Jumatano, 7 Juni 2017

SALAMU ZA RAMBI RAMBI ZA CCM KUHUSIANA NA KIFO CHA MAREHEMU PROF. ISHAU ABDULLAH KHAMIS.


CHAMA Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyewahi kuwa Mjumbe  wa Halmashauri Kuu na Afisa Mwandamizi (Mstaafu) wa Idara ya Organaizesheni CCM Zanzibar Marehemu Prof. Ishau Abdullah Khamis, kilichotokea tarehe 06 Juni, 2017, katika Hospitali ya Muhimbili, Mjini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg. Abdulla Juma Saadalla (Mabodi) kwa niaba ya Viongozi, Watumishi na Wanachama wote wa CCM, ametuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Mzee Ishau na kuwaomba kuwa na moyo wa subra katika wakati huu mgumu wa maombolezi yampendwa wetu huyo. Bila ya shaka kifo cha marehemu kimeacha pengo kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa letu kwa ujumla.

Naibu Katibu huyo wa CCM Zanzibar amesema, Chama Cha Mapinduzi kimempoteza mwanachama mahiri, mchapakazi hodari, mpenda watu wa rika na jinsia zote na kwamba kifo chake kimekuja wakati Chama bado kinamhitaji kutokana na utumishi wake uliotukuka.

Katika uhai wake, na katika nyakati tofauti, marehemu Prof. Ishau Abdullah Khamis, aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Mkuu wa Mkoa, Mwalimu katika Chuo cha Uchumi (Dar), Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na  Waziri wa Utalii na Misitu.

Kwa upande wa Chama marehemu aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Katibu wa Fedha, uendeshaji na Miradi ya Chama, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Idara ya Organaizesheni - Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, cheo alichoshikilia hadi mwaka 2014, alipostaafu Utumishi wa Chama.


Kama hiyo haitoshi na kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Utumishi wa Umma, mwaka 2016, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu ya Zanzibar, cheo ambacho alikuwa nacho hadi umauti ulipomfika.

Chama Cha Mapinduzi kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu Tunamuomba Mwenyezi Mungu muumba Mbingu na Ardhi na Vyote viliomo ndani aiweke roho ya marehemu mahali pema Peponi. AMIN.


(Waride Bakari Jabu),
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
07/06/2017

PEREIRA ATOA NASAHA NZITO KWA VIONGOZI WA CCM Z'BAR



Ni  Katibu wa NEC,  Idara ya Organazesheni CCM Taifa,Nd. Pereira Ame Silima   akizungumza na Wajumbe wa  Kamati  ya siasa ya Mkoa ya CCM Mjini pamoja na Wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho huko  Katika Ukumbi wa CCM  Amani Unguja.

Ni  Baadhi ya Wajumbe wa  Kamati  ya siasa ya Mkoa ya CCM Mjini pamoja na Wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho wakimsikiliza kwa Umakini Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima   huko  Katika Ukumbi wa CCM  Amani Unguja.

KATIBU wa NEC,  Idara ya Organazesheni ya CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima amewataka viongozi na watendaji wanaochaguliwa kwenye uchaguzi wa chama na jumuiya zake  kwa sasa kuwa na fikra na mitizamo mipya itakayoongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya CCM.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za  siasa za Mikoa ya CCM Mjini na Magharibi pamoja na wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho huko Amani Unguja, alisema chama hicho kitaendelea kuwa imara kutokana na utamaduni wa kupata viongozi kwa njia za kidemokrasia hasa Uchaguzi huru na wa haki.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha chama sambamba na kujitambulisha kwa viongozi hao kwani tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo hivi  karibuni Mjini Dodoma hiyo ndio ziara yake ya mwanzo.

Alizitaka kamati mbali mbali zilizopewa dhamana ya kusimamia na kuchuja viongozi katika  uchaguzi wa chama hicho kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye nia ya kweli ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji ndani ya chama hicho na sio wababaishaji.

Aidha Katibu huyo alisema Chama hicho kina nia ya kuanzisha utaratibu wa kutengeneza kadi za uanachama zitakazokuwa katika mfumo wa kielectroniki ili kupata idadi kamili ya wanachama kwa lengo la kujipanga katika michakato ya uchaguzi wa ndani na wa Dola.

“ Viongozi na watendaji wenzangu tujue kuwa chama cha mapinduzi kipo kwa ajili ya wananchi wote hivyo lazima tufanye kazi kwa ushirikiano ili tutimize kwa vitendo dhamira ya mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Katiba yanayolenga kuongeza ufanisi katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiuchumi ndani ya chama chetu.”, alisema Katibu  Amen a kuongeza kuwa dhana ya CCM mpya itekelezwe na kusimamiwa na fikra mpya na sio upya wa viongozi wanaochaguliwa kwa sasa.

Alisisitiza umuhimu wa kufuata  Katiba kwa kila hatua  ya kufanya maamuzi ndani ya chama hicho kwa lengo la kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima kwa baadhi ya wanachama wanaokwenda kinyume na maadili ya Chama hicho.

Hata hivyo aliyataja majukumu muhimu yanayotakiwa kutekelezwa na idara yake kuwa ni kusimamia Uchaguzi wa Chama na Dola pamoja na  kusimamia jumuiya za CCM kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa miongozo ya Kikatiba.

Mapema akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Bora Afya Silima Juma alisema  Mkoa huo unaendelea kupanga mikakati ya kudumu itakayosaidia chama hicho kushinda katika Uchaguzi  Mkuu ujao.

Akisoma taarifa ya utekelezaji Katibu wa CCM Mkoa wa  Magharibi, Aziza Ramadhan Mapuri alisema licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo katika uchaguzi unaoendea hivi sasa ndani ya mkoa huo wamefanikiwa kuwapata viongozi makini na wachapaka kwa baadhi ya ngazi ambazo tayari zimeshakamilisha zoezi hilo.