoja huo na Chama cha Mapinduzi ili kujiepusha na migogoro.
  

Jumamosi, 19 Oktoba 2019

MAMA MWANAMWEMA SHEIN-AFUNGUA KONGAMANO LA WAJASIRIAMALI WA UWT UNGUJA.


 MKE  wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa  Kongamano la Mafunzo ya Ujasiriamali kwa Wanawake wa Mikoa ya Unguja yaliyoandaliwa na UWT  Zanzibar  na kufanyika katika Ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein SUZA-Tunguu.

  MKE  wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein akisalimiana na Viongozi mbali mbali wa UWT na Serikali walioudhuria katika Ufunguzi huo wa Mafunzo ya Ujasiriamali.

  MKE  wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein akikagua bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na Wajasiriamali hao wa Mikoa ya Unguja.






  MKE  wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein akielezwa Huduma zinazotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ambao ni moja ya Shirika lililodhamini Mafunzo hayo ya Ujasiriamali.

 BAADHI ya Wadhamini wa Mafunzo ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na UWT Zanzibar ambao ni Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) na Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC) wakiwa katika maonyesho hayo.

 BAADHI ya Viongozi na Wanachama wa CCM na Jumuiya zake wakisikiliza nasaha za Viongozi mbali mbali zinazotolewa katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Ujasiriamali kwa Wajasiriamali wa Zanzibar.


Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa.Bi.Thuwaiba Edington Kisasi,akizungumza katika kongamano hilo na kuwasisitizi Vijana na Akina Mama Mijini na Vijijini kuchangamkia fursa mbali mbali zinazopatikana katika Ujasiriamali ili wajikwamue kiuchumi na kujiongezea kipato.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo, akizungumza na kuwakaribisha Viongozi na Waalikwa mbali mbali katika Ufunguzi wa Kongamano hilo la Ujasiriamali lililofanyika  katika Ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein SUZA-Tunguu.

 Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akihutubia wakati akilifungua Kongamano la Wajasiriamali Wanawake Zanzibar linalofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu (SUZA) kulia Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar.Mhe. Maudline Castico na kushoto Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa.Bi.Thuwaiba Edington Kisasi, ufunguzi huo umefanyika leo.19-10-2019.  


MKE  wa Rais wa Zanzibar, mama Mwanamwema Shein amesema shughuli za ujasiriamali zinahitaji taaluma ili ziweze kufanyika kwa ufanisi na kuleta tija pamoja na kuondokana na changamoto.

Mama Mwanamwema amesema hayo katika ufunguzi wa Kongamano la  Wajasiriamali wanawake wa Mikoa ya Unguja, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, SUZA - Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema shughuli za ujasiriamali kama ilivyo shughuli nyengine zinahitaji elimu ya nadharia na vitendo ili kumwezesha mjasiriamali kupata tija na kuongeza kipato katika familia.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya saba inayoongozwa na Rais Dk. Shein imeunda Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto, pamoja na kaunzisha Mfuko wa Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili kufanikisha azma ya kukuza Sekta ya ujasiriamali.

Ameeleza kuwa Serikali imeandaa mipango mbali mbali ya kuwasaidia wananchi ili kuongeza kipato, hivyo akawataka wananchi kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo ili kuongeza kipato cha familia.
Aidha, Mama Mwanamwema ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kw uamuzi wa kuandaa kongamano hilo, ambapo pamoja na mambo mengine linazungumzia umuhimu wa kuimarisha Daftari la wapiga kura.

Alisema wakati huu wananchama wa CCM wakiajiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao mwakani, kuna umuhimu wa kukumbushana uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, hivyo akatowa wito kwa kila mmoja kushiriki na kutekeleza wajibu wake wakati utakapofika.

Amesema ushindi wa CCM utapatikana kupitia uimarishaji wa daftari hilo, kwa msingi kuwa bila ya kujiandikisha hakutakuwa na fursa ya mtu kupiga kura.

Amesema vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na matumizi ya dawa za kulevya  ni mambo yanayohitaji mikakati mizuri ya  haraka katika kupambana navyo.

Mama Mwanamwema amewataka washirki wa kongamano hilo kuwa makini na watulivu katika kipindi chote cha mafunzo ili kufikia malengo yaliokusudiwa, sambamba an kuwapongeza wafadhali mbali mbali waliowezesha kufanyika kongamano hilo.

Nae, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto Moudline Castico, alimpongeza Mama Mwanamwema kwa mchango mkubwa anautowa katika kusaidia harakati za ujasiriamali kwa akinamama.

Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Edington Kisasi, amesema lengo la Jumuiya hiyo kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu ya ujasiriamali nchi nzima.

Amewata washiriki wa mkongamano hilo kuitafutia ufumbuzi changamoto ya udhalilishaji wa kijinsia, akibainisha chanzo chake kinatokana na jamii kuondokana na utamaduni, mila na silka za Wazanzibari.

Ndugu Thuwayba amewapongeza wafadhali mbali mbali, ikiwemo ZRB, NMB, ZSSF, ZURA, Bima, Chuo Kiku cha Taifa SUZA na wengineo kwa michango yao iliyofanikisha kufanyika kongamano hilo.

Mapema, katika hafla hiyo Mama Mwanamwema amekagua bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na vikundi vya ujasiriamali kutoka Mikoa hiyo ya Unguja.

Jumanne, 8 Oktoba 2019

DK.MABODI- AWAPIGA MSASA MAKATIBU WA CCM MKOA WA KUSINI UNGUJA

 
 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla Mabodi, akifungua Mafunzo Elekezi kwa Makatibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja wa ngazi za Matawi hadi Mkoa yaliyofanyika Chuo Cha Utawala wa Umma Tunguu,  Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, amewata Makatibu wa Chama hicho kubuni masuala mbali mbali ya kiutendaji yatakayoongeza ufanisi katika Shughuli za Chama na Jumuiya zake.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Makatibu wa CCM ngazi za Matawi hadi Mkoa katika Mkoa wa Kusini Zanzibar, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utawala wa Umma Tunguu, Zanzibar.

Dk.Mabodi amesema mafunzo hayo yamefanyika katika wakati mzuri wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020,hivyo Watendaji hao wanatakiwa kujifunza kwa bidii ili watekeleze kwa ufanisi shughuli za Chama.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amewambia Makatibu hao kuwa wanatakiwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa miongozo ya CCM na kuepuka kufanya kazi za Wanasiasa ikiwa wao wanakabiliwa na majukumu ya kiutendaji.

Pamoja na hayo amesisitiza kila Mtendaji kuendeleza kwa vitendo dhana ya kushuka kwa wananchi wa ngazi mbali mbali kwa lengo la kuratibu changamoto zao ili zifanyiwe kazi na Mamlaka husika.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi amewasihi Makada Wasomi Nchini kuhakikisha elimu waliyonayo wanawafundisha Wanachama wengine ili Chama kiwe imara katika masuala ya Uongozi,Utawala,Uchumi na Kijamii.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, amewapongeza Viongozi mbali mbali wa Mkoa huo kwa juhudi zao za kulinda heshima ya Mkoa huo kwa vitendo na ukaendelea kuwa ngome ya CCM Kisiasa.

Kupitia ufunguzi wa mafunzo hayo Dk.Mabodi, amewakumbusha Watendaji kuepuka vitendo vya rushwa ndani ya Chama kwani vinasababisha madhara ya kupatikana kwa viongozi wasiokuwa waadilifu.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja ambaye pia ni Kimu Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Suleiman Mzee Suleiman amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji makatibu hao ili wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Amesema Mkoa huo licha ya kuwa ni ngome ya CCM bado baadhi ya Makatibu wake walikuwa na changamoto ya ukosefu wa uwezo wa kuandaa mitahsari na taarifa mbali mbali za Chama.

Akisoma risala Katibu wa CCM Jimbo la Tunguu Sharifa Maabadi, amesema mafunzo yatatolewa kwa siku Sita na yatawashirikisha Makatibu 120  kuanzia ngazi za wadi hadi Mkoa.

Ameeleza kuwa katika mafunzo hayo Makatibu watafundishwa masuala ya Uongozi,Uzalendo,itifaki kwa Viongozi,utunzaji wa habari na kumbukumbu na mbinu za kuzungumza na kuwashawishi watu kuendelea kujiunga na CCM.

Aidha ametoa rai kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu kwani yatawasaidia Viongozi na Watendaji wa CCM katika Mkoa huo kuwa na Weledi na mbinu mbali mbali za kufanya kazi za Chama Cha Mapinduzi kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.

Jumapili, 6 Oktoba 2019

MAMA SALMA KIKWETE-KIKUNDI CHA UTALII 255 COMMUNITY.


MKE wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Rashid Kikwete,akiwahutubia waalikwa mbali mbali katika Hafla ya Uzinduzi wa Utalii 255 Community uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert Ilala, Dar es Saalam.

MWENYEKITI wa Kikundi cha Utalii 255 Community Mhe.Angelina Adam Malembeka, akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Jumuiya ya masuala ya kuhamasisha na kutangaza Vivutio vya Utalii wa ndani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shaaban Robart, Dar es Saalam

 BAADHI ya Wageni mbali mbali walioudhuria hafla ya Uzinduzi wa kikundi cha Utalii 255 Community wakisikiliza nasaha mbali mbali zinazotolewa katika uzinduzi huo.


MKE wa Rais Mstaafu Mama Salma Rashid Kikwete amewasihi Wanawake Nchini kufuata nyayo za  Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe.Angelina Malembeka katika kubuni miradi mbali mbali yenye maslahi kwa jamii.

Wito huo aliutoa katika uzinduzi wa Kikundi cha Utalii 255 Community huko katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, Ikala Dar es saalam, ambapo kikundi hicho  kinachojihusisha na masuala ya sekta ya Utalii pamoja na shughuli za jamii katika uzalishaji zikiwemo ujasiriamali. 

Amesema Sekta ya Utalii ni fursa ya kuikomboa Nchi kiuchumi hivyo juhudi zilizofikiwa na Mhe.Angelina zinatakiwa kuthamini na kupongezwa ili zisaidie vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika maelezo yeke Mama Salma Kikwete,amekitaka kikundi hicho kufanya kazi zake kwa bidii kubwa kwa lengo la kwenda na mahitaji ya kutangaza vivuti vya Utalii.

Kupitia hafla hiyo ya uzinduzi Mama Salma Kikwete, amewasisitiza Wanawake na Vijana kujitokeza kuwania fursa za Uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Pamoja na hayo amewashauri viongozi mbali mbali hasa Wabunge kufungua milango ya Kutangaza Utalii katika maeneo wanayotoka ili kikundi hicho kiwafikie na kuhamasisha jamii juu ya fursa hizo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kikundi cha Utalii 255 COMMNITY  Angelina Malembeka, 
amesema  kikundi cha utalii 255 kilianzishwa mwaka 2017 kimesajiliwa Mambo ya Ndani na cheti cha Utambuzi kutoka Manispaa ya Ilala mwaka 2019.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kuwawezesha vijana wa makundi mbali mbali kunuika na fursa zinazopatikana katika kikundi hicho juu ya masuala ya Utalii sambamba na Ujasiriamali.

Aidha, ameeleza kuwa kikundi hicho kinafanya kazi zake kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara na muundo wa Wanachama wake wanatoka sehemu hizo kwa lengo la kuwaunganisha katika kuzifikia fursa za kukuza uchumi wa nchi.

Akizitaja baadhi ya kazi zinazotekelezwa na kikundi hicho kuwa ni kuelimisha juu ya ajira Binafsi ikiwemo ujasiriamali wa aina mbalimbali ufugaji,kilimo,uchoraji sanaa na kutangaza sekta ya Utalii wa ndani kwa jamii. 

Kwa upande wake Katibu wa Utalii 255 COMMUNITY Eveln Mwakatuma, amesema wanatarajia  kutembelea maeneo mbali mbali nchini, kwa sasa wameandaa safari ya Utalii kwa watoto yatima 100 ambao watakwenda kutembelea mbuga za wanyama watoto 50 kutoka Tanzania Tanzania Bara na 50 Zanzibar lengo la safari hiyo kujionea vivutio vya Utalii Tanzania.

Katika hafla hiyo Viongozi,Wanachama na waalikwa  mbali mbali walikabidhiwa Tuzo za heshima juu ya mchango wao katika kufanikisha shughuli mbali mbali za kijamii,kiuchumi na kimaendeleo.

Ijumaa, 4 Oktoba 2019

MHE.AIFARIJI FAMILIA YA KADA WA CCM ALIYEPOTEZA NYUMBA KWA AJALI YA MOTO


 MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe.Amina Idd Mabrouk(kushoto) akimfariji na kumkabidhi Magodoro Kada wa CCM aliyepata ajali ya kuungua kwa Nyumba yake hivi karibu Ndugu Amina Wajihi Kitwana (kulia), makabidhiano hayo yamefanyika Nyumbani kwao Kwa Mchina Zanzibar.


MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe.Amina Idd Mabrouk,amewashauri Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla kuendeleza Utamaduni wa kuwafariji wananchi wenzao wakati wanapokabiliwa na majanga mbali mbali yanayosababisha kupoteza mali na maisha ya watu.

Rai hiyo ameito wakati alipofanya ziara ya kumtembelea Kada wa CCM Bi.Amina Wajihi Kitwana aliyepata ajali ya kuungua kwa nyumba yake na kifo cha Mtoto mmoja hivi karibuni huko Mombasa SOS Zanzibar.

Akizungumza Mhe.Amina Idd huko nyumbani kwao kada huyo huko kwa Mchina,ametoa pole kwa familia ya kada huyo na kumsihi aendelee kuwa na moyo wa subira kwa kipindi hiki na kutambua kuwa Wanachama wa CCM wako pamoja naye wakati wote.

Amesema suala la Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kusaidiana wakati wa majanga kama hayo ni jambo muhimu kwani wananchi wanaopata majanga wanakuwa katika wakati mgumu wa kimaisha hivyo wanatakiwa kufarijiwa ili waondokana na mawazo mabaya yanayoweza kuwaletea madhara ya Kisaikolojia.

Mwakilishi huyo Amina aliyefuatana na Viongozi wa UWT Wilaya ya Dimani,ametoa msaada wa Magodoro kwa familia ya Kada huyo ikiwa ni sehemu ya kumfariji kwa kumpatia vifaa hivyo vitakavyotumika kwa malazi ya familia yake.

Katika maelezo yake Mhe.Amina, alikishukuru Chama Cha Mapinduzi na Serikali pamoja na Wananchi mbali mbali waliojitokeza kumsaidia kwa masuala mbali mbali kada huyo mara baada ya kupata majanga hayo.

Naye Kada huyo aliyepata ajali ya kuungua kwa nyumba yake bi.Amina Wajihi Kitwana, amemshukuru Mwakilishi huyo wa Viti Maalum kwa mchango wake alioutoa kwani utasaidia kupunguza changamoto katika familia hiyo.

Amesema ajali hiyo imetokea na kusababisha hasara kubwa ya kupoteza mali na kifo cha Mtoto jambo ambalo kwa upande wake amelichukulia kama ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwa sasa anajipanga kutafuta makaazi mengine ya kuishi kwani kwa sasa anaishi kwa Mama yake mzazi.

Ajali hiyo ya kuungua kwa nyumba ya kada huyo iliyotajwa kuwa imetokana na hitilafu za Umeme ilitokea siku za hivi karibuni na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na kuteketea kwa nyumba yote.