Jumamosi, 14 Aprili 2018

CCM WILAYA YA DIMANI WATEMBELEA MAENEO YA KIHISTORIA

 VIONGOZI wa ngazi mbali mbali za Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya Dimani wakiwa katika eneo alilouawa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume hapo Kisiwandui Zanzibar,  ikiwa ni sehemu ya mafunzo yao ya vitendo  katika madarasa ya Itikadi ya Wilaya hiyo.
  VIONGOZI wa ngazi mbali mbali za Chama Cha Mapinduzi(CCM)Wilaya Dimani, wakielekea katika kaburi la Mzee Abeid Aman Karume lililopo Kisiwandui Zanzibar.

  VIONGOZI wa ngazi mbali mbali za Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya Diman, wakisoma Dua katika kaburi la Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Aman Karume.


WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kuendeleza harakati za kulinda, kutetea na kusimamia misingi ya taasisi hiyo ili kuenzi kwa vitendo juhudi za waasisi wa ASP na TANU.

Hayo ameyasema Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Dimani Hassan Suleiman  Jaku katika ziara ya watendaji na viongozi mbali mbali wa Wilaya hiyo walipotembelea  maeneo ya historia ya kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman Karume,  Kisiwandu Unguja.

Amesema nguvu za Chama Cha Mapinduzi zinatokana na wanachama wazalendo wanaolinda na kuthamini urithi wa Chama hicho toka enzi za vyama vya ASP na TANU.

Katibu huyo Mwenezi amesema lengo la ziara hiyo ni kuwajengea uwezo watendaji wa Chama hasa wenye dhamana ya masuala ya itikadi na uenezi wajue uhalisia wa historia ya nchni ili nao wawafundishe wanachama wengine.

 Amesema viongozi hao wamepewa darasa la itikadi na kujifunza mambo mbali mbali darasani na kwa sasa wamefikia hatua ya kujifunza kwa vitendo na kwenda katika maeneo mbali mbali ya kihistoria na kujionea wenyewe maeneo hayo.

Ameeleza kuwa mambo mema yaliyoasisiwa na marehemu Karume na Wana Mapinduzi wenzake ni urithi wa kudumu unaotakiwa kuthaminiwa na kila mwananchi.

Pia ameeleza kuwa moja ya mbinu ya kushinda mbinu chafu za wapinga maendeleo ni kuhakikisha CCM inashinda na kuendelea kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao.

 “ Tusomeni historia ili tuwe na ujasiri wa kulinda neema hizi tulizorithiwa na wazee wetu na baadae vizazi vyetu viweze kujifunza mambo mema kukoka kwetu na kupigania nchi yao ibaki katika mikono ya Serikali ya CCM.”, amesema Hassan.

Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Dimani, Abdallah Maulid amesema viongozi, wanachama na watendaji kwa ujumla wanatakiwa kujifunza historia halisi ya Zanzibar kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upotoshwaji zinazosambazwa na wapinzani.

Amesema vijana wa CCM wanatakiwa kujiunga na madarasa ya Itikadi  kwa lengo la kujifunza masuala mbali mbali ya historia, Demokrasia na mwenendo wa siasa za visiwa vya Zanzibar.

Katika ziara hiyo wametembelea eneo alilouwawa marehemu Abeid Aman Karume pamoja na kumuombea dua katika eneo la kaburi alipozikwa Mwasisi huyo wa Mapinduzi

Jumatatu, 9 Aprili 2018

SMZ NA CHINA WAZINDUA TEKNOLOJIA YA KILIMO CHA MPUNGA.

 WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud(kushoto wa pili) akimkabidhi zawadi ya mlango mdogo Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke, ikiwa ni ishara ya kuendeleza mahusiano baina ya Zanzibar na China.
  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud(kushoto wa pili) akimkabidhi zawadi ya mlango mdogo wataalamu wa kilimo.


 MGENI Rasmi Waziri Aboud Mohamed Aboud akiwasha pikipuki maalum ya kubebea mpunga kutoka bondeni ambayo ni miongoni mwa vifaa vya kisasa vilivyotolewa na Serikali ya China kwa wakulima wa bonde la Cheju waliofundishwa teknolojia mpya ya kilimo cha mpunga.
 


  WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Aboud Maohamed Aboud, akiwahutubia wananchi katika uzinduzi wa mashamba ya maonyesho ya kilimo bora cha mpunga na makabidhiano ya vifaa kwa ajili ya kilimo hicho kutoka serikali ya China  iliyofanyika bonde la Cheju Mkoa wa Kusini Unguja.

WAZIRI wa Kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi Rashid Ali Juma akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga bonde la Cheju.
 BONDE la mpunga la Cheju Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 

WAZIRI wa Kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi Rashid Ali Juma akitoa maelezo katika shamba darasa la kilimo cha mpunga katika bonde la Cheju.
 MKULIMA wa zao la mpunga kutoka Mkoa wa Pwani Zulfiker Mituro, akitoa ushuhuda baada ya kunufaika na kilimo hicho .

 WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar  Aboud Mohamed Aboud(kushoto) akibadilishana mawazo na Balozi wa Tanzania Nchini China Wang Ke, katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.
 Balozi wa Tanzania Nchini China Wang Ke, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.
 BAADHI ya wananchi na wataalamu wa masuala ya kilimo kutoka China wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya kilimo cha mpunga.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Aboud Mohamed Aboud amewataka wakulima  wa zao la mpunga kuchangamkia fursa ya teknolojia ya kisasa ya kilimo hicho kutoka nchini China.

Wito huo ameutoa leo katika hafla ya uzinduzi wa mashamba ya maonyesho ya kilimo bora cha mpunga na makabidhiano ya vifaa kwa ajili ya kilimo hicho kutoka kwa serikali ya China.

Hafla hiyo iliyofanyika katika bonde la mpunga la Cheju lililopo Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo Waziri huyo  amesema kilimo hicho kimefanyiwa tafti mbali mbali Tanzania bara na kubaini kina uwezo wa kuzalisha tani 4.5 hadi tani tisa kwa heka moja.

Aboud aliyemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd katika hafla hiyo, amewasihi wakulima wa mpunga visiwani Zanzibar kuipokea teknolojia hiyo na kuifanyia kazi ili wapate mavuno ya uhakika na kupunguza umaskini.

“ Itumieni vizuri teknolojia hii ya kilimo cha kisasa cha mpunga hakika mtapata mafanikio na Cheju itakuwa eneo maarufu kwa uzalishaji wa mpunga mwingi utakaosaidia serikali kupunguza uagizishaji wa chakula cha mchele kutoka nje ya nchi.” Amesema 

Teknolojia hii imekuja wakati mwafaka ikizingatiwa mchele ndio chakula kikuu hapa visiwani Zanzibar, na wakulima mkiweza kwenda sambamba na ujuzi na mbinu za kilimo hiki, naamini tutafikia kiwango cha kuwa na chakula cha kutosha hapa nchini”, anafafanua, Aboud.

Waziri Aboud ameeleza kuwa urafiki baina ya China na Zanzibar ulianza kuimarika baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na baada ya hapo China imekuwa ikitoa misaada katika sekta mbali mbali za SMZ na binafsi.

Ameahidi kuwa Serikali  itaendelea kushirikiana na China ili kuhakikisha wananchi wa nchi zote mbili wananufaika na mahusiano hayo ya kudumu na yenye tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza Waziri wa kilimo, maliasili, uvuvi na mifugo, Rashid Ali Juma amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya kilimo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanaondokana na kilimo duni na kufanya kilimo chenye manufaa ya kupata mazao mengi katika eneo dogo.

Amewasisitiza wakulima waliopewa taaluma hiyo mpya kuwa walimu wa kuwafundisha wakulima wengine ili teknolojia hiyo isambae katika mabonde mbali mbali hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi wa China Nchini Tanzania, Wang Ke amesema kilimo hicho kimekuwa ni sehemu ya mafanikio ya uzalishaji wa chakula cha kutosha katika taifa la China.

Amefafanua kuwa kilimo hicho kinafanyika kwa mfumo wa kanuni za kitaalamu kupitia utaratibu wa teknolojia hiyo, hivyo wakulima wanatakiwa kuwa makini ili wapate mazao mengi kwa kila msimu wa kilimo.

Amesema mbali na teknolojia hiyo pia taifa la China limetoa vifaa mbali mbali vya kumsaidia mkulima aweze kurahisisha kazi wakati wa kilimo.

Pia amesema baada ya kusambaza teknolojia hiyo ya zao la mpunga katika maeneo mbali mbali nchini, wataendelea kutoa teknolojia zingine zikiwemo ukulima bora wa mboga mboga na maboga.

Mapema Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao ameeleza kuridhishwa kwake na hatua za uimarisha wa serikali ya kilimo zinazotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema CCM inaisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kikamilifu ili wakulima wanufaike na sekta ya kilimo na kujinasua wimbi la umaskini na utegemezi wa chakula.

" Nampongeza Dk. Shein kwa kasi yake ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, na tukio la leo ni sehemu ya juhudi zake kwa kufungua milango ya ushirikiano na taifa la China.", amesema Catherine.

Amewambia wakulima wa bonde hilo kuwa wanatakiwa kuwa wabunifu pindi wanapofundishwa matumizi ya teknolojia hiyo ili wataalamu hao waweze kuwapa ujuzi wa teknolojia tofauti za kilimo.