Jumanne, 24 Oktoba 2017

DK.MABODI AONGOZA MAMIA YA WANANCHI KATIKA MAZIKO YA KADA WA CCM MAREHEMU HASSAN VUAI HASSAN ''NYOMBOA".

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi leo ameongoza mamia ya wanachama na wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa Kusini Unguja marehemu Hassan Vuai Hassan ‘’Nyomboa’’ yaliyofanyika kijijini kwao Bwejuu Wilaya ya Kusini Unguja.

Marehemu huyo ambaye pia alikuwa ni Afisa Usalama na Maadili wa CCM Wilaya ya kusini Unguja ameumwa ghafla na kufariki dunia jana akiwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja  alikopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza Dk. Mabodi katika mazishi hayo amesema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na imepoteza kada jasiri aliyejitolea kwa muda mrefu kulinda na kutetea maslahi ya chama hicho.

Dk. Mabodi ameeleza kwa masikitiko kuwa CCM imepata pigo kubwa baada ya kumpoteza mwanachama huyo aliyefanya kazi za chama kwa ufanisi mkubwa bila ya kuchoka na atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa makada wengine wanaotakiwa kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.

Pia Dk. Mabodi alitoa salamu za pole kutoka kwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein aliyeelezea kusikitishwa kwake na kifo hicho na kuiomba familia ya marehemu kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.

“Marehemu Nyomboa ni mpiganiji mwenzangu tumekuwa wote toka tukiwa wadogo toka enzi za Paunia hadi tukawa wakubwa na tukaendelea kukitumikia chama, alikuwa ni mchapakazi na mtu wa watu.

Nasaha zangu sisi tuliobaki tuendelee kumuombea dua na kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.”, alieleza kwa uzuni Dk.Mabodi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja , Ramadhan Abdallah Ali alisema Mkoa huo umepoteza kiongozi na kada muhimu aliyekuwa ni mtu makini na asiyeyumba kwa kile anachoamini kuwa ni sahihi katika kuimarisha chama hicho kiitikadi na kisiasa.

Akisoma wasifu wa Marehemu Hassan Vuai Hassan, Kaimu Katibu wa CCM  Wilaya ya Kusini Unguja, Hafidh Hassan Mkadam amesema marehemu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka  66 na ametumikia chama, serikali  na Jumuiya zake kwa nafasi mbali mbali za uongozi na utendaji.

Marehemu Nyomboa enzi za uhai wake ameshika nyadhifa mbali mbali zikiwemo Afisa Utumishi Afisi ndogo ya Wazazi Zanzibar, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Wete Pemba, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Chunya, Mjumbe wa Kamati ya siasa wa CCM Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja, Diwani wa Wadi ya Paje.  

Katika wasifu wake marehemu ameacha vizuka wawili na watoto 13 na wajukuu 17.



Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pahali pema pepo Amini.

Baadhi ya makada wa CCM na Wananchi wakibeba jeneza la marehemu Hassan Vuai Hassan '' Nyomboa'' kulitoa msikitini na kulipeleka katika sehemu ya makaburi ya kijiji cha Bwejuu kwa ajili ya maziko.


 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi(kulia) aliyevaa kanzu na koti jeusi na miwani na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar  Ndg. Vuai Ali Vuai pamoja na wananchi wengine wakiwa katika maziko ya marehemu Nyomboa.

Baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali na Makada wengine na wananchi kwa ujumla walioudhuria mazishi ya marehemu Nyomboa wakiomba dua mara baada ya mazishi hayo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwa na familia ya marehemu Hassan Vuai Hassan ''Nyomboa'' wakimwombea marehemu dua. 

   
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akitoa mchango wa Ubani kwa  niaba ya Chama Cha Mapinduzi  katika Familia ya Marehemu Hassan Vuai Hassan.( PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR)

Jumapili, 22 Oktoba 2017

DK.MABODI : ASEMA MABALOZI WA MASHINA YA CCM NI WACHAPAKAZI.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kitaendelea kuthamini kwa vitendo  maarifa, mbinu na uchapakazi wa Mabalozi wa mashina katika kufanikisha harakati za maendeleo ndani ya chama hicho.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.  Abdalla Juma Mabodi wakati akifunga mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo juu ya Uchaguzi na Takwimu, Kazi za Mabalozi, Mageuzi katika CCM kwa Mabalozi wa CCM Jimbo la Mpendae Zanzibar, alisema mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya kuwaongezea uwezo katika utendaji wa shughuli zao za kila siku.

Alisema  mabalozi hao ndio uti wa mgongo wa CCM kwani wamekuwa wakijitolea kupigania maslahi ya chama hicho katika mazingira yoyote bila ya kuchoka wala kujali changamoto za kisiasa.

Dk. Mabodi alisema matarajio ya Chama cha Mapinduzi ni kuona mabadiliko ya kiutendaji katika mashina mbali mbali ya Jimbo hilo yanayoendana na maelekezo ya taaluma waliyopewa.

“ CCM tunajivunia kuwa na makada makini na wazalendo ambao ndio nyinyi mabalozi kwani kundi lenu lipo karibu zaidi na wananchi ambao ndio wapiga kura walioiweka madarakani CCM nasi tunakuahidini kuwa hatutowaangusha.

Kukutana kwenu katika mafunzo haya ni moja ya mafanikio kwani mmebadilishana uzoefu na mikakati itakayosaidia kuimarisha chama chetu na kikapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.”,  alieleza Dk. Mabodi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema miongoni mwa mambo ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na washiriki wa mafunzo hayo ni suala la takwimu  sahihi za wanachama ambao ndio mtaji  wa CCM kisiasa.

Alisema mabadiliko ya Kikatiba yaliyofanyika hivi karibuni ndani ya Chama hicho dhamira yake ni chama kurudi kwa wanachama wa ngazi za chini ambao ndio waliotoa ridhaa ya kuiweka serikali madarakani ili iweze kuwatumikia wananchi bila ubaguzi.

Hata hivyo alisisitiza kupitia Uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake ni lazima wapatikane viongozi wenye uwezo wa kuendelea Itikadi ya Chama na kuheshimu maadili ya uongozi kwa yanayosisitizwa kikatiba.

Hata hivyo aliwapongeza viongozi wa Jimbo hilo kwa kuandaa mafunzo hayo na kuyataka majimbo mengine kuiga utamaduni huo ili kuleta ufanisi wa pamoja ndani ya chama hicho.

Wakizungumza baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameahidi  kwa wakati tofauti wameahidi kuyafanyia kazi ili kwenda sambamba na malengo ya CCM kisiasa na kiutendaji.

Kwa upande Mbunge wa Jimbo hilo, Salim Turky alisema anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote na katika kupunguza tatizo la ajira ametoa mkopo wa shilingi milioni 200 kwa wananchi mbali mbali ili waweze kujiajiri na kuondokana na hali ya umasikini.


Jumamosi, 21 Oktoba 2017

CCM ZANZIBAR YAIFARIJI FAMILIA ILIYOPATA AJALI YA MOTO

CHAMA cha Mapinduzi (CCM)Z anzibar kimetoa mkono wa pole kwa familia iliyopata ajali ya kuungua moto nyumba na kusababisha vifo vya watu wanne huko katika kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi wakati wa kuifariji familia hiyo amesema CCM Zanzibar imesikitishwa sana na tukio hilo kwani limegharimu maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia.

 Dk. Mabodi alisema kwa niaba ya Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  anatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia hiyo na kuwasihi waendelee kuwa  na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba huo.

“ Kupoteza watu  Wanne katika familia moja  ni jambo zito linalotia huzuni lakini tuendelee kuwa wavumilivu kwani Allah amewapenda zaidi na sisi tuliobaki tuendelee kuwaombea  dua ili wapate makaazi mema na kusamehewa madhambi yao”, alitoa nasaha hizo kwa maskitiko makubwa Dk. Mabodi.”

Mapema Sheha wa Shehia ya Fumba, Mohamed Suleiman alifafanua kuwa nyumba hiyo ilianza kuwaka moto majira ya saa 6:15 usiku Oktoba 21 mwaka huu, ambapo wananchi mbali mbali walianza juhudi za kuzima moto huo na kushindwa kuokoa watu waliokuwa ndani kwani uliku ni mkubwa.

Suleiman alisema wakati juhudi za kuzima moto huo zikiendelea waliwasiliana na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar ambacho kilifika na kusaidiana na wananchi hao ambapo walizima moto huo na kukuta watu wanne tayari wamefariki dunia.

Akidhibitisha tukio tukio hiloalisema chanzo cha moto huo ni hitilafu za umeme zilizoanzia katika waya wa jokofu (Friji) lililokuwa likifanya kazi wakati wa usiku.

Kamanda Nassir aliwataja watu waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Bahati Ali Ameir (40), Sinawema Abdalla Ali, Hashim Abdalla Ali (6) na Latifa Mohamed Ali (8).

Alitoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuzima vifaa vya umeme wakati wa usiku ambavyo havina umuhimu wa kutumiwa wakati huo ili kuepuka majanga yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu.

Jumatatu, 16 Oktoba 2017

DK.MABODI ASHAURI PEMBEJEO ZA KILIMO WANAZOUZIWA WAKULIMA ZIWE NA UBORA.



 
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi ameishauriserikali kuhakikisha Pembejeo za kilimo wanazouziwa wakulima zinakuwana viwango vinavyoendana na mazingira ya kilimo yaliyopo nchini.


Ushauri huo ameutoa jana wakati akizindua msimu wa kilimo cha Mpungakatika mabonde yaliyopo katika Jimbo la Bububu na vitongozi vyake ukokatika bonde la Mahakani lililopo katika kijiji cha Kizimbani Wilayaya magharibi "A".


Alisema wananchi wengi wanafanya shughuli za kilimo katika mazingira magumu hivyo ni lazima taasisi za umma zinazohusika na kuuza pembejeo za kilimo ambazo ni mbolea, dawa na mbegu kuwa makini kwa kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi vigezo vya kilimo ili kuepusha hasara kwa wakulima.


Dkt. Mabodi alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwakilishi wa jimbo la Bububu, Mh. Masoud Abrahman Masoud kueleza kuwa katika msimu wa kilimo ulipita baadhi ya wakulima wanaolima mpunga katika mabonde ya mpunga ya jimbo hilo walipata walikosa mavuno kutokana na mpunga kukauka kwa sababu ya kutumia pembejeo mbovu zisizokuwa na viwango.


"Nitakaa na viongozi wa Wizara husika kwa lengo la kuwaeleza changamoto hiyo nao waweze kuifanyia kazi ili isiweze kujitokeza katika misimu ijayo.", alifafanua Dk. Mabodi na kuwasihi wakulima wasivunjike moyo kwani serikali yao ni makini na ina dhamira ya kuhakikisha ardhi ndogo iliyopo inatumika kwa kilimo cha kisasa.
Alieleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeahidi kuisimamia serikali kuhakikisha inaweka miondombinu endelevu ya kilimo itakayosaidia Zanzibar kulima mazao ya aina mbali mbali hasa mpunga kwa lengo la kupunguza uagizishiaji wa chakula kutoka nje ya nchi.

Alisisitiza wakulima hao kuhakikisha wanaendelea kufanya maandalizi mapema ya msimu wa kilimo cha mpunga na mazao mengine ili kwenda sambamba na msimu wa mvua kwa lengo la kupata mavuno mengi.

Hata hivyo aliwasihi kuwatumia wataalamu wa kilimo ili waweze kutoa ushauri wao juu ya mbegu zinazostahili kupandwa kwa mujibu wa maeneo husika ya kilimo.

Aliwapongeza viongozi wa Jimbo la Bububu ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani kwa ushirikiano wao unaozaa matunda ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020  kwa vitendo kwa kuanzisha mradi wa kilimo cha mpunga unaowanufaisha wakulima wengi wa jimbo hilo.

Akizungumzia uchaguzi unaondelea ndani ya CCM Dk.Mabodi alisema msimamo wa chama hicho ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa wanakuwa ni viongozi safi kimatendo, kimaadili na wanaokubalika katika jamii na wenye uwezo wa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa dola wa  mwaka 2020.

" Ajenda ya wapinzani ni kuzungumzia uchaguzi uliopita na kuzua na kuaminishana mambo ambayo hayawezekani kutekelezeka lakini CCM kazi yetu kubwa ni kuwapelekea maendeleo wanachama wetu popote walipo nasi tunawafikia", alisema Dk. Mabodi.

Sambamba na hayo Dk.Mabodi aliahidi kuchangia nusu ya fedha za kununua tirekta ndogo aina ya Powertiller ili iweze kuwasaidia wakulima hao katika shughuli za kilimo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Mh. Mwantakaje Haji Juma alisema mradi huo wa kilimo cha mpunga umeendeshwa kwa awamu tatu na kuwapatia wananchi mafanikio makubwa ya chakula na awamu ya sasa jumla ya shilingi milioni 16 zinatarajia kutumika fedha zitakazotolewa na mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.

Akisoma risala kwa niaba ya wakulima wa jimbo hilo, Bw. Saleh Said Njonjo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na kupunguziwa bei ya pembejeo za kilimo pamoja na kupunguziwa bei ya kulimiwa na matrekita ya serikali katika mabonde yao.


Hata hivyo alisema kuwa jumla ya wakulima 723 wa jimbo hilo na maeneo jirani watanufaika na mradi huo wa kilimo cha mpunga katika mabonde ya Mahekani, Tomokani, Mkanyageni, Mkuruwinda, Ndagoni, Mbuyuni Dole, Kichakani Bumbwisudi, Shamba ndogo, chemchem, kipanga na saraya.

Kwa upande wake mkulima wa bonde la mahekani, Bw. Abdalla Haji Abdalla amesifu juhudi za viongozi wa jimbo la Bububu kwa kuwajali wakulima wa jimbo hilo na kuelezea kuwa yeye ni mmoja kati ya watu walionufaika na mradi wa kilimo cha mbunga kwa awamu mbili zilizopita.
 

Jumapili, 15 Oktoba 2017

Picha Mbali mbali za Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar akizindua kilimo cha Mpunga katika Jimbo la Bububu, Zanzibar

 


 Mhe. Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dkt. Mabodi akisalimia na wananchi wa Jimbo la Bububu mara tu baada ya kuwasili katik bonde hilo la mpunga kwa lengo la kufanya uzinduzi wa kilimo cha mpunga 

Mhe. Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dkt. Mabodi akisalimia na Mwakilishi wa Jimbo la Bububu mara tu baada ya kuwasili katik bonde hilo la mpunga kwa lengo la kufanya uzinduzi wa kilimo cha mpunga

Mhe. Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dkt. Mabodi akijaribu Matreka ambayo yanyatarajiwa kufanyia kazi katika kilimo cha mpunga




















Jumatatu, 9 Oktoba 2017

DK. MABODI ATOA NASAHA NZITO CCM W/KASKAZINI "B" UNGUJA.


CHAMA cha  Mapinduzi (CCM) Zanzibar viongozi watakaochaguliwa kupitia Uchaguzi wa ngazi ya Wilaya ya Kaskazini “B” kichama Unguja kuwa mstari wa mbele kukemea vikali vitendo vya makundi na safu za uongozi zenye nia ya kuhatarisha uhai wa CCM katika Wilaya hiyo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Abdalla Juma Mabodi wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo wa kuwachagua  viongozi wa nafasi mbali za ngazi hiyo huko Mahonda katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema  matarajio ya CCM ni kuona viongozi  wanaochaguliwa katika uchaguzi huo wanakuwa na makundi ya kuimarisha chama na sio kukibomoa.
Dk.Mabodi alieleza kwamba msimamo wa CCM ni  kuhakikisha Katiba, kanuni na miongozo inasimamiwa  na kufuatwa ipasavyo ili kupata viongozi na makada wenye uwezo wa kuleta maendeleo yewnye tija ndani ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Aidha amewambia viongozi watakaopata nafasi ya kuchaguliwa kupitia uchaguzi huo wahakikishe wanajenga ngome imara ya kisiasa katika wilaya hiyo sambamba na  kuwashawishi wapinzani waliomo katika Wilaya hiyo kujiunga na CCM kwani ndio chama pekee kinachojali maslahi ya wananchi wote.

Amewasihi makada watakaochaguliwa kuwa viongozi kushirikiana vizuri na makada wenzao ambao hawakupata fursa ya kuchaguliwa kwa lengo la kuendeleza misingi imara ya ukomavu wa kisiasa na Demokrasia  iliyotukuka.


Hata hivyo amewapongeza wanachama hasa makada waliogombea nafasi mbali mbali kwa kutofanya kampeni za fujo, vurugu na kuchafuana hali aliyosema kuwa inaonyesha ishara njema ya kukamilika kwa uchaguzi huo bila kujitokeza mapungufu.

Aidha amesema chama hicho baada ya uchaguzi huo kinakusudia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo  viongozi wa ngazi mbali mbali za chama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk. Mabodi amewataka wananchi  wapuuze kauli zinazotolewa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif za kuwa ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar  jambo ambalo haliwezi kutokea kwani Rais halali wa Zanzibar ni Dk. Ali Mohamed Shein mpaka mwaka 2020.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya , Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano Mkuu wa taifa pamoja na nafasi za Halmashauri kuu ya CCM Wilaya.


                                         MATUKIO KATIKA PICHA

Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Nd. Mulla Othman Zubeir akikabidhi taarifa ya Utekelezaji kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi huko Mahonda katika Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B"  kichama Unguja. 

 Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo Nd. Ramadhani Abdalla Shaaban kionyesha sanduku la kupigia kura kabla ya kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Wilaya hiyo.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kamati Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo akipiga kura katika uchaguzi huo.

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo wakifuatilia kwa kina nasaha zinazotolewa na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi. 

Alhamisi, 5 Oktoba 2017

MATUKIO KATIKA PICHA UCHAGUZI WA CCM NGAZI ZA WILAYA ZANZIBAR ULIOFANYIKA LEO.

Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Mabodi akifungua mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya  Kaskazini “A”  kichama katika uchaguzi wa Wilaya  uliofanyika leo katika ukumbi wa CCM MKoa wa kaskazini Unguja Mahonda

Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa, Dk. Hussein Mwinyi akifungua mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Mjini uliofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Unguja.
 Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kati akipiga kura katika uchaguzi uliofanyika leo huko katika ukumbi wa Skuli ya Dunga.


Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Amani wakifuatilia kwa makini harakati mbali mbali zinazofanyika katika uchaguzi huo huko katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini huko Amani Unguja.

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini wakifuatilia kwa makini harakati mbali mbali zinazofanyika katika uchaguzi huo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Unguja.


CCM ZANZIBAR YAFANYA UCHAGUZI NGAZI ZA WILAYA LEO.

          
CHAMA Chama cha Mapinduzi  (CCM)  leo kimefanya uchaguzi  wa ngazi ya Wilaya katika Mikoa ya Zanzibar ili kupata viongozi watakaoongoza nafasi mbali mbali ndani ya ngazi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.


Katika uchaguzi huo mamia ya wanachama wa chama hicho wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “A” kichama  Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda, amewasihi wajumbe wa mkutano huo kutumia vyema fursa hiyo kwa kuwachagua viongozi makini na wachapa kazi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba uchaguzi huo ni muhimu sana kwa chama hicho kwani viongozi watakaochaguliwa watakuwa na dhamana ya kuzitendea haki nafasi zao kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho.

Alisema katika uchaguzi wa ndani wa CCM unakuwa ni wa wanachama wote hivyo baada ya uchaguzi watakaoshinda na wale ambao kura zao hazitotosha na wakawa hawakuchaguliwa wote wanatakiwa kushirikiana katika harakati mbali mbali za kuleta maendeleo ya chama hicho.

Dk. Mabodi alieleza kuwa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo ndio jeshi la kisiasa litakaloweza kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2020.

Alisema katika kujenga dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya chama hicho kimedhamiria kuondosha vitendo vyote vya rushwa, ufisadi, makundi , safu na usaliti ili kuimarisha misingi ya demokrasia na uhuru kwa kila mwanachama ndani ya CCM.

“ CCM Zanzibar haitoweza kuruhusu vitendo vya rushwa, makundi na usaliti vitokee katika uchaguzi unaoendelea na mara baada ya uchaguzi kwani lengo letu ni kukisafisha chama kiwe na viongozi waadilifu watakaosimamia maslahi ya wananchi kwa uzalendo.”alisisitiza Dk. Mabodi.

Pamoja na hayo aliwataka viongozi watakaochaguliwa kubuni miradi endelevu ya kiuchumi na kichama itakayoimarisha siasa katika masuala ya Itikadi kwa kupata wanachama ambao ni makada wenye uzalendo na imani ya kuitumikia CCM katika mazingira yoyote.

Aidha aliwasisitiza viongozi watakaochaguliwa kuwa waadilifu wakati wa uongozi wao kwa kulinda kwa vitendo hadhi na heshima ya CCM iliyojengwa kisiasa ndani na nje ya chama hicho.

Naye Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa,  Dk.Hussein Mwinyi akifungua mkutano  Mkuu wa CCM Wilaya ya Mjini, alisema ukomavu wa kisiasa ulioonekana katika chaguzi za ngazi za matawi hadi majimbo uliokamilika bila kutokea vurugu ama dalili za rushwa ndio matarajio yanayotegemewa kuonekana katika uchaguzi wa ngazi zilizobaki.

Alisema kwa sasa CCM imeamua kujisahihisha kwa kutorudia makosa yaliyokuwa yakitokea katika chaguzi za ndani ya chama zilizopita hivyo viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo wafuate Katiba na kanuni  za chama cha mapinduzi.

Dk. Mwinyi alisema baada ya uchaguzi huo wanachama wa chama hicho wanatakiwa kuendeleza mshikamano wa kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura pamoja na kuongeza wanachama wapya ili kujiimarisha kisiasa katika uchaguzi mkuu wa dola ujao.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya ,Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano Mkuu wa taifa pamoja na nafasi ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya.