Alhamisi, 1 Machi 2018

CCM ZANZIBAR YATOA AGIZO ZITO KWA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Ikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bi, Catherine Peter Nao akizungumza mara baada ya kuwasili katika studio za Swahiba Fm iliyopo Mbweni Zanzibar.

 Mkurugenzi wa Swahiba Fm, Maalim Kassim Mohamed Kassim(kulia) akizungumza na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao mara baada ya kuwasili katika Kituo cha radio hiyo kwa ajili ya kujitambulisha.

 WAFANYAKAZI wa Swahiba Fm wakiwa katika picha ya pamoja na wageni wao kutoka Afisi Kuu CCM Zanzibar wakiongozwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao.

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao akizungumza mara baada ya kuwasili katika studio za Chuchu FM iliyopo Mlandege Zanzibar.

 MKUU wa Vipindi Chuchu Fm, Mulhat Doria(wa kwanza kulia aliyevaa mtandio wa rangi nyekundu) akizungumza na ujumbe wa ugeni huo kutoka CCM Zanzibar.

 Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Yussuf Khamis Yussuf(wa kwanza kushoto) akizungumza na Katibu  wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao alipofika ofisini kwake Maisara kwa ajili ya kujitambulisha. 
 Mhariri wa Zanzibar leo Juma Khamis (aliyesimama akizungumza mwenye shati la mistari) akiwatambulisha wafanyakazi wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar waliokuwepo katika Chumba cha Habari baada ya kutembelewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao.

 MKUU wa Waandishi wa habari Zanzibar leo Ndugu Mwantanga Ame (kulia) awakionyeshwa machapisho mbali mbali ya Gazeti la Zanzibar leo Toleo la No.5804 la Machi 1, 2018 Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao (kushoto) na Katibu msaidizi wa Idara hiyo Daud Ismail Juma(wa pili kushoto).


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


TASNIA ya Habari ni sekta muhimu inayoziwezesha Serikali mbali mbali Duniani kuimarisha dhana ya Demokrasia kupitia matangazo na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala, miongozo na mipango ya maendeleo ili wananchi wajue uwajibikaji wa serikali yao na kupima uhalisia wa sera zinazotekelezwa kama zinakidhi mahitaji yao.


Maelezo hayo yametolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine Peter Nao katika mwendelezo wa ziara yake katika vyombo Zanzibar, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo Katibu huyo ameagiza viongozi na watendaji wa Chama na Serikali kupanga utaratibu wa   kuzungumza na vyombo vya Habari mara kwa mara  ili waweze kuwaeleza wananchi utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika taasisi zao.


Catherine amesema  kiongozi yeyote mwenye dhamana ya kutoa taarifa za Chama ama Serikali atakayekataa kuzungumza na vyombo vya habari atakuwa anaenda kinyume na falsafa ya CCM mpya na Tanzania mpya inayotaka Chama kirudi mikononi mwa wananchi kwa kuanza na hatua ya kuwapatia taarifa sahihi zinazohusu masuala ya maendeleo.


Amesema kiongozi anayetekeleza wajibu wake vizuri hawezi kuwa na hofu ya kuzungumza na vyombo vya habari, hivyo ni lazima watumishi hao wa umma kukubali mabadiliko ya zama mpya za utandawazi zinazotoa fursa ya wananchi kuhoji na kudadisi viongozi waliowapa dhamana nini wamefakanya katika maeneo yao.


“Serikali ya Mapiunduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imefanya mambo mengi mazuri lakini cha kusikitisha wananchi wengi hawajui serikali yao nini inafanya kutokana na baadhi ya Viongozi wenye dhamana ya kuzungumza wapo kimya”, alisema Catherine.


Agizo hilo limetolewa baada ya Vyombo vya Habari mbali mbali nchini kulalamikia urasimu usikuwa na tija wa baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutotoa ushirikiano kwa taasisi za kihabari hali inayosababisha baadhi ya vyombo hivyo kutoa taarifa za upande mmoja baada ya kukosekana ushirikiano kutoka kwa viongozi wa umma.


Pia amewapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zao za kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM kwa kasi kubwa hatua inayoleta furaha ya kudumu kwa wananchi.


Hata hivyo Katibu huyo amesema  licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji bado CCM inaendelea kubaki katika msimamo wake kwa mujibu wa Ibara ya tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 kwa kuhakikisha mwaka 2020 CCM inashinda katika Uchaguzi wa ngazi zote  na kubaki madarakani.


Ameeleza kuwa  lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa vyombo hivyo ambavyo ni wadau wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya wananchi.


Akizungumza Mkurugenzi wa Swahiba FM Radio, Maalim Kassim Mohamed Kassim alisema Vyombo vya habari vipo kwa ajili ya wananchi hivyo kiongozi yeyote aliyepewa dhamana na wananchi ana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo.


Mkurugenzi huyo amekishauri Chama Cha Mapinduzi kukaa pamoja na viongozi wa Serikali hasa mawaziri na wakurugenzi kuwasihi watoe ushirikiano kwa kituo chake pindi wanapohitajika kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.


Naye Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Yussuf Khamis Yussuf amesema Shirika hilo litaendelea kutoa habari mbali mbali zinazohusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, huku wakizingatia kanuni na miongozi ya maadili ya Tasnia ya habari.


Naye Meneja wa Chuchu Fm Salma Ahmed Alley, amesema pamoja juhudi za taasisi hiyo katika    kuelimisha, kuhabarisha, kukosoa na kuhamasisha amani na utulivu bado wanakabiliwa na  changamoto ya ukosefu wa matangazo ya biashara kutoka Serikalini na taasisi zingine hali inayosababisha baadhi ya wakati chombo hicho kuyumba kifedha.



Pamoja na hayo Salma amesifu juhudi za  Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine kwa ujasiri wake wa kuvithamini vyombo vya habari na kufungua milango ya ushirikiano wa kudumu.

Jumanne, 27 Februari 2018

BI.CATHERINE AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUONGOZA MAPAMBANO YA VITA YA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao akizungumza na viongozi na watendaji wa Zenj Fm Radio katika ziara yake kwenye vyombo vya Habari Zanzibar.

 MENEJA wa Zenj Fm Winifrida Mayao(kushoto) Meneja Mkuu wa Zanzibar Media Corperations Ramadhan Sender(kulia) wakizungumza na wageni kutoka Afisi Kuu CCM Zanzibar wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi.Catherine Peter Nao.

 KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi.Catherine Peter Nao (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Iland Media Group  Bw.Fauz Abdul Razaki (kushoto).
 KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi.Catherine Peter Nao, akiwa katika studio za Zenj Fm.

Mkurugenzi Iland Media Group  Bw.Fauz Abdul Razak (kushoto), akitoa ufafanuzi wa vifaa vya kurushia matangazo ya TV katika Chumba maalum cha kuzalisha vipindi.

 BAADHI ya wafanyakazi wa Coconut Fm Radio wakiwa katika Chumba Cha Habari mara baada ya kuupokea Ugeni kutoka CCM ulioongozwa na Katibu wa Idara ya NEC, Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi.Catherine Peter Nao aliyetembelea Radio hiyo.
 Katibu wa Idara ya NEC, Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi.Catherine Peter Nao akiwa katika Studio za Coconut Fm Radio iliyopo Migombani Mnara wa Mbao Zanzibar.


 Muhariri Mkuu Mtendaji wa Bomba Fm Radio Mwinyi Sadala (wa tatu kulia) akiwakaribisha wageni hao walioongozwa na Katibu  wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao katika mwendelezo wa ziara.

 KATIBU msaidizi Mkuu  Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Daud Ismail Juma akitambulisha maafisa mbali mbali wa CCM waliofustana na Mkuu wa Idara hiyo.

 Katibu  wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao akiwa katika studio za Bomba Fm Radio.
 Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao (kushoto) akizungumza na Bw. Aziz(kulia)  Mkuu wa udhibiti wa fedha wa Bomba FM Radio. 
Katibu  wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao katika mwendelezo wa ziara, akiwa katika Chumba Cha kuzalisha Vipindi vya Iland TV.



 MKUU wa Vipindi  Tifu TV Bw. Mwanjie Saleh Mgeni (kulia wa mwanzo) akitoa ufafanuzi juu wa chumba cha matangazo cha Tifu TV, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi akifuatilia kwa makini maelezo hayo.
 Chumba cha kurushia matangazo cha Tifu TV.
 Meneja Mkuu wa Tifu TV  Bw.Abdalla Kesi Shaaban(kulia) akizungumza na Katibu  wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao akizungumza na viongozi na watendaji wa Zenj Fm Radio katika ziara yake kwenye vyombo vya Habari Zanzibar.



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao amesema Vyombo vya Habari ni taasisi muhimu zinazotakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea na kuibua vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto ili wahalifu wa matukio hayo waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara yake kwenye Vyombo vya Habari nchini, amesema taasisi hizo zenye dhamana ya kuelimisha,kuburudisha,kukosoa na kushauri zina jukumu kubwa la kueleza kwa upana athari mbaya zinazotokana na vitendo hivyo.

Alisema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuishauri serikali na wadau mbali mbali wa haki za binadamu kutekeleza wajibu wao wa kuvisimamia vyombo vya kisheria kuharakisha uendeshaji wa kesi hizo na kutoa hukumu kali kwa watu wanaotiwa hatia kwa makosa hayo.

Pia, alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuondokana na mfumo duni wa upelelezi juu ya kesi za udhalilishaji badala yake waongeze kasi na kutumia weledi na uaminifu kama kanuni na miongozo ya jeshi hilo inavyowaelekeza.

Katibu huyo alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua ikiwemo Baraza la wawakilishi kupitisha mswaada wa sheria mpya ya mwaka 2018, inafuta sheria ya adhabu kwa makosa ya jinai ya mwaka 2004, hivyo baada ya Rais wa Zanzibar kuitia saini na kuwa sheria kamili kinachobaki ni wananchi na wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo.

“ CCM ni taasisi inayojali misingi ya haki za binadamu na utu kwa watu wote bila kujali tofauti za kisiasa, hivyo hawezi kubaki kimya huku nchi yetu inaendelea kuangamia kwa vitendo viovu vya ubakaji kila sehemu, ni muhimu kila mtu kupambana kwa nafasi yake ili tuondoshe janga hili.

Lakini pia taasisi zinazosimamia masuala ya utekelezaji wa Kisheria sasa tunawambia huu ndio muda wa kujitathimini na kufanya kazi vinginevyo Chama Cha Mapinduzi kitachukua hatua kali za kimaadili kwa baadhi ya viongozi wakuu wa Taasisi hizo ambao hawatekelezi wajibu wao kiutendaji”, alisema Bi,Catherine.

Hata hivyo alieleza kuwa Zanzibar haikuwa na utamaduni wa kesi za aina hiyo lakini vitendo hivyo vimeongezeka kutokana na utandawazi unaopelekea baadhi ya wananchi kuacha utamaduni wa asili na kuiga masuala ya kigeni.

Akizungumzia mchango wa vyombo vya Habari katika ukuaji wa Demokrasia, Catherine amesema taasisi hizo za kihabari zimekuwa mstari wa mbele kuandika na kuripoti vipindi, makala na habari mbali mbali za kisiasa zinazochangia ukuaji wa kidemokrasia kwa wananchi.

Alisema Vyombo vya habari  sio tu kutangaza  habari za kisiasa bali hata katika ukuaji wa kiuchumi wa Zanzibar taasisi hizo zimechangia kutangaza  fursa za nchi  katika anga za kimataifa hasa utaliii na zao la karafuu na kusaidia ukuaji wa pato la taifa unaotokana na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Pamoja na hayo alisema lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha,kubadilishana mawazo, kujenga mahusiano  kwa vyombo hivyo ambavyo ni wadau wakubwa wa CCM katika masuala ya kueneza Itikadi na Habari za Chama kwa wananchi.

Ameahidi kuendelea kufanya kazi na ukaribu na vyombo vya Habari mbali mbali na kuvishauri vielekeze nguvu zake sehemu za kijamii hasa za vijijini kuibua kero zinazowakabili wananchi ili taasisi husika zitafute ufumbuzi wa kudumu.

Naye  Meneja wa Radio ya Zenj Fm, Winifrida Mayao amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa busara zake za kuendeleza mahusiano ya kiutendaji na Kituo hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Iland Media Group, Hatwab Mbarouk Khamis ameeleza kuwa ziara hiyo imefungua milango ya kiutendaji baina ya Kituo Chake na CCM.

Akizungumza Muhariri Mkuu Mtendaji wa Bomba Fm Radio, Mwinyi Sadala amesema Kituo hicho kimekuwa ni mdau mkubwa wa kuripoti na kuandika habari za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinazohamasisha dhana ya Utawala bora, Demokrasia, uhuru wa kutoa na kupokea maoni kwa wananchi.

Hata hivyo Sadala alikishauri Chama hicho kuwakumbusha baadhi ya Wabunge, wawakilishi,Madiwani na viongozi wengine wa Serikali ambao bado hawajatekeleza  ahadi walizotoa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, kutumia wakati huu kutekeleza ahadi hizo kwa lengo la kurejesha matumaini ya jamii.

Ziara hiyo imeendelea katika Vyombo vya Habari mbali mbali ikiwemo Zenj Fm, Coconut Fm, Iland TV, Bomba Fm na Tifu TV.