MAMIA ya Wananchi
wameudhuria mazishi ya Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar.Vuai
Ali Vuai, Marehemu Bi.Mwanaisha Hassan Vuai huko Kijijini kwao Bwejuu, Mkoa wa
Kusini Unguja.
Mazishi hayo
yameongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,
aliyeambatana na viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na jamhuri ya muungano Tanzania.
Bi. Mwanaisha amefariki
jana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tasakhtaa iliyopo
Vuga Mjini Zanzibar.
Akizungumza
mara baada ya mazishi hayo, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar, Nd. Vuai
Ali Vuai alisema kifo cha Mama yake mzazi kimeacha pengo kubwa katika familia hiyo kwani marehemu huyo alikuwa akitegemewa na
jamii kutokana na busara zake.
Aidha Vuai amewashukru wananchi mbali mbali
waliojitokeza kumuunga mkono katika mazishi hayo na kuwasihi waendelee kuwa na
umoja wa kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kijamii.
“ Mama yetu tulimpenda sana lakini ndio hivcyo
amefariki sasa kilichobaki kwetu sisi tuliobaki ni kumuombea dua yeye pamoja na
wazee wetu wengine waliofariki kabla yake.”, alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Mbali
na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd pia Mazishi
hayo yameudhuriwa na Viongozi mbali
mbali wakiwemo Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Omar Kinana, Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma
Saadala “ Mabodi”, Kaimu Katibu Mkuu wa
UVCCM Tanzania Shaka Hamdu Shaka, Mkuu
wa Mkoa kusini Unguja Dk.Idrissa
Muslim Hija, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar,
Waride Bakari Jabu.
Viongozi
wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrissa Kitwana
Mustafa, Mnadhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM, Ali Salum Haji pamoja na baadhi ya
Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu
wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Bi.Mwanaisha Hassan Vuai amefariki dunia akiwa
na umri wa miaka 85 ameacha watoto tisa (9) pamoja na wajukuu kadhaa.
Mungu ailaze roho ya
marehemu pahali pema peponi-Amin.