Jumatatu, 1 Mei 2017

DR.MABODI AWATAKA BARAZA LA WAZEE PEMBA KUSIMAMIA MAADILI YA VIJANA.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala” Mabodi” amewasihi Wazee wa Chama hicho kisiwani Pemba kusimamia ipasavyo suala la Maadili kwa vijana ili waishi wakiwa na uzalendo wa kweli wa kukitumikia na kukilinda chama dhidi ya wapinga maendeleo wanaotamani kuking’oa madarakani.

Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumza na Baraza la Wazee wa Chama hicho kisiwani humo wakati akihitimisha ziara yake kisiwani humo huko katika Afisi ya kitengo cha Uratibu wa CCM, Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba .

Alisema Wazee ni hazina kubwa kwa chama na taifa kwa ujumla kutokana na busara na nasaha zao kuwa ni muongozo mwa nyenzo za kuongeza ufanisi wa maendeleo ya chama hicho katika nyanja ya kisiasa na kiuchumi.

Dkt. Mabodi aliwambia Wazee hao kwamba endapo wataweka mkakati maalum wa kukaa na vijana wao kuwaeleza historia ya Zanzibar kabla na baada ya mapinduzi nasaha hizo zitawajengea ukomavu na misimamo imara ya uzalendo juu ya CCM.

Pia alisema maendeleo na fursa mbali mbali za kiuchumi zilizopo nchi kwa sasa zimetokana na utumishi mzuri,uadilifu na uzalendo wa viongozi hao wastaafu katika sekta za chama na serikali hivyo bado wana nafasi kubwa ya kutumia ujuzi wao kushauri na kukosoa baadhi ya mambo wanayoona hayaendani na misingi ya Wana ASP waliofanya Mapinduzi ya 1964.

“Katika Sayansi ya kisiasa  Wataalamu wanaamini kwamba hakuna upinzani unaodumu katika maisha ya Serikali Tawala inayoongoza nchi kwa mfumo wa utawala wa bora, Haki, Utu na Usawa kwa wananchi wote.

 Pia Chama chetu hakina uadui na wapinzani siku zote tumekuwa tukiwasihi watushauri na kutukosoa watakavyo juu ya masuala mbali mbali ya kisera na Ilaya ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/ 2020,  lakini wasiharibu  wala kuchafua amani na utulivu  wa nchi yetu kwani wao jukumu lao ni siasa na sio vurugu na migogoro hayo hatuwezi kuyavumilia”, alieleza  Dkt. Mabodi.

Aidha  alitoa agizo kwa viongozi na watendaji wa Chama hicho kufanya utafti wa kitaalamu kwa baadhi ya majimbo ya Pemba ambayo CCM imekuwa  ikiaminishwa kwamba inashindwa kwa kila uchaguzi, jambo ambalo alidai sio sahihi mpaka apate maelezo ya kitaalamu  ili kuhakikisha majimbo yote  ya Pemba yanarudi mikononi mwa chama hicho 2020.

Naibu Katibu Mkuu huyo alitamka  kuwa maandalizi ya kuandika historia mpya ya kisiasa kisiwani Pemba toka kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, yanaanza sasa kutokana na kuwepo kwa  mamia ya wanachama wa CUF wanaotamani kuhamia CCM wakati wowote baada ya Chama chao kukosa muelekeo wa kisiasa na kutawaliwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.

Alisema kwamba chama hicho kinatambua na kulaani vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa wafuasi wa CCM vinavyosadikiwa kutekelezwa na wapinzani kisiwani humo  ambao wanachochewa na viongozi wao,  lakini  serikali kupitia vyombo vya Dola wamekuwa wakithibiti hali hiyo, huku Chama kikitafuta ufumbuzi wa kudumu katika kuthibiti hali hiyo.

“ Wanachama wetu wanapopigwa kuchomewa nyumba, kung’olewa mazao yao, kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara na kuchomwa ofisi za umma hatusikii viongozi wa CUF wakikemea vitendo hivyo hali ya kuwa wanaofanyiwa sio raia ama hawana haki ya kuishi Pemba kwa Amani”, alisema CCM itaendelea kufanya siasa za kistaarabu  Zanzibar lakini haitovumilia  vitendo  vya uonevu  wakati yenywe ndiyo iliyoweka serikali madarani na kuvisisitiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutafuta ufumbuzi wa tatizo haraka.

Dkt. Mabodi aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, kwa juhudi zao katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wote bila ya ubaguzi kwa zaidi ya asilimia 90.

Alisema Pemba kwa sasa imekuwa na miundombinu yote muhimu ambayo zamani walikuwa wakiifuata nje ya kisiwa hicho lakini kwa sasa imeimarishwa na Serikali inayotokana na CCM kama ilivyoahidi kwa wananchi kuwa itatoa huduma hizo.

Nao Wazee hao walisifu juhudi za Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kasi yake ya utendaji unaolenga kuongeza uimara na nguvu za CCM Zanzibar ambapo wamemtaka awakumbushe baadhi ya viongozi wengine wafuate nyayo zake.

Hata hivyo walimpongeza Dkt. Shein kwa juhudi zake za kuimarisha Sekta ya Afya na miundombinu ya barabara kisiwani Pemba ambayo ni pamoja na uimarishaji wa Hospitali ya Abdalla Mzee inayotoa huduma za kisasa, ambapo wameahidi kuthamini na kulinda huduma hizo.
Ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Kisiwani humo katika Ofisi ya Kitengo cha Uratibu wa CCM Chake Chake Mkoa wa Kusini  Pemba.


Wajumbe wa Baraza hilo pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” wakiomba dua baada ya kumaliza kikao katika Ofisi ya Kitengo cha Uratibu wa CCM Chake Chake Mkoa wa Kusini  Pemba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni