Jumanne, 8 Oktoba 2019

DK.MABODI- AWAPIGA MSASA MAKATIBU WA CCM MKOA WA KUSINI UNGUJA

 
 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla Mabodi, akifungua Mafunzo Elekezi kwa Makatibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja wa ngazi za Matawi hadi Mkoa yaliyofanyika Chuo Cha Utawala wa Umma Tunguu,  Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, amewata Makatibu wa Chama hicho kubuni masuala mbali mbali ya kiutendaji yatakayoongeza ufanisi katika Shughuli za Chama na Jumuiya zake.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Makatibu wa CCM ngazi za Matawi hadi Mkoa katika Mkoa wa Kusini Zanzibar, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utawala wa Umma Tunguu, Zanzibar.

Dk.Mabodi amesema mafunzo hayo yamefanyika katika wakati mzuri wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020,hivyo Watendaji hao wanatakiwa kujifunza kwa bidii ili watekeleze kwa ufanisi shughuli za Chama.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amewambia Makatibu hao kuwa wanatakiwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa miongozo ya CCM na kuepuka kufanya kazi za Wanasiasa ikiwa wao wanakabiliwa na majukumu ya kiutendaji.

Pamoja na hayo amesisitiza kila Mtendaji kuendeleza kwa vitendo dhana ya kushuka kwa wananchi wa ngazi mbali mbali kwa lengo la kuratibu changamoto zao ili zifanyiwe kazi na Mamlaka husika.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi amewasihi Makada Wasomi Nchini kuhakikisha elimu waliyonayo wanawafundisha Wanachama wengine ili Chama kiwe imara katika masuala ya Uongozi,Utawala,Uchumi na Kijamii.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, amewapongeza Viongozi mbali mbali wa Mkoa huo kwa juhudi zao za kulinda heshima ya Mkoa huo kwa vitendo na ukaendelea kuwa ngome ya CCM Kisiasa.

Kupitia ufunguzi wa mafunzo hayo Dk.Mabodi, amewakumbusha Watendaji kuepuka vitendo vya rushwa ndani ya Chama kwani vinasababisha madhara ya kupatikana kwa viongozi wasiokuwa waadilifu.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja ambaye pia ni Kimu Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Suleiman Mzee Suleiman amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji makatibu hao ili wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Amesema Mkoa huo licha ya kuwa ni ngome ya CCM bado baadhi ya Makatibu wake walikuwa na changamoto ya ukosefu wa uwezo wa kuandaa mitahsari na taarifa mbali mbali za Chama.

Akisoma risala Katibu wa CCM Jimbo la Tunguu Sharifa Maabadi, amesema mafunzo yatatolewa kwa siku Sita na yatawashirikisha Makatibu 120  kuanzia ngazi za wadi hadi Mkoa.

Ameeleza kuwa katika mafunzo hayo Makatibu watafundishwa masuala ya Uongozi,Uzalendo,itifaki kwa Viongozi,utunzaji wa habari na kumbukumbu na mbinu za kuzungumza na kuwashawishi watu kuendelea kujiunga na CCM.

Aidha ametoa rai kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu kwani yatawasaidia Viongozi na Watendaji wa CCM katika Mkoa huo kuwa na Weledi na mbinu mbali mbali za kufanya kazi za Chama Cha Mapinduzi kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.

Jumapili, 6 Oktoba 2019

MAMA SALMA KIKWETE-KIKUNDI CHA UTALII 255 COMMUNITY.


MKE wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Rashid Kikwete,akiwahutubia waalikwa mbali mbali katika Hafla ya Uzinduzi wa Utalii 255 Community uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert Ilala, Dar es Saalam.

MWENYEKITI wa Kikundi cha Utalii 255 Community Mhe.Angelina Adam Malembeka, akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Jumuiya ya masuala ya kuhamasisha na kutangaza Vivutio vya Utalii wa ndani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shaaban Robart, Dar es Saalam

 BAADHI ya Wageni mbali mbali walioudhuria hafla ya Uzinduzi wa kikundi cha Utalii 255 Community wakisikiliza nasaha mbali mbali zinazotolewa katika uzinduzi huo.


MKE wa Rais Mstaafu Mama Salma Rashid Kikwete amewasihi Wanawake Nchini kufuata nyayo za  Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe.Angelina Malembeka katika kubuni miradi mbali mbali yenye maslahi kwa jamii.

Wito huo aliutoa katika uzinduzi wa Kikundi cha Utalii 255 Community huko katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, Ikala Dar es saalam, ambapo kikundi hicho  kinachojihusisha na masuala ya sekta ya Utalii pamoja na shughuli za jamii katika uzalishaji zikiwemo ujasiriamali. 

Amesema Sekta ya Utalii ni fursa ya kuikomboa Nchi kiuchumi hivyo juhudi zilizofikiwa na Mhe.Angelina zinatakiwa kuthamini na kupongezwa ili zisaidie vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika maelezo yeke Mama Salma Kikwete,amekitaka kikundi hicho kufanya kazi zake kwa bidii kubwa kwa lengo la kwenda na mahitaji ya kutangaza vivuti vya Utalii.

Kupitia hafla hiyo ya uzinduzi Mama Salma Kikwete, amewasisitiza Wanawake na Vijana kujitokeza kuwania fursa za Uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Pamoja na hayo amewashauri viongozi mbali mbali hasa Wabunge kufungua milango ya Kutangaza Utalii katika maeneo wanayotoka ili kikundi hicho kiwafikie na kuhamasisha jamii juu ya fursa hizo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kikundi cha Utalii 255 COMMNITY  Angelina Malembeka, 
amesema  kikundi cha utalii 255 kilianzishwa mwaka 2017 kimesajiliwa Mambo ya Ndani na cheti cha Utambuzi kutoka Manispaa ya Ilala mwaka 2019.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kikundi hicho ni kuwawezesha vijana wa makundi mbali mbali kunuika na fursa zinazopatikana katika kikundi hicho juu ya masuala ya Utalii sambamba na Ujasiriamali.

Aidha, ameeleza kuwa kikundi hicho kinafanya kazi zake kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara na muundo wa Wanachama wake wanatoka sehemu hizo kwa lengo la kuwaunganisha katika kuzifikia fursa za kukuza uchumi wa nchi.

Akizitaja baadhi ya kazi zinazotekelezwa na kikundi hicho kuwa ni kuelimisha juu ya ajira Binafsi ikiwemo ujasiriamali wa aina mbalimbali ufugaji,kilimo,uchoraji sanaa na kutangaza sekta ya Utalii wa ndani kwa jamii. 

Kwa upande wake Katibu wa Utalii 255 COMMUNITY Eveln Mwakatuma, amesema wanatarajia  kutembelea maeneo mbali mbali nchini, kwa sasa wameandaa safari ya Utalii kwa watoto yatima 100 ambao watakwenda kutembelea mbuga za wanyama watoto 50 kutoka Tanzania Tanzania Bara na 50 Zanzibar lengo la safari hiyo kujionea vivutio vya Utalii Tanzania.

Katika hafla hiyo Viongozi,Wanachama na waalikwa  mbali mbali walikabidhiwa Tuzo za heshima juu ya mchango wao katika kufanikisha shughuli mbali mbali za kijamii,kiuchumi na kimaendeleo.