Jumanne, 9 Mei 2017

" ITUMIENI VYEMA FURSA YA UCHAGUZI " WARIDE


KATIBU wa  Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi   CCM Zanzibar,  Waride Bakari  Jabu  amewataka  wanachama  wa  CCM  Tawi la Chukwani  kutumia  vizuri fursa ya Uchaguzi wa Chama kuwachagua  viongozi  na watendaji  waadilifu  na wasioyumbishwa  wakati  wanapotekeleza  majukumu.

Rai hiyo  aliitoa  wakati  akizungumza na  wanachama  na Kamati ya siasa ya  Tawi la Chukwani  katika ziara ya kuimarisha chama huko  katika  Ofisi ya Tawi la Chukwani  nje kidogo ya Mjini wa Zanzibar.

Alisema safu za viongozi  wa ngazi mbali mbali watakaochaguliwa  kupitia uchaguzi huo ndio watakaokuwa na jukumu  la  kuwaidhinisha  viongozi watakaovusha chama hicho salama na kuhakikisha kinashinda kwa ngazi zote  katika uchaguzi mkuu ujao.

Kupitia  kikao  hicho  aliwaagiza  Viongozi  wa  ngazi ya  majimbo  ambao ni  Mbunge, Mwakilishi  na Madiwani  kuhakikisha wanasilisha  kwa  wananchi  wao taarifa  ya utekelezaji  wa Ilani  ya Uchaguzi  ya CCM mwaka 2015/2020 ili  waweze kujua  ahadi zilizotekelezwa  na kuhoji ambazo bado utekelezaji wake.

Alisema   Katiba  ya  Chama hicho  inaagiza  Viongozi  hao   kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Ilani kila baada ya miezi mitatu kwa wananchi  pamoja na ngazi za juu za chama ili waweze kujiridhisha kama ahadi zilizoahidiwa  wakati  wa kampeni kama zimetekelezwa  kwa ufanisi.

Pamoja na agizo hilo pia aliwataka viongozi hao kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili wananchi  ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu na wahusika.

“ Viongozi lazima tuendeleze  utamaduni  wa kuwa karibu zaidi na wananchi wetu kwani ndio waliotuajiri  katika nafasi hizi tulizokuwa nazo na mkataba wetu na wao ni kuwatatulia kero zinazowakabili katika maeneo yao.

Pia naamini mnatekeleza  ilani ya Uchaguzi lakini kama hamrudi kwa wananchi mkawambia  mliyoyafanya wakafahamu  mnatarajia wao watajuaje  kama kuna  ahadi zimetekelezwa katika jimbo husika, lazima tubadilike na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.”, alisema  Waride na kuongeza kwamba msimamo wa CCM ni kujiimarisha kuanzia ngazi za chini wadi na matawi.

Pamoja na hayo alisema njia pakee ya kumaliza baadhi ya  malalamiko  katika Tawi  hilo ni  viongozi na wanachama kutumia njia ya vikao rasmi vya Kikatiba  kujadili changamoto zinazowakabili ili waweze kupata maamuzi ya pamoja ya kutafuta ufumbuzi wake.

Naye  Kaimu  Katibu  wa  Tawi hilo, Iddi Khamis   Akitoa tathmini ya Uchaguzi wa CCM kwa ngazi ya Tawi  na jumuiya alisema  linaendelea vizuri na kwa baadhi ya ngazi tayari fomu zote zimepata  wagombea wa nafasi  za uongozi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo hilo,   Mwanaasha  Khamis Juma alisema toka ameshika nafasi ya uongozi ameshiriki kikamilifu kutatua changamoto za jimbo hilo zikiwemo kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama, kusaidia vikundi vya ujasiria mali kwa wanawake na vijana na kuahidi kuendelea kuzitafutia ufumbuzi hatua kwa hatua kero zingine zilizipo katika jimbo hilo.

Wakizungumza  baadhi ya wanachama  wa  Tawi  hilo waliwapongeza  Mwenyekiti wa CCM Taifa  ambaye pia ni Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa  Tanzania  Dkt. John Pombe  Magufuli  pamoja na Makamo Mwenyekiti  wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi   Dkt. Ali Mohamed  Shein  kwa  usimamizi na utekelezaji mzuri  wa  Ilani ya Chama hicho kwa wanannchi wote.

Pia walilalamikia changamoto  ya uongozi  wa  Tawi  hilo  kutofanya vikao  vya  kikanuni mara kwa mara hali inayosababisha  baadhi ya viongozi wa ngazi za juu  kutotekeleza  wajibu wao ipasavyo.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni