Jumamosi, 21 Desemba 2019

MHE.ASHA AKING'ARISHA KITUO CHA UJASIRIAMALI CHA UWT


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdulla Juma akikabidhi Vifaa vikiwemo vitambaa pamoja na Vyerehani kwa Mwenyekiti  wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Mjini Habiba Nassib Suleiman kwa ajili ya Kituo cha Elimu Amali UWT Wilaya ya Mjini.

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdulla Juma akizungumza na Viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya mjini wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kituo cha elimu amali UWT wilaya ya mjini iliyofanyika katika kituo hicho Mwembe Matumbaku Wilaya ya Mjini unguja.

MWENYEKITI wa UWT Wilaya ya Mjini Ndugu Habiba Nassib Suleiman akimkabidhi zawadi maalum Mbunge wa Viti Maalum  Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdulla Juma katika hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa kituo cha elimu amali UWT wilaya ya mjini iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho mwembe matumbaku wilaya ya mjini unguja.

katibu wa UWT wilaya ya Mjini akizungumza na baadhi ya viongozi na wa jumuiya hiyo wakati wa makabidhiano ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kituo cha elimu amali UWT wilaya ya mjini uliotolewa na mbunge wa viti maalum ccm mkoa wa mjini Asha Abdulla Juma.





MBUNGE wa viti maalum wa Mkoa wa Mjini,Mhe Asha Abdulla Juma amefurahishwa na hatua ya Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi ya wilaya ya Mjini kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi kwa kuhakikisha vijana wanajikwamua kiuchumi.

Amesema kitendo cha UWT kuwakusanya vijana tofauti ndani ya mkoa huo kwa lengo la kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kuondokana na hali ya utegemezi ambapo baadaye wakipata ujuzi wanajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kujiingizia kipato ni moja ya sehemu ya maagizo ya ilani pamoja na viongozi wa chama.

Kauli hiyo ameitoa wakati akikabidhi vifaa vya ushonaji ikiwemo chereheani mbili,meza pamoja na vitambaa vya kutengeneza mapambo katika kituo cha mafunzo ya amali cha UWT wilaya ya mjini ambapo alisema hiyo ni ahadi za CCM katika kuwakusanya vijana na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuondokana na utegemezi.

Amesema baada ya kuona Jumuiya hiyo imeanzisha kituo hicho cha mafunzo kwa ajili ya vijana akaiona aunge mkono juhudi hizo za kuhakikisha vijana hao wanaokombolewa dhidi ya ukosefu wa ajira ili kuongeza uzalishaji nchini kama maagizo ya viongozi wa CCM wanavyoelekeza.

"Nina amini chuo hichi kitasaidia sana juhudi hizi kwa vijana wetu na ndio maana nikaona nilete nguvu kwenye kituo hichi cha UWT hasa kwa wakina mama katika kujifunza ujasiriamali wa ushonaji,upishi na mambo mengine,"ameeleza

Naye Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mjini,Habiba Nassir Suleiman amesema lengo la uongozi wa wilaya hiyo ni kuendelea  kubuni miradi itakayosaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira na ongezeko la uzalishaji kwa lengo la kukuza uchumi kama inavyoelekeza CCM.

Amesema uongozi wa UWT wilaya imeamua kufanya ubunifu wa aina hiyo wa kuwakusanya vijana na kuwapatia mafunzo ya ujuzi wa shughuli za ujasiriamali ambapo kwa namna moja ama nyingine itawasaidia sana wanawake katika kuondokana na hali ya utegemezi na kuweza kujikwamua kiuchumi.








Ijumaa, 20 Desemba 2019

BI.CATHERINE- AWAWEKA KIKAANGONI ACT-WAZALENDO.

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar Bi.Catherine Peter Nao,akizungumza na Vyombo vya Habari leo Tarehe 20/12/2019.



CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimekitaka Chama cha ACT-Wazalendo kuacha siasa za maji taka na kishamba zilizopitwa na wakati zinazolenga kuhatarisha amani ya nchi.  

Kimesema Viongozi wa ACT-Wazalendo wameendelea na mikakati michafu ya kutafuta umaarufu na huruma ya kisiasa kupitia matamshi yenye uchochezi,kashifa,dharau na upotoshaji dhidi ya Viongozi wa Serikali na CCM.

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao, amesema CCM haitovumilia mwenendo wa siasa za maji taka za kuwatukana na kuwadhalilisha Viongozi wa Serikali na Chama hicho zinazofanywa na ACT-Wazalendo.

Catherine, ameendelea kuvitaka Vyombo vya Dola nchini kuchukua hatua za haraka dhidi ya wanasiasa hao wachochezi wanaotumia vibaya uhuru wa kisiasa kwa kuwadhalilisha viongozi wa umma.

"Siku za hivi karibuni tumeona namna viongozi ACT-Wazalendo walivyomtukana Naibu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Mhandisi Hamad Yussuf Masauni mitandaoni na Jeshi la Polisi lipo na halijachukua hatua stahiki.

Wenzetu hao baada ya kushindana kwa hoja na kufanya kazi za Wananchi wao wanakuja na mtindo wa matusi sasa tunawaonya na wasipoacha tabia hiyo wajue ushahidi wa maovu yao tunao na tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria.", amesema Catherine Peter nao.

Kupitia mkutano huo Catherine alilaani hatua ya upotoshwaji unaofanywa na chama cha ACT-Wazalendo kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajia kuanza uandikishwaji visiwani hapa Januari 18  hadi Machi 4 mwaka 2020.

Amesema mchakato wa uandikishaji wa daftari hilo upo kikatiba na kidemokrasia hivyo usichafuliwe kwa hoja dhaifu na wanasiasa  wanaoweka mbele maslahi yao  badala ya maslahi ya nchi.

Ameongeza kuwa mshakato huo ndio chimbuko la uwepo wa uchaguzi mkuu ujao hivyo panahitajika ustaarabu kwa vyama vyote vya kisiasa nchini.

Katibu huyo Catherine amesema kinachofanywa na ACT-Wazalendo ni kuwajengea hofu wananchi kwa lengo la kukwamisha ukamilishaji wa uandikishwaji wa daftari la wapiga kura ambapo jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria.

"Tunahitaji siasa za kistarabu pamoja na mchakato huu ambao unaanza wa uandikishwaji wa daftari hilo la wapiga kura hivi karibuni ufanyike kistaarabu na hakuna sababu ya kuwepo kwa hali ya uvunjifu waamani,"amesema.

Catherine amesema CCM haifanyi kazi ya uandaaji wa vitambulisho bali inafanya kazi za siasa na kwamba katika Ofisi ya Chama hakuna kitu kama hicho ambacho ACT-Wazalendo wanadai shutuma hizo.

Katika maelezo yake Katibu huyo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kuchukua vitambulisho vyao vya Mzanzibar Mkaazi pamoja na kujiandisha katika daftari la wapiga pindi wakati utakapofika.  

Jana Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Abdallah Bimani alishutumu kuwa CCM imeandaa njama za kuwaandikisha vijana ambao hawajatimia umri wa kupiga kura lengo likiwa kuongeza idadi ya kura kwa Chama, madi ambayo ni uongo na yanatakiwa kupuuzwa na Wananchi wote.