Ijumaa, 22 Februari 2019

WANANCHI WASEMA DK.SHEIN NI SHUJAA WA MAENDELEO


BARABARA ya Mkanyageni-Kangani  Wilaya ya Mkoani Pemba.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

BAADHI ya Wananchi wa Wilaya ya Mkoani Pemba wamepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundo mbinu ya Barabara ndani ya Wilaya hiyo.

Wameeleza kuwa Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk.Shein, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo sugu yaliyowathiri wananchi wa wilaya hiyo kwa miaka mingi kabla na baada ya  Mapinduzi ya mwaka 1964.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi hao, mara baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kuweka Jiwe la Msingi katika Barabara ya Mkanyageni -Kangani (KM5), wamesema barabara hiyo itakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo jirani.

Mkaazi wa Kijiji cha Mkanyageni Juma Faki Hamad(45), amesema barabara ni moja ya kichocheo cha maendeleo kwa wananchi waoishi vijijini kwani wanapata kusafirisha mazao na bidhaa mbali mbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Naye Mkaazi wa Kijiji cha Mkanyageni Fatma Masoud Kombo( 50) amempongeza Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake za kutengeneza barabara hiyo itakayokuwa mkombozi kwa Akina mama wajawazito kufika kwa wakati katika Vituo vya Afya.

Katika maelezo yake Bi.Fatma amemtaja Dk.Shein kuwa ni shujaa wa maendeleo anayeasisi maendeleo ya kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameeleza kwamba Dk.Shein amekuwa ni kiongozi muadilifu anayejali maisha ya wananchi wa kipato cha chini kwa sasa amewafanya wamekuwa na hadhi kutokana na kuimarika kwa huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Naye Zuwena Hiji Kombo(65), amesema mtu yeyote anashindwa kushukru na kuthamini huduma za kimaendeleo zinazotekelezwa na Serikali, mtu huyo atakuwa hana uzalendo na hastahiki kuishi katika jamii ya watu wanaopenda maendeleo ya Zanzibar.

Said Nassor Mjaja(39), amewataka wananchi wa Wilaya ya Mkoani kuendeleza utamaduni wa ustarabu na kuachana na siasa zilizopitwa na wakati za kuharibu miundombinu mbali mbali inayotekelezwa na Serikali kwani wanaonufaika ni wananchi wote.

VISIWA VIDOGO VIDOGO PEMBA NA UNGUJA KUPATA VIVUKO VYA KISASA.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Mkoani na Chama Cha Mapinduzi katika Majumuisho ya ziara yake huko Skuli ya Sekondari ya Mohamed Juma Pindua.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akitoa salamu za CCM katika majumuisho hayo.


KATIBU wa CCM Wilaya ya Mkoani Mohamed Ali Abdalla akisoma taarifa ya CCM katika majumuisho hayo.

BAADHI ya Viongozi mbali mbali wa CCM wakiwa katika majumuisho hayo.

BAADHI ya Maziri wa SMZ wakiwa katika majumuisho ya ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein katika Wilaya ya Mkoani Pemba.

WAZEE wa Chama Cha Mapinduzi Pemba wakiwa katika majumuisho.


 NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzbar Dk.Ali Mohamed Shein,a mesema serikali inaendelea na juhudi za kutafuta vivuko vya kisasa vyenye uwezo wa kuwavusha kwa usalama wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo Pemba na Unguja.

Amesema mipango hiyo inaendelea kwa umakini Zaidi wa kupata vivuko hivyo vilivyokuwa katika viwango vya kimataifa ili wananchi wa visiwa vyote wawe na uhakika wa usafiri wa baharini.

Ameeleza kuwa mkakati huo unaenda sambamba na uimarishaji wa ulinzi wa maeneo yote ya Bahari, kikosi  cha KMKM kwa lengo la kudhibiti uhalifu na magendo katika maeneo ya bahari.

Dk.Shein ameeleza kwamba fursa hizo zinatokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayoangazia kumaliza changamoto zote zinazowakabili wananchi ili kujenga taifa imara lililoendelea kiuchumi na kijamii.

Amefafanua kwamba CCM imekuwa ni taasisi yenye viongozi waadilifu wanaoahidi na wakatekeleza kwa vitendo masuala mbali mbali yayosaidia jamii bila ya kuwabagua watu kidini na kikabila.

Ameeleza kwamba kabla ya mwaka 2020 Zanzibar itakuwa ni miongoni mwa Nchi ya Visiwa yenye maendeleo ya kupigiwa mfano katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisiasa na kimaendeleo.

Amewambia baadhi ya Viongozi na watendaji wa Serikali kuwa asiyeweza kutekeleza Ilani ya CCM huyo atakuwa hatoshi kuwa kiongozi hivyo ni bora akajiondoa mapema katika nafasi anayoitumikia.

Ameeleza kwamba kwa sasa Chama kinahitaji viongozi wabunifu na wachapakazi ili kwenda sambamba na Sera imara za kukuza uchumi wa Nchi.
Alisoma taarifa ya utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya CCM katika Wilaya hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Mkoani Mohamed Ali Abdallah, amesema kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, umekuwa ni kivutio kikubwa cha wanachama wengi wa upinzani kisiwani Pemba wakiwemo vigogo kujiunga na CCM.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Mhe,Issa Juma Ali,akisoma taarifa ya Wilaya hiyo ameeleza kuwa Serikali imetekeleza kwa ufanisi masuala mbali mbali yakiwemo kuimarisha Sekta za Afya, Elimu, Kilimo,Uvuvi, Mazingira na miundombinu ya Majini na Nchi Kavu.

Akitoa salamu za CCM Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Abdulla Juma Mabodi ameeleza Chama kinaridhishwa na kasi ya kiutendaji kwa upande wa Serikali na Chama kwa ujumla.

Amesema kazi iliyobaki kwa sasa ni kila mwanachama kujipanga vizuri katika kuhakikisha CCM inashinda katika majimbo yote yaliyomo katika Wilaya hiyo.