NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” amewataka viongozi wa kisiasa wa chama hicho waliopewa dhamana ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi waanze kujitathimini mapema kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Rai hiyo ameitoa katika hafla ya utekelezaji wa Ilani hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Donge, Nd. Sadifa Juma katika jimbo hilo huko Kaskazini “B” Unguja.
Dkt. Mabodi aliwambia viongozi wa kisiasa waliochaguliwa na wananchi kuanzia ngazi za Madiwani, Wawakilishi, Wabunge na Rais wa Zanzibar kuwa utaratibu wa kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo sambamba na kuimarisha miradi ya huduma za kijamii sio suala la hiari bali ni lazima kwa kila aliyetumia tiketi ya chama hicho kuomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesifu juhudi za baadhi ya viongozi wanaoendelea kutekeleza ahadi walizoahidi kwa wananchi awamu kwa awamu kuanzia ngazi za chini hadi taifa, na kuwataka waliojisahau kurudi Majimboni mwao kutatua kero zinazowakabili wananchi.
“ Njia pekee ya CCM kubaki madarakani ni kutatua kero za wananchi mijini na vijijini bila kujali itikadi za kisiasa na kidini ili jamii endelee kujenga imani na upendo wa kudumu kwa Chama kilichoiweka serikali madarakani”, alisema Dkt. Mabodi.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt. Mabodi alitoa ahadi ya shilingi 300,000 kwa skuli ya maandalizi Mkataleni pamoja na kusaidia ujenzi wa vyoo vya skuli hiyo ili watoto waweze kusoma katika mazingira bora.
Akizungumza Mbunge wa Jimbo hilo, Nd. Sadifa Juma mara baada ya kutoa mabati 400 yenye thamani ya shilingi milioni saba ili kuezekea Hospitali ya Vijibweni, Maskani ya Kitaruni, Maskani ya Karange, vijibweni “B” Maskani, Donge bridge, pamoja na Skuli ya maandalizi ya Mkataleni.
Aidha Nd.Sadifa mbali na kugawa mabati hayo pia alitoa fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 1.5 kwa hospitali ya Vijibweni inayotegemewa na wananchi wa Jimbo hilo na maeneo jirani kwa huduma mbali mbali za afya ili kiweze kufanyiwa matengenezo na kuwa cha kisasa.
Akitoa shukrani zake Daktari dhamana wa Kituo hicho, Bi.Miza Ali Ussi alipongeza juhudi za mbunge huyo na alisema msaada huo umepatikana kwa wakati mwafaka kwani kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto za upungufu wa vifaa tiba na mabati ya kuezekea baadhi ya nyumba za hospitali hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni