Alhamisi, 23 Machi 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kesho (24/03/2017) anatarajia kukiongoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya CCM Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi Mhe. Waride Bakari Jabu, amesema kikao hicho maalum cha siku moja kitafanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Amesema kwa kuwa kikao hicho ni maalum, kitakuwa na agenda moja tu, ambayo ni kupokea na kujadili majina ya wana CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Kwa mnasaba huo, Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar amewataka Wajumbe wote wa kikao hicho kuwa wameshakaa kwenye viti vyao ifikapo saa 3:30 barabara za asubuhi.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, iliyokutana leo (23/03/2017) chini ya Mwenyekiti wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Abdullah Juma Abdullah (Mabodi) kwa ajili ya kuandaa ajenda ya kikao hicho.


KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

(Waride Bakari Jabu),
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi,
ZANZIBAR.

23/03/2017.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni