Ijumaa, 24 Machi 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

     
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, leo amekiongoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa..

Akizungumza na vyombo vya habari  Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM wa Idara ya Itikadi na Uenezi Mama Waride Bakari Jabu, amesema kikao hicho cha siku moja kilifanyika Afisi Kuu ya CCM, Mjini Unguja.

Amesema pamoja na mambo mengine, kikao kilipokea na kujadili majina ya wana CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya Chama chao, ili waweze kuwania nafasi ya Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kwa kipindi cha mwaka 2017 - 2022.

Kikao hicho kimefanyika kwa kuzingatia Ibara ya 114 (7) (b) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la  2012, ambayo inatoa Mamlaka kwa Kamati Maalum ya H/Kuu yaTaifa ya CCM Zanzibar, kupokea na kujadili na hatimaye kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu, kwa hatua zinazofuatia.

Amesema jumla ya wana CCM 33, wakiwemo wanawake 7 na wanaume 26, kutoka Mikoa mbali mbali ya Unguja na Pemba, wamejitokeza kuomba  waruhusiwe na CCM kugombea nafasi hizo.

Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi amefafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania inapaswa kuwakilishwa na Wabunge  tisa (9).

Aidha kikao hicho kilimtambulisha Ndugu. Abdullah Juma Saadalla (Mabodi) aliyepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM hapo Machi 13, mwaka huu, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar. Aidha, kimeahidi kumpa kila aina ya mashirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake aliyopewa na Chama  ipasavyo.

Kikao pia kimewapongeza kwa dhati wana CCM hasa Vijana  waliojitokeza kuomba kugombea nafasi hizo muhimu za Uongozi katika  Jumuiya ya Afrika Mashariki hali inayoonyesha kuimarika kwa Demokrasia ndani ya Chama hicho.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
                                            

Waride Bakari Jabu),
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.

24/03/2016.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni