Jumamosi, 22 Desemba 2018

NAIBU KATIBU MKUU WAZAZI ATUA Z'BAR, MAPOKEZI YAKE HAIJAWAHI KUTOKEA.

 NAIBU Katibu Mkuu wa Wazazi Ndg.Othman Ally Maulid akivishwa koja mara baada ya kuwasili Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa kushika wadhifa wake. 

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya ya Wazazi Zanzibar,Najma Murtaza Giga, amemtaka Naibu Katibu Mkuu mpya wa jumuiya hiyo, Othman Ally, kuendeleza mabadiliko yaliofanyika ndani ya jumuiya ikiwemo kutunza na kuthibiti mali za jumuiya hiyo. 

Giga amesema jumuiya hiyo kwa sasa inaendana na mabadiliko hayo ambayo jumuiya imeshirikiana na chama katika kuzitunza mali hizo.

Amesema  jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi(CCM),kimefanikiwa kuwabaini na kuwatia nguvuni waliohusika na upotevu wa mali za jumuiya hiyo hivyo ni vyema kwendana na mabadiliko hayo.

Mbali na hilo, Giga amesema  jumuiya hiyo iko salama na kwamba hakuna tuhuma zozote zilizoikumba wanachama wa jumuiya katika suala la usaliti na mambo mengine.

Kauli hiyo ameitoa katika hafla ya mapokezi ya mrithi wake kiungozi mjini Unguja ambapo amesema anamkabidhi jumuiya hiyo ikiwa katika hali ya usalama ikiwemo kutokuwepo kwa majungu na makundi.

"Hali hii inatokana na kuwepo kwa upendo baina ya viongozi wa jumuiya hiyo ikumbukwe katika jumuiya hii hakuna viongozi waliopatikana na suala la usaliti wa tuhuma zozote zile," amesema

Naye Naibu Katibu Mkuu huyo mpya, Othman Ally alisema atahakikisha anaendeleza hatua zilizofanyika na uongozi uliopita kwa kuzingatia katiba na misingi ya jumuiya hiyo.

Amesema  jukumu lilokabidhiwa ni kubwa ikiwemo kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 CCM ina shinda na kwamba lazima wanachama wa jumuiya hiyo watoe ushirikiano ili kutekeleza azma ya ushindi wa chama katika uchaguzi huo.

"Tufanye kazi kwa ushirikiano tuache makundi,majungu na hata hivyo ninamshukuru Rais na Mwenyekiti wa Taifa John Magufuli kwa kuendelea kukijengea heshima chama,"amesema 

Ameongeza kuwa kazi ambayo ataendelea kufanya ni pamoja na kuhakikisha jumuiya hiyo inaongeza idadi ya wanachama katika CCM na kwamba hatokubaliana na kuwepo kwa makundi ndani ya jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar wa CCM,Dk.Abdallah Sadala Juma 'Mabodi' amewataka  wanajumuiya na viongozi wa jumuiya hiyo kumpa ushirikiano Naibu Katibu Mkuu huyo mpya katika kutekeleza maendeleo ya CCM.

Amesema jumuiya hiyo ni chachu,tegemeo kubwa kwa chama katika kusimamia maadili na mambo ya kisiasa hivyo wanachama wa jumuiya wanapaswa kuelewa kuwa jumuiya hiyo ina historia ndefu.
"Jumuiya hii ndio msimamizi wa kazi za chama hivyo tunatakiwa tumpe ushirikiano wa kutosha Naibu huyu mpya mimi nimefurahi kuwa tumempata mtu makini na tunakukaribisha katika utendaji kichama,"ameeleza.

Ijumaa, 21 Desemba 2018

NAIBU KATIBU MKUU MPYA WA UWT ZANZIBAR NDG.TUNU JUMA KONDO APOKELEWA KWA SHANGWE.


 
NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo akivishwa koja ikiwa ni ishara ya mapokezi yake mara baada ya kuwasili kisiwanduzi Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.


 
NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CCM Zanzibar  Ndugu Khadija Kabir(kushoto) mara baada ya kuwasili Zanzibar  kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.


 
NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo akifurahia na wanachama wa UWT katika mapokezi hayo.


 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo akizungumza na viongozi wa Jumuiya hiyo wa ngazi mbali mbali Zanzibar.



NAIBU Katibu Mkuu mpya wa Zanzibar wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Tunu Juma Kondo, amesema atahitumikia jumuiya hiyo kwa hekima na busara ili kutimiza kwa vitendo malengo ya CCM na Jumuiya hiyo.

Amesema baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ametambua kuwa siasa ni hekima na busara hivyo katika utendaji wake atafanya kwa misingi hiyo kwa uadilifu mkubwa.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na wanajumuiya wa UWT katika ukumbi wa CCM kisiwandui,Naibu huyo alisema hakutarajia kushika nafasi hiyo na kwamba utaratibu wa chama ni mzuri wa kuwateua viongozi bila ya ubaguzi.

Katika maelezo yake Naibu huyo alisema CCM haina ubaguzi na kwamba inazingatia utendaji wa mtu na si vinginevyo akitoa mfano alisema kwa upande wake hakutarajia kuwa siku moja atapewa jukumu kama hilo.

"Nashukuru UWT kwa kuridhia jina langu lipelekwe katika uongozi wa juu wa chama hivyo sina budi kuwashukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk.John Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM,Dk.Bashiru Ally,kamati ya Halmashauri Kuu kwa kuniamini na wameonesha imani kubwa kwangu,"amesema Naibu Katibu Mkuu huyo Tunu aliwataka wanajumuiya hiyo kumpa ushirikiano katika utendaji wake na amewataka wakumbuke kuwa siku za mbele kuna uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kwamba wao ndio wapiganaji hivyo wanapaswa kushirikiana.

"Naomba tushirikiane kwa karibu kutokana na kuwa ushirikiano wetu ndio nguzo ya utendaji katika kuwasemea wanawake wenzetu na watoto wetu ninaomba sana ushirikiano wenu kwani nyinyi wanajumiuya ndio mmenifanya kuwa Naibu Katibu Mkuu,"alisema Kwa upande wake Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi,Mgeni Hassan Juma alisema anashukuru Mwenyekiti wa Taifa CCM,kwa kumteua kuwa Naibu Katibu Mkuu na kwamba uamuzi alioufanya ni sahihi.

Amesema Naibu huyo anatosha katika nafasi hiyo na kwamba akiwa mwanamke wanamatarajio makubwa katika jumuiya hiyo kutokana na uwezo wake wa kiutendaji wa muda mrefu ndani ya UWT.

"Tunamuelewa sana uwezo wake katika utendaji wake wa kazi na kwamba ni mstaarabu,mvumilivu na ana hekima hivyo kwa kipindi kirefu amekuwa akikaimu nafasi hiyo na amefanya kazi za siasa ndani ya jumuiya,"amesema Naibu Spika huyo.

Katika maelezo yake ameongeza kuwa Tunu amefanya mambo mengi ndani ya jumuiya hiyo ikiwemo amesimamia uchaguzi wa jumuiya kwa usalama hivyo wanajumuiya ya wanatarajia Naibu Katibu Mkuu huyo kusimamia kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 kwa uweledi mkubwa.

Akizungumza katika Mapokezi hayo Mjumbe wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ndugu Mgeni Hassan Juma ameeleza kuwa matumaini yake juu ya Naibu Katibu Mkuu huyo aliyeteuliwa hivi karibuni ataweza kuongoza kwa ufanisi jumuiya hiyo.

Naye Mwakishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Hidaya Ali Makame, amesema kwamba Naibu Katibu Mkuu huyo amekuwa ni kiongozi asiyejikweza anayefanya kazi na wanachama wa ngazi zote ndani na nje ya chama hicho.