Jumapili, 9 Desemba 2018

MAKATIBU WA SIASA NA UENEZI WA MATAWI NA WADI WILAYA YA DIMANI WAPIGWA MSASA


MWAKILISHI wa Jimbo la Kijitopele Mhe.Ali Suleiman Shihata akifungua Mafunzo ya Siku Moja ya Kuwajengea Uwezo Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM ngazi za Matawi na Wadi za Wilaya ya Dimani Kichama yaliyofanyika Tawi la CCM Mwanakwerekwe.

 KATIBU wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Dimani Ndugu Hassan Suleiman Jaku 'Hassan Bosi' akizungumza katika Mafunzo hayo.
 BAADHI ya Washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini nasaha za mgeni rasmi 
 AKISOMA Taarifa ya Mafunzo Katibu wa Siasa na Uenezi Tawi la Mbweni Ndugu Asya Ali Khamis.
 Akitoa mada ya maandalizi ya Mikutano ya Hadhara pamoja na Itifaki na Ushiriki katika Mikutano Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ya Mfenesini Haji Abdallah Daima.

 KADA  wa CCM Baraka Mohamed Shamte, akitoa mada ya Kazi na wajibu wa Makatibu wa Siasa na Uenezi kwa Mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo jipya la mwaka 2017.



NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKATIBU wa Siasa na Uenezi wa ngazi za Matawi na Wadi nchini wametakiwa kutangaza  Sera imara za Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayotekelezwa kwa ufanisi katika maeneo mbali mbali nchini ili jamii ijue kwa upana maendeleo yaliyofikiwa katika nyanja za kisiasa, kijamii na kichumi.

Rai hiyo ameitoa Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Mhe.Ali Suleiman Shihata leo wakati akifungua Mafunzo ya Siku moja ya kuwajengea Uwezo Makatibu wa Siasa na Uenezi wa Ngazi za Matawi na Wadi za CCM Wilaya ya Dimani Kichama yaliyofanyika Tawi la CCM Mwanakwerekwe Unguja.

Mwakilishi huyo amewakumbusha  Makatibu hao kwamba pamoja na majukumu mbali mbali waliyokuwanayo bado wana wajibu wa kutangaza na kueneza kwa kasi kubwa Sera za maendeleo zinazotekelezwa kwa vitendo katika maeneo yao  na Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.

Amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya ustawi wa maendeleo na kijamii katika Sekta mbali mbali jambo linalotakiwa kufafanuliwa vizuri na Makatibu hao ili wananchi wapate kufahamu utekelezaji wa ahadi wa viongozi wao waliowapa ridhaa ya kuongoza nchi kupitia mfumo huru wa Kidemokrasia.

Katika maelezo yake Shihata amewasisitiza Makatibu hao kuwa wabunifu na wenye kujituma katika kuibua masuala mbali mbali yatakayokijenga Chama Cha Mapinduzi Kisiasa na Kiitikadi, ili kiende sambamba na siasa za sasa zinazotatminiwa kwa maendeleo ya kiutekelezaji kuliko maneno mengi ya majukwaani.

Pamoja na hayo ametoa tahadhari kwa kuwataka Makatibu hao wasimamie utaratibu wa baadhi ya Watu wanaojitokeza wakitaka kupewa kadi za CCM bila kupitia mdarasa ya Itikadi wachunguzwe kama wana sifa ya kuwa makada wa kweli ama wana lengo la kupata kadi kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Aidha amewataka watendaji hao kuwa na msimamo imara usioyumba kwa kufanya kazi kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na wasifanye kazi kwa matakwa ya Watu binafsi badala yake wasimamie kwa uadilifu maslahi ya Chama kwanza.

Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Dimani Ndugu Hassan Suleiman Jaku, amesema Mafunzo hayo yanatokana na agizo la CCM baada  ya kuwapatia Mafunzo kama hayo Makatibu wa Siasa na Uenezi wa ngazi za Majimbo, Wilaya na Mikoa yote yaliyofanyika Juni 23, mwaka 2018, waliwaagiza Makatibu hao washuke ngazi za Matawi hadi Wadi kuwajengea uwezo Makatibu  wa ngazi hizo.

Amefafanua kuwa Mafunzo hayo yatakuwa endelevu katika Wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha kazi za CCM zinafanywa kwa mujibu wa Taratibu za Kikatiba, Kanuni na Miongozo ya CCM, na zitekelezwe katika hali ya ufanisi wenye tija kwa wanachama wote.

Awali akisoma Taarifa ya Mafunzo Katibu wa Siasa na Uenezi Tawi la Mbweni Ndugu Asya Ali Khamis amesema jumla ya Makatibu 47 wameshiriki katika mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wajiimarishe kiitikadi, kisiasa na kimkakati kwa lengo la kufanikisha kwa ufanisi mikakati mbali mbali ya Chama na Serikali zake.

Kupitia taarifa hiyo waliomba Watu wanaotaka kujiunga na CCM lazima wapatiwe mafunzo ya miezi katika Matawi yao na wasimamiwe na kufuatiliwa kwa karibu na wahusi.

Kwa upande wake Kada wa CCM Ndugu Baraka Mohamed Shamte, Akitoa mada ya Kazi na wajibu wa Makatibu wa Siasa na Uenezi kwa Mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo jipya la mwaka 2017,amewataka viongozi hao kusoma na kuchambua kwa kina Katiba, Ilani na miongozo mbali mbali za Chama cha Mapinduzi ili wafanye kazi zao kwa kujiamini na kwa uhakika zaidi.

Amesema CCM itaendelea kuwa Taasisi bora ya kisiasa endapo viongozi na Watendaji wake watakuwa mstari wa mbele kufuata maadili na miiko ya uongozi kwa lengo la kujenga Chama bora chenye misingi imara ya kimaadili.

Akitoa mada ya Wajibu wa Viongozi na Watendaji wa CCM Kujiimarisha Kiitikadi na Kimkakati wa kuweza kujenga nguvu imara zaidi ya Mapambano ya ushindi , Kada wa CCM Ndugu Mohamed Haji Hassan, amesema kuwa kila mwachama wa CCM anatakiwa kuwa muadilifu anayeamini na kutetea misingi ya umoja, uzalendo na ukweli usiokuwa na shaka wakati wote.

Amewambia  Makatibu hao kuwa ushindi wa CCM utatokana na juhudi binafsi wa viongozi wanaofanya kazi za Chama kwa kufuata miongozo ya Kitaasisi inayobadilika kulingana na matakwa ya nyakati kwa lengo la kusimamia ipasavyo mikakati ya maendeleo kwa kila vipindi tofauti vya uongozi.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ya Mfenesini Ndugu Haji Abdallah Daima,  akitoa mada ya maandalizi ya mikutano ya hadhara pamoja na Itifaki na Ushiriki katika Mikutano, amesema Makatibu hao ni lazima wajue masuala ya itifaki na maandalizi ya mikutano na shughuli za Chama kwa lengo la kuepuka kasoro mbali mbali zinazoweza kuharibu shughuli za kisiasa.

Katika Mafunzo hayo zimetolewa Mada tano zikiwemo Kazi na wajibu wa Makatibu wa Siasa na Uenezi kwa Mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo jipya la mwaka 2017, ya Wajibu wa Viongozi na Watendaji wa CCM Kujiimarisha Kiitikadi na Kimkakati wa kuweza kujenga nguvu imara zaidi ya Mapambano ya ushindi , Maandalizi ya Vikao na uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu , maandalizi ya mikutano ya hadhara pamoja na Itifaki na Ushiriki katika Mikutano pamoja . 

Alhamisi, 6 Desemba 2018

DK.MABODI: AFANYA MKUTANO WA MAJUMUISHO, AWATAKA WANANCHI WACHAMKIE FURSA WIZARA YA UWEZESHAJI Z'BAR.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na Watendaji wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya za Unguja katika Mkutano wa Majumuisho ya Ziara zake za kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Taasisi hizo.

 BAADHI ya Watendaji wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya za Unguja wakisikiliza maelekezo ya hotuba ya  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi katika Mkutano wa Majumuisho uliofanyika katika Kisiwandui, Afisi Kuu ya CCM Zanzibar. 

 Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa Zanzibar Mwl.Kombo Hassan Juma, akizungumza katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara ya Dk.Mabodi katika Manispaa na Halmashauri za Wilaya Unguja.

 MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Magharibi ndugu Mohamed Rajab akizungumza katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara ya Dk.Mabodi katika Manispaa na Halmashauri za Wilaya Unguja.

 Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Amini Salmin Amour, kichangia hoja juu ya masuala mbali mbali kiutendaji katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara ya Dk.Mabodi katika Manispaa na Halmashauri za Wilaya Unguja.
 Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Garos Nyimbo akizungumza katika Mkutano huo wa Majumuisho ya Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi. 

 MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa ufafanuzi wa hoja mbali zilizotolewa katika Mkutano huo wa Majumuisho.

 Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Garos Nyimbo akizungumza katika Mkutano huo wa Majumuisho ya Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi. 
  
 AFISA Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Kusini akizungumza katika Mkutano huo.



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR. 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimebainisha kuwa endapo vikundi vya Ujasiriamali vitajengewa mazingira rafiki ya kupewa mitaji na mikopo yenye masharti nafuu itasaidia kuwainua wananchi.  

Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi katika majumuisho ya ziara zake katika Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri za Wilaya  na Mabaraza ya Manispaa za Unguja. 

Amesema sekta ya Ujasiriamali inategemewa na wananchi wengi kutokana na kuwa ndio sehemu rahisi ya wananchi kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. 

Ametoa wito kwa wananchi kuchamkia fursa za mikopo iliyopo Wizara ya Kazi, Uwezeshaji ,Wazee, Wanawake na Watoto ili wajikwamue kiuchumi.

Ameeleza kwamba wakati umefika wa serikali Kuu na Serikali ya Mitaa 
nchi kuvipa kipaumbele kwa kuviwezesha vikundi vya ushirika kupitia mfumo wa ugatuzi viweze kujitegemea na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyotoa ajira kwa wingi kwa vijana. 

Ameziagiza Manispaa na Halmashauri za Wilaya kuwasimamia Maafisa Ushirika watoe elimu na kuwahamasisha wananchi wajiunge na vikundi vya ushirika waweze kukopeshwa fedha kwa masharti nafuu.

Katika maelezo yake Dk. Mabodi amesema Wizara ya Kazi, Uwezeshaji ,Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar wanazo fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.1 zinazotakiwa kukopwa na wananchi kupitia vikundi mbali mbali vya ushirika. 

"Kila mwaka Serikali inatenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, lakini wanaokopa ni kidogo jambo linalosababisha fedha nyingi zirudi Serikali kuu bila ya kutumiwa na walengwa hivyo watendaji wa Wizara husika pamoja na Maafisa Ushirika watoe elimu ya kutosha kwa jamii",amesema Dk. Mabodi. 

Kupitia Majumuisho hayo Dk.Mabodi amekemea baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Chama kuacha tabia ya kuwagawa kisiasa watendaji wa Serikali za Mitaa na watakapobaini mapungufu katika utendaji wa Sekta hizo wafuate taratibu husika ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo. 

Pia amewataka baadhi ya viongozi na wanachama kuacha tabia za makundi ya kudhoofisha juhudi za CCM,na badala yake Watumie muda mwingi kuwaeleza wananchi mambo mema yanayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Akizungumzia ugatuzi Dk.Mabodi amesifu mfumo huo wa kuzipa nguvu na maamuzi Serikali za mitaa zipekeleke huduma bora kwa wananchi na kusema kuwa ugatuzi imetatua kwa kiwango kikubwa changamoto za wananchi. 

Pamoja na hayo amezipongeza Manispaa na Halmashauri kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na kuziagiza zifanyie kazi kwa wakati mapungufu mbali mbali yaliyojitokeza katika mfumo wa ugatuzi hasa kwenye nyanja za Elimu, Ukusanyaji wa mapato,Afya ,Kilimo pamoja na Mifugo. 

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa Zanzibar Mwl.Kombo Hassan mesema CCM itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kuwapelekea wananchi huduma bora zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab amesisitiza ushirikiano baina ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kusimamia vizuri mfumo wa ugatuzi ili uende sambamba na matakwa ya wananchi.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Garos Nyimbo amezitaka Taasisi hizo  kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya mfumo wa ugatuzi ili wachangamkie fursa zinazopatikana kupitia utaratibu huo.

 Akichangia hoja juu ya masuala ya kiutendaji kwa Taasisi hizo, Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Ndugu Amini Salmin Amour, amezishauri Manispaa na Halmashauri zote nchini kuweka mifumo imara na ya kisasa katika ukusanyaji wa kodi kwa lengo la kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato.

Pia  MNEC Amini, amewataka watendaji wa Taasisi hizo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na waanzishe mfumo maalum wa kielectroniki wa kuhifadhi kumbukumbu zote za vyanzo vya mapato pamoja na miradi yote ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohusu taasisi hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi  Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud  amesema changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika Manispaa zote zilizomo katika Mkoa anaoungoza atahakikisha zinafanyiwa kazi kwa haraka.