Ijumaa, 20 Desemba 2019

BI.CATHERINE- AWAWEKA KIKAANGONI ACT-WAZALENDO.

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar Bi.Catherine Peter Nao,akizungumza na Vyombo vya Habari leo Tarehe 20/12/2019.CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimekitaka Chama cha ACT-Wazalendo kuacha siasa za maji taka na kishamba zilizopitwa na wakati zinazolenga kuhatarisha amani ya nchi.  

Kimesema Viongozi wa ACT-Wazalendo wameendelea na mikakati michafu ya kutafuta umaarufu na huruma ya kisiasa kupitia matamshi yenye uchochezi,kashifa,dharau na upotoshaji dhidi ya Viongozi wa Serikali na CCM.

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao, amesema CCM haitovumilia mwenendo wa siasa za maji taka za kuwatukana na kuwadhalilisha Viongozi wa Serikali na Chama hicho zinazofanywa na ACT-Wazalendo.

Catherine, ameendelea kuvitaka Vyombo vya Dola nchini kuchukua hatua za haraka dhidi ya wanasiasa hao wachochezi wanaotumia vibaya uhuru wa kisiasa kwa kuwadhalilisha viongozi wa umma.

"Siku za hivi karibuni tumeona namna viongozi ACT-Wazalendo walivyomtukana Naibu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Mhandisi Hamad Yussuf Masauni mitandaoni na Jeshi la Polisi lipo na halijachukua hatua stahiki.

Wenzetu hao baada ya kushindana kwa hoja na kufanya kazi za Wananchi wao wanakuja na mtindo wa matusi sasa tunawaonya na wasipoacha tabia hiyo wajue ushahidi wa maovu yao tunao na tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria.", amesema Catherine Peter nao.

Kupitia mkutano huo Catherine alilaani hatua ya upotoshwaji unaofanywa na chama cha ACT-Wazalendo kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajia kuanza uandikishwaji visiwani hapa Januari 18  hadi Machi 4 mwaka 2020.

Amesema mchakato wa uandikishaji wa daftari hilo upo kikatiba na kidemokrasia hivyo usichafuliwe kwa hoja dhaifu na wanasiasa  wanaoweka mbele maslahi yao  badala ya maslahi ya nchi.

Ameongeza kuwa mshakato huo ndio chimbuko la uwepo wa uchaguzi mkuu ujao hivyo panahitajika ustaarabu kwa vyama vyote vya kisiasa nchini.

Katibu huyo Catherine amesema kinachofanywa na ACT-Wazalendo ni kuwajengea hofu wananchi kwa lengo la kukwamisha ukamilishaji wa uandikishwaji wa daftari la wapiga kura ambapo jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria.

"Tunahitaji siasa za kistarabu pamoja na mchakato huu ambao unaanza wa uandikishwaji wa daftari hilo la wapiga kura hivi karibuni ufanyike kistaarabu na hakuna sababu ya kuwepo kwa hali ya uvunjifu waamani,"amesema.

Catherine amesema CCM haifanyi kazi ya uandaaji wa vitambulisho bali inafanya kazi za siasa na kwamba katika Ofisi ya Chama hakuna kitu kama hicho ambacho ACT-Wazalendo wanadai shutuma hizo.

Katika maelezo yake Katibu huyo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kuchukua vitambulisho vyao vya Mzanzibar Mkaazi pamoja na kujiandisha katika daftari la wapiga pindi wakati utakapofika.  

Jana Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Abdallah Bimani alishutumu kuwa CCM imeandaa njama za kuwaandikisha vijana ambao hawajatimia umri wa kupiga kura lengo likiwa kuongeza idadi ya kura kwa Chama, madi ambayo ni uongo na yanatakiwa kupuuzwa na Wananchi wote.
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni