Jumamosi, 3 Machi 2018

KATIBU MPYA WA IDARA YA SUK CCM Z'BAR AKABIDHIWA OFISI


 KATIBU mpya wa Idara hiyo Ndugu Kombo Hassan Juma akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi ya Idara ya Siasa na uhusiano wa Kimataifa (SUK) CCM Zanzibar.

 KATIBU mstaafu wa Idara hiyo  Eng. Hamad Yussuf Masauni(kushoto)  akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Katibu mpya wa Idara hiyo Ndugu Kombo Hassan Juma(kulia aliyekaa).

 MKUU wa Sehemu Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar, Khamis Haji Khamis(kulia) akitoa ufafanuzi juu ya majukumu mbali mbali ya Idara katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa Katibu mstaafu wa Idara hiyo Hamad Yussuf Masauni na kumkabidhi Katibu mpya Maalim Kombo Hassan Juma.
 BAADHI ya Maafisa wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa(SUK) CCM Zanzibar. 
 Afisa wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa(SUK) CCM Zanzibar  Ndugu Mzee Khatib Abdallah akifuatilia kwa makabidhiano hayo.



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar, Ndugu Kombo Hassan Juma amesema ushindani wa kisiasa na mbinu za upinzani zinazidi kuongezeka hivyo Chama tawala ni lazima kiwe imara kukabiliana na mabadiliko yanayotokea katika uwanja wa kisiasa nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Idara hiyo yaliyofanyika katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amesema wanachama, viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi wanatakiwa kubadilika na kuondokana na mazoea ya siasa za wakati  wa  mfumo wa chama kimoja na  badala yake waendane na siasa za ushindani.

Ameeleza kuwa ni lazima CCM iendelee kujifunza baadhi ya mbinu na mikakati ya kisiasa iliyopo katika vyama vingine vya kisiasa ili Chama kiweze kukabiliana na sera za vyama vyenye lengo la kukikondosha madarakani.

Katibu huyo mpya wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ndugu Kombo alisema kazi kubwa ya CCM ni kusimamia viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali waliopewa dhamana ya uongozi na wananchi wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa ufanisi.

“ Tutaendelea kuikumbusha serikali mara kwa mara waendelee na kasi hiyo hiyo ya utekelezaji wa Ilani kwani ndio sehemu pekee ya mtaji wetu kisiasa ambao tunaamini ipo siku wananchi watahoji nini tumetekeleza katika maeneo yao”, amesema Ndugu Kombo.

Aidha Ngugu Kombo amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kumuamini kwa kumteuwa awe Mkuu wa Idara hiyo na kuongeza kuwa atafanya kazi kwa bidii ili CCM ishinde na kubaki madarakani katika uchaguzi Mkuu ujao.

Naye Katibu Mstaafu wa Idara hiyo Eng. Hamad Yussuf Masauni amesema ana imani kuwa idara hiyo ameikabidhi mikononi mwa Kiongozi makini mwenye uzoefu na weledi mkubwa ndani ya CCM na Serikali  kwa ujumla.

Amesema Idara hiyo ndio moyo wa Chama kwani ina dhamana ya kufuatilia hali ya kisiasa nchini pamoja na kuendeleza mahusiano mazuri na taasisi na wadau mbali mbali wa Kimataifa ili kukuza urafiki na ustawi wa kijamii baina ya Chama na taasisi hizo.

Hata hivyo amewasihi watendaji wa SUK Chama na Jumuiya kwa ujumla kumpa ushirikiano Katibu mpya ili kuimarisha shughuli za kisiasa na kiuchumi ndani na nje ya CCM.

Mapema Mkuu wa Sehemu katika Idara hiyo Ndugu Khamis Haji Khamis amesema makabidhiano hayo ni fursa kwa watendaji hao kutumia ujuzi na uzoefu wao katika kubuni mipango mbali mbali ya kiutendaji itakayoleta maendeleo ndani ya CCM.

Hafla hiyo imekuja mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kuteuwa Wakuu wa Idara mbali mbali za Chama  ikiwemo Idara ya Siasa na uhusiano wa Kimataifa Zanzibar(SUK) ili waongoze idara hizo kwa miaka mitano ijayo.



DK.MABODI-AWATAKA WANANCHI KUJIUNGA NA VIKUNDI VYA UJASIRIA MALI

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akihutubia katika hafla ya maonyesho ya  wajasiriamali iliyofanyika huko Fuoni Skuli Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dk.Mabodi awataka wajasiri wa Jimbo la Dimani kujinga na wajasiriamali kutoka sehemu mbali mbali za Dunia ili wapate ujuzi wa kutengeneza bidhaa bora zinazokubalika katika masoko ya biashara ya ndani na nje ya nchi.

Wito huo ameutoa leo wakati akizungumza na wajasiria mali hao huko Viwanja vya Skuli ya Fuoni  Unguja, amesema endapo wajasiriamali hao watatengeneza bidhaa bora watakuwa wamefungua fursa ya bidhaa zao kuongezeka thamani na kukunuliwa kwa wingi.


Amesema njia pekee ya kuongeza ubunifu katika utengenezaji wa bidhaa hizo kwa wajasiriamali hao ni kujifunza ubunifu kutoka kwa wenzao wenye uzoefu mkubwa wa utengenezaji wa bidhaa hizo kwa lengo la kujiongeza kibiashara na kuingiza kipato cha uhakika.

"Nimefurahi sana kuona baadhi ya bidhaa zetu za ndani zinawekwa katika vifungashio kwa kisasa na zinakuwa na muonekano mzuri ambao ni moja ya kivutio kikubwa katika masoko ya kimataifa",amewapongeza Wajasiriamali hao Dk.Mabodi.

Ameeleza kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo katika nchi zilizostawi kiuchumi bila kutaja mchango wa Sekta ya ujasiriamali inayoingiza fedha nyingi kutoka katika mzunguko wa biashara na masoko.

Pamoja na hayo aliwambia wananchi kupitia hafla hiyo kuwa fursa hizo zinatokana na usimamizi mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayotekelezwa na Serikali zote mbili ya  Jamhuri ya Muungano inaongozwa na Dkt. Magufuli  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inaongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein .

 Amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira ya kuendelea kuimarisha ustawi wa vijana kwa kuwapatia mafunzo mbali mbali ya stadi za maisha ili wawe na ujuzi utakaowawezesha kujiajili wenyewe.

Pia ametoa wito kwa wananchi mbali mbali kuvisajili vikundi vyao kupitia utaratibu unaotambuliwa kisheria ili wanufaike  na huduma ya  mikopo yenye masharti nafuu  kupitia mfuko wa uwezeshaji.

Dk. Mabodi akisalimiana na Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali mara tu baada ya kuwasili katika Viwanja vya Skuli ya Msingi Fuoni kwa lengo la kukutana na wajasiriamali wa Jimbo la Dimani

Mbunge wa Dimani Ndg, Juma Ali Juma akimuonesha Dk. Mabodi moja ya bidhaa ambazo zinafanywa na
 wajasiriamali  wa Jimbo la Dimani

Dk. Mabodi akipata malezo kutoka kwa mmoja kati ya wakufunzi Ndg, Fuadi

Naibu akizidi kukagua bidhaa za wajasiriamali hao

Dk. Mabodi akipokea zawadi aliyotunukiwa na wajasiri amali hao kutoka Dimani

Dk. Mabodi akitizama kwa bashasha moja kati ya zawadi aliyotunukiwa na wajasiri amali hao kutoka Dimani

Dk. Mabodi akisalimiana na mmoja kati ya washirika wa maendeleo kutoka Canada

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akiwa katika picha ya pamoja na Wasiriamali na viongozi mbali mbali wa CCM Wilaya ya Dimani.