Jumapili, 13 Agosti 2017

Dkt. SHEIN "Serikali nnayoiongoza itahakikisha inawapelekea huduma za afya, umeme, maji safi na salama, elimu na barabara ndani ya miezi sita ijayo."

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewahakikishia wananachi wa vijiji vya Mbuyumaji na Mlilile Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inawapelekea huduma za afya, umeme, maji safi na salama, elimu na barabara ndani ya miezi sita ijayo.

Dk. Shein ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti mara baada ya kuvitembelea vijiji hivyo vilivyopo Wilaya ya Kaskazini A, ambapo aliwataka Mawaziri husika wa sekta hizo kuhakikisha huduma hizo muhimu zinawafikia wananchi hao katika kipindi hicho.

Dk. Shein alieleza kuwa kilio cha wananchi wa vijiji hivyo amekisikia na kuwaahidi juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha huduma hizo muhimu zinapatikana.

Nao Mawaziri wa sekta hizo pamoja na Mawaziri wengine aliofuatana nao Dk. Shein, wameahidi kutekeleza agizo hilo kwa wakati na kutumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi.

Wananchi wa maeneo hayo walielezea kufurahishwa kwao na ziara ya Rais wa Zanzibar na kueleza matumaini yao makubwa kutokana na ziara hiyo ya Dk. Shein katika vijiji vyao na kufarajika na ahadi zake anazozitoa kwa lengo la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Mapema Dk. Shein alianza ziara yake katika Wilaya hiyo ya Kaskazini A, kwa kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Soko la Kinyasini na kuwaeleza wananchi kuwa Serikali inayoongozwa na CCM kwa mashirikiano ya washirika wa maendeleo ndio wanaojenga soko hilo na sio mwengine.

Dk. Shein amesema wananchi wengi watafaidika na ujenzi wa soko hilo kwa kupata ajira sambamba na kuwa na sehemu nzuri ya kufanyia biashara ambapo maisha yataimarika kwa familia nyingi zitakazotumia soko hilo.

Aidha, Dk. Shein ameelezea kutoridhika kwake na hali ya baadhi ya wafanyabiashara hivi sasa kuuza mazao yao pembezoni mwa barabara katika eneo hilo la soko na kueleza kuwa jambo hilo sio muwafaka.

Pamoja na hayo, Dk. Shein amewahakikishia wananchi wa kijiji hicho cha Kinyasini kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Bububu hadi Mkokotoni ambayo itaanzia Chuini na kuwa si muda mrefu ujenzi wake utaanza na kuweza kuwasaidia sana wananchi wakiwemo wa kijiji hicho na  maeneo mengine ya Mkoa huo.

Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inayogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ulieleza kuwa mradi wa ujenzi wa soko hilo utagharimu TZS Bilioni 2.5.

Mara baada ya kuweka jiwe la Msingi na kupata maelezo katika kituo cha uokozi na uzamiaji kiliopo Nungwi Dk. Shein alitoa pongezi kwa kuanza vyema mradi huu wa ujenzi wa vituo vya uokozi na uzamiaji.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Radhia Rashid Haroub alieleza kuwa Mradi huo umeanza rasmi mwaka 2014/2015 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018/2019.

 Pamoja na hayo, Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa katika kutekeleza ununuzi wa Boti katika mradi huo Serikali imetenga TZS 2.1 Bilioni kwa ununuzi wa boti mbili mpya za kisasa zenye uwezo wa kuokoa na kutoa visaidizi 600 kwa wakati mmoja kwa chombo kimoja.

Katika ziara yake hiyo pia, Dk. Shein ameweka jiwe la msingi katika Maskani ya CCM Tushikamane na kusalimiana na wanachama na wananchi katika eneo hilo na kuahidi kutoa mchango wake kwa kuliezeka pamoja na kuliweka madirisha na milango.

Akiwa katika eneo la Mkokotoni ambapo Serikali ina ampango wa kujenga bandari kwa ajili ya vyombo vya usafiri wa watu pamoja na bidhaa, Dk. Shein alipongeza hatua nzuri za matayarisho, bandari ambayo itakuwa na urefu wa mika 170 na urefu wa mita 6.

Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Shirika la Bandari, ujenzi wa Bandari hiyo ya Mkokotoni hadi kumalizika kwake utakharimu jumla ya TZS Bilioni 1.8 ambapo ujenzi wa nyumba hiyo ya Shairika hilo umegharimu jumla ya TZS milioni 378.7.

Baada ya ziara hiyo Dk.Shein alifanya majumuisho katika Ukumbi wa Hoteli ya Bravo iliyopo Kiwengwa na kusisitiza kuwa maagizo aliyoyatoa kwa wizara mbali mbali za SMZ kutafuta ufumbuzi wa haraka kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ndani ya mkoa huo.

Kupitia majumuisho hayo alizungumzia suala la uchimbaji wa Mchanga katika maeneo ya Kaskazini ‘B’ Unguja, na kuongeza kuwa serikali imeamua kusimamia zoezi la kudhibiti uchimbaji wa rasilimali hiyo kutokana na kuwepo kwa dalili za kumalizika mchanga nchini.


Pamoja na hayo aliwasihi viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali za mkoa huo kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ili viongozi waweze serikali waweze kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
























Jumamosi, 12 Agosti 2017

Dkt. Shein anza rasmi ziara yake kisiwani Zanzibar




MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  Dkt. Ali Mohamed Shein  amewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kufanya kazi za kuimarisha taasisi hiyo ya kisiasa ili ishinde na kuongoza dola katika uchaguzi mkuu ujao.
Rai hiyo ameitoa  wakati akizindua Tawi la CCM la Kitope ‘B’  jimbo la Mahonda kwenye ziara yake ya kukagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo aliyoianza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dkt. Shein alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa kutumia vyema ofisi za Tawi hilo ambalo ni la kisasa kwa lengo la kutekeleza kwa ufanisi kazi za kisisaa zitakazozaa matunda ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Kwanza nakupongezeni viongozi na wanachama wote wa jimbo la Mahonda mlioshiriki kujenga tawi hili la kisasa linaloendana na hadhi ya chama chetu kimaendeleo kwani lina ofisi zote ambazo ngazi zote kiutendaji ndani ya tawi mtafanya kazi zenu kwa utulivu.

Pia nasaha zangu kwenu ni kwamba uchaguzi mkuu unakaribia haupo mbali hivyo tumieni ofisi hii vizuri kuchapa kazi kwa bidii sambamba na kuongeza wanachama wapya ambao ndio mtaji wetu mkubwa wa kisiasa ili kuhakikisha 2020 tunashinda.”, alisisitiza Dkt. Shein.

Aidha alisema kuwa lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inayotokana na CCM ni kuimarisha huduma zote za kijamii na kiuchumi ili wananchi wa mijini na vijijini waweze kunufaika na fursa hizo.

Dkt.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea ujenzi wa kituo kipya cha mashine za kutibia maji kinachojengwa katika eneo la Donge mbiji ambapo mradi huo uliofadhiliwa na serikali ya China utagharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 5.5.

Katika ziara hiyo  Dkt. Shein alitembelea  shamba la  karafuu  na  kuzungumza  na mliki wa mradi wa kilimo cha karafuu huko Donge  Pwani, Haroun Abou Mbarouk alieleza kuwa shamba hilo lenye mikarafuu zaidi ya 170 limekuwa likizalisha zao hilo kwa wingi ambapo kwa mavuno ya mwaka wanapata zaidi ya gunia 25.

Sambamba na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea mradi wa ujenzi wa tangi la Maji huko Donge Kisongo unaojengwa na mafundi  kutoka jamhuri ya watu wa China utakaowanufaisha  wananchi  wa Wilaya ya Kaskazini “B”  na maeneo jirani.

Ziara hiyo itaendelea kesho katika Wilaya ya Kaskazini  ‘’A” Unguja ambapo Dkt.Shein ataweka  mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya kijamii na kuhitimisha kwa hotuba ya majumuisho ndani ya Mkoa huo.