Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” amewasihi viongozi na waumini wa dini ya kiislamu kutumia fursa ya Ijitimai kuliombea taifa liendelee kudumu katika hali ya Amani na Utulivu.
Nasaha hizo amezitoa mara baada ya kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Msikiti wa Ijitimai ya Kimataifa huko katika kijiji cha Kidoto Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema mamia ya waumini wa dini ya kiislamu watakaoshiriki katika ijitimai hiyo watakuwa ni sehemu muhimu ya kufanya dua mbali mbali za kuimbea nchini inusurike na maafa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kijamii.
Alieleza kwamba CCM inaunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi za kidini nchini katika kuhubiri amani na mshikamano kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Alisema licha ya Chama hicho kuwa ni taasisi ya kisiasa bado kina jukumu kubwa la kushiriki kikamilifu katika shughuli za kidini zinazoendeshwa na wananchi wa wa itikadi tofauti za kisiasa.
Aidha kwamba Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kitatoa msaada wa kupeleka nguzo za umeme katika nyumba ya wageni pamoja na kununua vifaa vya samani za ofisi ya jumuiya inayosimamia Ijitimai hiyo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Akitoa taarifa juu ya maendeleo ya Ijitimai hiyo, Katibu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Mwalim Hafidh amesema bado wanaendelea kumalizia ujenzi wa msikiti utakaochukua waumini zaidi ya 5100 kwa wakati mmoja.
Alisema bado wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa vifaa vya ujenzi wa mabanda yatakayotumika wakati wa Ijitimai pamoja na ujenzi wa shule , chuo cha madrasa, hospitali na maktaba pamoja na miundombinu mingine nyingine ya kijamii.
Aidha ameupongeza uongozi wa CCM kwa ziara hiyo na kueleza kuwa taasisi nyingi za kisiasa zimekuwa hazishiriki ipasavyo katika masuala ya kidini hali inayosababisha kutokuwepo na ushirikiano mzuri kwa taasisi hizo.
Naye Makamo Mwenyekiti wa Jukumiya Fiysabilillah Tabligh Markaz Zanzibar, Sheikh Wakat Hassan Bakar Alisema lengo la jumuiya hiyo ni kukifanya kijiji hicho kuwa chimbuko la uislamu na ibada.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameambatana na baadhi ya ujumbe kutoka Baraza la Wazee CCM Zanzibar, Uongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Mkoa huo, Vuai Mwinyi Mohamed.
Ijitimai hiyo inatarajiwa kufanyika Mai 19, mwaka huu na kuudhuriwa na wageni kutoka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni