Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdallah Juma Abdallah amewaahidi Viongozi, Watendaji, wanaCCM na wananchi kwa ujumla kuwa atasimamia kwa vitendo maendeleo, amani na mshikamano ndani na nje ya chama hicho.
Ahadi hiyo ameitoa wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa chama na jumuiya zake mara baada ya kuwasili visiwani humu akitoka Dodoma ambapo aliteuliwa kushikilia nafasi hiyo, ambayo awali ilikuwa chini ya Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Vuai Ali Vuai.
Dkt. Juma alisema kuwa CCM Zanzibar itaendelea kuimarika endapo wanachama na viongozi wa Taasisi hiyo ya kisiasa watazifanyia kazi kwa vitendo falsafa za maendeleo na umoja kwa wote.
" Nimekabidhiwa kijiti hiki ili niweze kuendeleza na kusimamia maslahi ya CCM Visiwani Zanzibar ambayo mtangulizi wangu Nd. Vuai Ali Vuai na wengine waliopita kabla yake wamefanya kazi kubwa ya kusimamia bila ya woga misingi ya maendeleo ndani ya chama chetu, nami nitafuata nyayo hizo na kuongezea mikakati mingine itakayosaidia kuongeza ufanisi.", alisema Dkt. Juma maarufu Mabodi huku akimsifu Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Vuai Ali Vuai kwa utendaji na ukomavu wa kisiasa uliomjengea heshima na uaminifu mkubwa ndani na nje ya chama hicho.
Akitaja baadhi ya vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuishauri na kuisimamia serikali iliyopo madarakani chini ya CCM, kuhakikisha inatatua changamoto sugu zinazowakabili wananchi kwa baadhi ya mitaa na maeneo ya pembe zoni.
Alisema katika juhudi za kupunguza changamoto za ajira nchini serikali imeweza kutekeleza mpango wa awamu ya tatu wa kuimarisha uchumi wa nchini kwa kufungua milango ya wawekezaji kujenga viwanda ili vitoe ajira kwa wazalendo.
Pia alieleza kwamba mbali na mikakati hiyo bado serikali ina mipango endelevu ya kuanzisha viwanda huru vya usindikaji wa samaki, kilimo cha kisasa na kuimarisha miundombinu ya ndani.
Akitaja mikakati ya kuimarisha utendaji wa chama hicho kuanzia ngazi za chini alisema atahakikisha kila tawi na maskani za CCM zinawekewa masanduku ya maoni ili wanachama waweze kutoa maoni yao na makatibu wa ofisi hizo wayawasilishe kwa ngazi husika ili yafanyiwe kazi na ngazi husika.
Aliweka wazi msimamo wake kuwa yeye sio muumini wa makundi ya kugawa na kuharibu CCM , bali ni mtu anayependa kujumuika na watu wenye fikra na mitizamo ya kimaendeleo na kiutendaji.
" Naomba nisije kueleweka vibaya kwa hilo kwani itafikia wakati nitaikosoa serikali kwa baadhi ya mambo ambayo naona hayaendi sawa kwa wananchi ili yaweze kutekelezwa kwa haraka, japo najua kuna baadhi yetu watasema nimekuwa mpinzani lakini ukweli ni kuwa natengeneza heshima ya Chama na serikali iliyopo madarakani.", alifafanua Naibu Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo aliwakumbusha baadhi ya viongozi watakaopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Chama unaotarajiwa kuanza hivi karibuni ili kuhakikisha kila mwanachama mwenye sifa na nia ya kugombea au kupiga kura anapata haki hizo kidemokrasia.
Mapema Naibu Katibu Mkuu mstaafu, Nd. Vuai Ali Vuai akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo mpya Dkt. Abdallah Juma, aliwashukru wafuasi wa CCM, viongozi na watumishi wa chama na jumuiya zote kwa ushirikiano wao pindi alipokuwa katika utumishi wa taasisi hiyo.
Aliwataka ushirikiano huo uendelezwe kwa Naibu katibu Mkuu mpya ili kuimarisha maendeleo ya kisiasa na kiuchumi ndani ya chama.
" Nimekitumikia chama hiki zaidi ya miaka 36 hivyo nimejifunza mengi na kupambana na changamoto mbali mbali lakini hakuna siku niliyorudi nyuma bali nilisonga mbele bila ya kujali ni nani anayenikwaza na nikaishi kwa imani moja ya kulinda maslahi ya CCM popote.
Pia kustaafu kwangu ni jambo la kawaida ndani ya CCM kwani wamepita viongozi wengi kwa kupokezana madaraka, na huo ndio ukomavu wa kisiasa na uimara wa Demokrasia uliopo ndani ya chama chetu, kwani hakuna kiongozi wa kudumu madarakani.", alisema Vuai Ali Vuai.
Kuteuliwa kwa Naibu Katibu Mkuu mpya wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdallah Juma kunatokana na maamuzi yaliyofanyika katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama uliofanyika Dodoma hivi karibu pamoja na mambo mengine ulifanya marekebisho katiba ya CCM ya mwaka 1977.
Dkt. Mabodi kitaaluma ni Daktari Bingwa wa masuala ya upasuaji na utafti wa maiti, ambaye amewahi kuhudumu nafasi mbali mbali zikiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazi mmoja, Mwanzilishi wa Chuo cha madaktari wa Cuba Zanzibar pamoja na nafasi mbali mbali zinazoendana na taaluma hiyo.
Taaluma nyingine ni mtaalamu wa masuala ya Mikakati ya maendeleo Kimataifa, nafasi iliyowahi kumpatia fursa ya unaibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wa siasa ni miongozi mwa vijana wa mwanzo wa CCM toka enzi za Youth legue ambayo kwa sasa ni UVCCM na amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Rahaleo kabla ya majimbo hayo kukatwa upya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni