Jumatano, 4 Aprili 2018

MHE.SAMIA AWATAKA WANANCHI, WABUNGE NA WAWAKILISHI KUSHIRIKIANA

 JUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan(kulia) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya siasa ya CCM  Mkoa wa Mjini na viongozi mbali mbali wa Chama mara baada ya kupokea taarifa ya hali ya kisiasa ya Mkoa wa mjini, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk.Abdulla Juma Mabodi(Katikati), Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud(kushoto).


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akipewa maelezo katika chumba maalum cha mafunzo ya Uunguzi katika Chuo Cha Mwenge Community Centre.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akipewa maelezo katika chumba maalum cha mafunzo ya fani ya Umeme katika Chuo Cha Mwenge Community Centre.
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na wanafunzi wa Chuo Cha Mwenge Community Centre kinachomilikiwa na CCM Mkoa wa Mjini Unguja katika mwendelezo wa ziara yake Unguja.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na wanafunzi, viongozi wa Mwenge FM Radio na walimu  wa Chuo Cha Mwenge Community Centre. 
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akifurahia ngoma ya asili ya Bomu wakati akizindua Ofisi ya UWT Mkoa wa Mjini.
 

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kusho) akikagua tawi la Jang’ombe Urusi , akiongozwa na  Mwenyekiti wa Tawi  hilo Mzee Ali Hassan Pandu(kulia).


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wana CCM wa Jang'ombe Urusi mara baada ya kukagua ujenzi wa Tawi la kisasa la Jang'ombe Urusi.
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi katika tanki la maji safi na salama Jimbo la Kikwajuni.
MBUNGE wa Jimbo la Kikwajuni Mhandisi Hamad Masauni(kulia wa mwanzo anayezungumza) akiwatambulisha madiwani wa wadi za Rahaleo na Kikwajuni kwa  Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan .

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na wananchi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mhe. Samia katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akipewa maelezo juu ya ramani ya mtandao wa maji safi na salama katika jimbo la Kikwajuni Unguja.
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan (kusho)  akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Jumiya ya Watu wenye ulemavu Jimbo la Shauri Moyo Makame Kai (kulia mwenye suti nyeusi) katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwenye Ofisi ya Jumuiya hiyo.
 


 Mwenyekiti wa Jumiya ya Watu wenye ulemavu Jimbo la Shauri Moyo Makame Kai akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Jumuiya ya watu wenye ulema
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.



MAKAMU wa Pili wa Rais,Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa visiwa vya Zanzibar kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Wabunge na Wawakilishi wa majimbo ili waongeze ari na kasi ya kutatuzi wa kero zinazoikabili jamii.

Rai hiyo ameitoa leo  katika mwendelezo wa ziara yake visiwani Zanzibar alipokutana na wanachama  wa CCM na wananchi wa  jimbo la Kikwajuni na  kuzungumza nao katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa tanki la maji safi na salama lenye uwezo wa kuhifadhi lita zaidi ya 200,000 katika jimbo la kikwajuni.

Amesema endapo wananchi watakuwa mstari wa mbele kuthamini miradi ya wabunge na wawakilishi kwani inatekelezwa kwa lengo la kumaliza changamoto zinazoikabili jamii.

“Wananchi mkiwa na umoja na kushirikiana kulinda na kuthamini yale yote mazuri yanayofanywa na viongozi wenu basi itakuwa rahisi sana kutatua kero zenu kwa wakati”, amesema Mhe. Samia

Pia amewataka wabunge na wawakilishi wa majimbo mbali mbali kuwa na maelewano mazuri  mazuri  kwa lengo la kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.

Amesema kitendo cha viongozi hao kutokuwa na maelewano mazuri yanasababisha kukwamisha na  kuwacheleweshea wananchi kupata maendeleo kwa wakati.

Makamu huyo wa Rais ameongeza kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo viongozi hao hawana ushirikiano na kwamba wanafikia hatua hawaongeii na kutofikiria kuleta maendeleo.

"Kuna majimbo ambayo wananchi wao wanakumbwa changamoto ya ukosefu wa maji na elimu na kwamba unakuta viongozi hao kati ya Mbunge na Mwakilishi hawafikirii kutatua kero za wananchi hizo kutokana na kuwa hawana ushirikiano,"amesema Samia.

Mbali na hilo katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa tanki la maji safi na salama jimbo la Kikwajuni pamoja na jiwe la msingi la ofisi ya tawi la Chama Cha Mapinduzi(CCM) Jang’ombe Urusi.

Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo la Kikwajuni kuhakikisha wanatunza miradi ya maendeleo ya maji na kwamba wanatakiwa kuanzisha kamati ya jimbo kwa lengo la kusimamia miradi hiyo ili iwe endelevu.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Mabodi, amesema CCM ipo kikazi na inaenda na wakati katika kutatua kero za wananchi.

 Ameeleza kuwa CCM inawahakikishia wananchi kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imejipanga kuwatatulia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ambapo inaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuhakikisha mikoa yote ya Zanzibar inapata huduma hizo.

Naibu huyo ameeleza katika kipindi hichi cha dharura SMZ na kushirikiana mradi wa Ras Al Khaimah imechimba visima 120 vya maji visiwani Zanzibar.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Hamad Yussuf Masauni, amesema kupitia mradi huo wa maji wa awamu ya pili utatatua changamoto ya upatikanaji wa maji unatokana na miundombinu ilioko zamani ambapo nyingi zilikuwa mibovu mengine ilipasuka na kuziba.

"Baada ya kumalizika mradi huu tunafumua mfumo wa maji wa jimbo la kikwajuni na tunaweka mfumo mpya wa kwetu ambao safari hii maji yatapatikana kwa urahisi na wananchi mtafurahi,"amesema Mhe. Samia.

Aidha ametembelea ujenzi wa Tawi la CCM Jang’ombe Urusi na kuwapongeza viongozi wa Jimbo la Jang’ombe kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na kuwataka wawe walimu wa majimbo mengine.

Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia ameweka Jiwe la msingi katika Ofisi ya Watu Wenye Ulemavu Jimbo la Shauri Moyo Unguja, na kuipongeza jumuiya hiyo kwa ubunifu wao wa kujenga ofisi ya kuzalisha kipato.

Amezitaka familia zenye watu wenye ulemavu kuwapeleka katika ofisi hiyo ili wajifunze fani mbali mbali zitakazowasaidia katika maisha ya kila siku.

Ameahidi kutatua hatua kwa hatua changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo ambazo ni pamoja na ukosefu wa viti vya watu wenye ulemavu, mashine ya photokopi ya rangi na mahitaji mengine.

Katika Hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi amesema Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar imeahidi kuchangia  shilingi 500,000 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za watu wenye ulemavu.

Hata hivyo ametembelea Chuo Cha Mwenge Community Centre kinachotoa mafunzo ya fani mbali mbali yakiwemo ya  ushoni, umeme, computer, Uuguzi na Uandishi wa habari kinachomilikiwa na  CCM Mkoa wa mjini.

Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Mohamed Nyawenga alisoma na kumkabidhi taarifa ya hali ya kisiasa kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Bi. Samia Suluhu Hassan.

Kupitia kikao hicho aliwataka viongozi na watendaji wa Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii sambamba na kulinda heshima ya Mkoa huo wenye historia kubwa ya uimara wa kisiasa na kijamii nchini.

Pia amewaagiza kutunza vizuri miradi ya maendeleo inayomilikiwa na Mkoa huo ili kwenda sambamba na sera ya siasa na uchumi.




















Jumanne, 3 Aprili 2018

MHE.SAMIA -AANZA ZIARA NA KUTEMBELEA MIRADI YA CCM KATIKA MKOA WA MAGHARIB Z'BAR

  MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan(katikati), Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdulla Juma Mabodi(wa kwanza kushoto) pamoja na viongozi na wananchi wengine wakisikiliza maelezo ya kitaalamu ya Katibu wa Jumuiya ya wakulima wa kizimbani. Ndugu Shafii Kibwana Said(kulia). 
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akieleza mafanikio yaliyopatikaka  kupitia  utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Sekta ya kilimo huko katika bonde la mpunga la Kizimbani.


 BAADHI ya wananchi na Wana CCM wakishiriki katika upandaji wa mpunga katika bonde la Kizimbani katika zira ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan.


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi katika hafla ya maandalizi ya kilimo cha mpunga na upandaji wa Mpunga katika bonde la kizimbani Unguja, kilimo kinaendeshwa na Wana CCM wa Jimbo la Bububu na maeneo jirani.
 ENEO lililopandwa mpunga katika bongde la kizimbani  katika ziara ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Hassan Suluhu iliyofanyika leo katika Mkoa wa Mjini.


 MJUMBE wa Kamati ya uhifadhi mazingira ya fuoni Kibondeni Ndugu Mwaka Masoud akisoma risala baada ya kuwasili mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan katika maeneo ya Fuoni Kibondeni.
  MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akielekea katika eneo la ufugaji wa kaa huko Fuoni Kibondeni. 

  MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi Tawi la Fuoni kibondeni.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameridhishwa na kasi ya viongozi wa CCM ya kuresha utamaduni wa kurudi kwa wananchi wa chini kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi  wa kudumu.

Amesema kwa kiasi kikubwa wananchi walikuwa wamepoteza imani kwa CCM kutokana na kuwa viongozi wengi walikuwa wanatabia ya kukaa ofisini n kutowafikia wananchi hao na kusikiliza changamoto zao zinazowakabili.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi wanaotumia bonde la mpunga la Kizimbani Unguja katika ziara yake ya kutembelea miradi mbali mbali inayotekelezwa na  Wana CCM katika maeneo hayo ya kilimo cha mpunga.

 Mhe. Samia ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  amesema  kuwa  ile dhana ya  CCM mpya na Tanzania mpya imeanza kustawi katika fikra za Wana CCM na kufanyiwa kazi kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2015.

"CCM mpya imeanza kuonekana ikiwemo kuwafuatilia wananchi wa chini zaidi kwa mfano katika mikakati ya kufuatilia kaya maskini kwenye miradi ya TASAF viongozi wa chama wameanza kuonekana kufuatilia utatuzi wa changamoto za kuondoa hali ya umaskini hivyo CCM iko karibu na wananchi kwa sasa," amesema Makamu wa Rais.

Katika maelezo yake Makamu huyo wa Rais, alisema ni ukweli kuwa chama cha siasa ni watu na kwamba chama hicho chochote cha siasa kinapaswa kuwa karibu na wananchi  kwani wao ndio walioiweka Serikali madarakani.

Amewataka viongozi na watendaji wa CCM kukukumbushana kuwa pindi wanapopewa dhamana za uongozi hawatakiwi kukaa maofisini bali wana majukumu ya msingi ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia, aliwapongeza wanajumuiya wa wakulima wa kilimo cha mpunga Kizimbani kwa juhudi zao za kuungana kwa jumuiya ambapo itawasaidia kuweza kusaidiwa kwa urahisi kwa pamoja kwenye sekta ya kilimo ikiwemo kupata mbolea kwa haraka.

Makamu wa Rais Samia ameahidi wanajumuiya hiyo kuwasaidia kiasi cha fedha na kuwapatia trekta kupitia CCM ili kuisaidia katika kilimo chao cha mpunga katika mabonde hayo mpunga ya Kizimbani na maeneo mengine.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk.Abdulla  Juma  Mabodi  amesema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kutatua  kero za wananchi hatua kwa hatua na kwa sasa kimesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wanaolima zao la mpunga katika bonde la Kizimbani.

Dk. Mabodi ameeleza kuwa lengo la kuwasaidia wakulima hao ni kukabiliana na changamoto za upungufu wa chakula hasa mchele ambao wakulima wengi wamewekeza  nguvu zao katika kilimo cha mpunga.

Mapema Mbunge wa Jimbo la Bububu na anakaimu Jimbo la Mtoni, Ndugu Mwatantakaje Haji Juma amesema kuwa bonde hilo lina wakulima zaidi ya 700 kutoka jimbo hilo na maeneo ya jirani.

Ameeleza kuwa mradi wa kilimo kilimo cha mpunga katika bonde hilo ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, ambayo viongozi mbali mbali wa jimbo wamekuwa wakitumia rasilimali fedha kuunga juhudi za wananchi ambao ni wakulima wa zao la mpunga.

 Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wakulima wa kilimo cha Mpunga Kizimbani, Shafii Kibwana Said alimshukuru Makamu huyo wa Rais kwa hatua aliyoifanya kuwafuata wakulima hao walioko chini kwa kuwasikiliza changamoto zao na kuonesha nia ya kuzitatua.

Alisema matokeo ya faida walioanza kunufaika nayo kupitia serikali ya CCM ni pamoja na kupata mbolea kwa gharama nafuu ambapo wanajumuiya hiyo wanalipa asilimia 25 ya mbolea huku serikali ikiwalipia asilimia 75.

Wakati huo huo ametembelea  eneo la uhifadhi wa mazingira huko  Fuoni Kibondeni  na kushiriki  katika uvunaji wa kaa, ambapo awasifu juhudi za Jumuiya ya uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko ambayo ni sehemu ya kulinda mazingira ya bahari.

Amesema kila mwananchi ana jukumu la kulinda mazingira yasiharibiwe hivyo kitendo cha Wana CCM na wananchi kwa ujumla kujitolea na kuhifadhi mazingira ni hatua muhimu inayotakiwa kuungwa mkono na Chama pamoja na Serikali.

Akiendelea na ziara hiyo pia  ameweka jiwe la msingi Tawi la Fuoni Kibondeni , na kuwasisitiza wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuendeleza utamaduni wa kujitolea katika utekelezaji  miradi ya Chama.

Ameelezea kufurahishwa kwake na hatua zilizofikiwa katika Tawi hilo ambalo chimbuko lake limetokana na Tawi la zamani la ASP, lililozalisha wanachama wazalendo na wenye msimamo imara juu ya Chama chao.

Mapema  Katibu wa CCM Mkoa wa Magharib Bi. Aziza Mapuri amemkabidhi taarifa ya hali ya kisiasa ya Mkoa huo iliyoeleza mipango endelevu ya kuimarisha CCM kisiasa, kiuchumi na kijamii itakayokiwezesha Chama hicho kushinda katika uchaguzi Mkuu ujao.